Dar es Salaam. Raia 119 wa Burundi na Malawi, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kuwepo Tanzania bila kuwa na kibali.
Kati ya washtakiwa hao, 76 ni raia wa Burundi na 43 wa Malawi na wamefunguliwa kesi tatu tofauti katika mahakamani hiyo.
Washtakiwa walifikishwa mahakama hapo jana Jumanne, Desemba 24, 2024 na kusomewa mashtaka saa 12:00 jioni na wakili wa Serikali kutoka Uhamiaji, Rapahel Mpuya akisaidiana na Hadija Masoud, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini.
Washtakiwa 43 raia wa Malawi walisomewa mashtaka katika kesi ya jinai namba 35730 ya mwaka 2024 wakidaiwa kuwapo nchini bila kuwa na kibali.
Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya Happy Mvula (24), Robert Mwale (35), Benson Phiri (19) na wenzao 40.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 22, 2024 eneo la Kawe wilayani Ilala.
Upande wa mashtaka umedai siku hiyo washtakiwa wakiwa raia wa Malawi walikutwa wakiishi nchini bila kibali au nyaraka yoyote inayotambulisha uhalali wao wa kuishi Tanzania.
Washtakiwa wamekiri shtaka linalowakabili isipokuwa mshtakiwa wa 33 katika kesi hiyo, Elizabeth Phakat ambaye alikana shtaka.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hadi Desemba 30, 2024 itakapoitwa kwa ajili wa washtakiwa waliokiri kusomewa hoja za awali (PH). Washtakiwa wamerudishwa rumande hadi siku hiyo.
Katika kesi nyingine, raia 41 wa Burundi walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kujibu mashtaka.
Washtakiwa hao ni Pacifique Iribagiza (28), Nzayimana Rona (30), Eliya Selemani (21), Paulo Msheli (40), Hamenyimana Selji na wenzao 36. Wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 35729 ya mwaka 2024 iliyo mbele ya hakimu Mhini.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 21, 2024 katika maeneo ya Ilala na Temeke. Wanadaiwa wakiwa raia wa Burundi, walikuta wakiishi Tanzania bila kibali au nyaraka inayoonyesha uhalali wao wa kuwa nchini.
Washtakiwa wote wamekiri shtaka. Upande wa mashtaka utawasomea PH Desemba 30, 2024 na wamerudishwa rumande.
Katika kesi ya tatu, raia 35 wa Burundi wanadaiwa kuwepo nchini kiyume cha sheria.
Washtakiwa katika kesi ya jinai namba 35670/2024 ni Bikolimana Desire (32), Shimirimana Trasis (32), Said Jafari (40), David Erick (25), Mukowimana Bienvenue (27) na wenzao 30.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 19, 2024 katika eneo la Jangwani, wilayani Ilala.
Wakiwa raia wa Burundi, wanadaiwa walikutwa wakiishi nchini bila kuwa na kibali au nyaraka inayotambulisha uhalali wao wa kuwepo Tanzania.
Washtakiwa wamekiri shtaka. Hakimu Mhini ameahirisha kesi hadi Desemb a 30, 2024 itakapoitwa kwa ajili wa washtakiwa kusomewa hoja za awali. Washtakiwa wamepelekwa rumande.