KOCHA wa KenGold, Omary Kapilima amesema minne ijayo ya Ligi Kuu Bara ndiyo itakayotoa hatma ya kikosi hicho kama kitasalia msimu ujao au kitashuka daraja.
Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 2-1 jana na Singida Black Stars ikiwa ni kichapo cha 12 katika michezo 16 iliyocheza, baada ya kushinda mmoja na kutoka sare mitatu ikisalia mkiani na pointi sita.
“Nafikiri michezo minne ijayo itatoa taswira ya sehemu tuliyopo kama kweli tutaweza kujitoa huku mkiani, ingawa naamini tuna nafasi nzuri ya kurekebisha kasoro ikiwa tutafanya maboresho makubwa kikosini,” alisema beki huyo wa zamani wa kimataifa aliyetamba na Yanga, Mtibwa Sugar, Majimaji na Taifa Stars.
Kapilima aliongeza jambo linalompa matumaini ni uongozi kumuahidi kufanyia kazi ripoti ya usajili, huku akidai kitendo cha kutokuwa na mchezo wowote hadi Januari 22, mwakani kitasaidia kupunguza presha kwa wachezaji. Timu hiyo haitakuwa na mchezo hadi Januari 22 itakapocheza na Yanga jijini Dar es Salaam, baada ya kuchapwa bao 1-0 mzunguko wa kwanza, kisha itaikaribisha nyumbani Fountain Gate Januari 26.
Baada ya hapo kitaifuata Tabora United, Januari 29, kisha kurejea nyumbani kuwakaribisha Kagera Sugar Machi 3.
Kocha huyo alijiunga na kikosi hicho Oktoba 22, mwaka huu akichukua nafasi ya Fikiri Elias aliyeondoka Septemba 17.
Tangu akabidhiwe kikosi, Kapilima amekiongoza katika mechi nane za ligi ambapo hakijashinda yoyote, kwani kimepoteza sita na sare mbili.
Timu hiyo mara ya mwisho kushinda ulikuwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania Oktoba 4, mwaka huu ukiwa ni pekee hadi sasa katika michezo 16 ya Ligi Kuu iliyocheza baada ya kutoka sare mitatu na kuchapwa 12.