Wafungwa 1,500 watoroka Maputo katika machafuko ya uchaguzi – DW – 25.12.2024

Mkuu wa Polisi Bernardino Rafael amesema jumla ya wafungwa 1,534 walitoroka kutoka gereza lenye ulinzi mkali lililoko umbali wa takriban kilomita 15 kutoka mji mkuu Maputo.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, alibainisha kuwa kati ya waliokuwa wakijaribu kutoroka, 33 waliuawa na 15 walijeruhiwa katika makabiliano na walinzi wa gereza. 

Operesheni ya kuwasaka wahalifu hao, ikisaidiwa na jeshi, imesababisha kukamatwa kwa takriban 150 kati ya waliotoroka.

Soma pia: Watu 21 wauawa katika machafuko Msumbiji baada ya uamuzi wa mahakama

Takriban wafungwa 30 kati yao walihusishwa na makundi yenye silaha ambayo yamekuwa yakisababisha machafuko na mashambulizi katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado kwa kipindi cha miaka saba. 

Msumbiji| Bernardino Rafael | Mkuu wa Polisi
Mkuu wa Polisi ya Msumbiji Bernardino Rafael.Picha: Amós Fernando/DW

“Tunahofia sana hali hii,” alisema Rafael. 

Mahakama ya juu kabisa nchini humo ilithibitisha Jumatatu kuwa chama tawala cha Frelimo, ambacho kimekuwa madarakani tangu 1975, kilishinda uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 9, uchaguzi ambao tayari ulisababisha wiki kadhaa za machafuko. 

Kundi la waandamanaji lilijitokeza karibu na gereza hilo Jumatano, likisababisha hali ya taharuki na machafuko ndani ya gereza, ambapo wafungwa walibomoa ukuta na kutoroka, alieleza. 

Mabaki ya vizuizi barabarani bado yalikuwepo katika maeneo kadhaa ya mji mkuu Jumatano, yakizuia harakati, huku vitendo vya uharibifu vikiendelea.

Mbali na maduka na majengo ya umma yaliyoporwa Jumatatu, magari ya wagonjwa yalichomwa moto pamoja na duka la dawa na biashara nyingine, kwa mujibu wa mwandishi wa AFP. 

Polisi yatawanya waandamanaji kwa gesi ya machozi Msumbiji

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Uthibitisho wa matokeo ya uchaguzi Jumatatu ulifanyika licha ya madai ya dosari kutoka kwa waangalizi wengi. 

Soma pia: Baraza la katiba laidhinisha matokeo ya uchaguzi Msumbiji

Mgombea wa Frelimo, Daniel Chapo, alipata asilimia 65.17 ya kura, takriban alama tano chini ya matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya taifa hilo.

Mpinzani mkuu wa Chapo, kiongozi wa upinzani aliye uhamishoni, Venancio Mondlane, amedai kuwa uchaguzi huo ulichakachuliwa, na kuzua hofu ya machafuko kati ya wafuasi wa vyama pinzani. 

Machafuko hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 150, kulingana na ripoti za mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali.

Related Posts