RC Tanga ataka udhibiti utoroshaji madini Horohoro

Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amezitaka taasisi na mamlaka zinazosimamia Kituo cha Huduma Jumuishi cha Horohoro kufuatilia na kudhibiti utoroshaji wa madini ya vito kwenye eneo hilo kwa kuwa kunaikosesha Serikali mapato.

Akizungumza na watumishi wa taasisi na mamlaka zaidi ya 17 zinazosimamia Kituo cha Huduma Jumuishi Horohoro leo Ijumaa Mei 10, 2024, mkuu huyo wa mkoa amesema kuna taarifa za utoroshaji wa madini ya vito kwenda Kenya, hivyo udhibiti ufanyike ili hayo yasitokee.

Amesema sehemu zote muhimu ambazo viongozi hao wanahisi zinatumika kupenyeza madini, mamlaka zilizopo ndani ya mpaka wa Horohoro zihakikishe zinasimamia na kudhibiti hilo haraka.

Pia, ameagiza udhibiti wa raia wa kigeni wanaoingia nchini kwa njia zisizo za halali na mbinu mpya za kuingia wageni kwa kuingizwa kwenye magari ya mafuta au makontena njia hizo zithibitiwe.

“Suala lingine ni udhibiti wa uingiaji wa dawa za kulevya nchini kupitia border ya Horohoro,kuna wengine wanaruhusu baadhi ya dawa ila kwa Tanzania ni makosa,hivyo lazima udhibiti uwepo wa madawa hayo ya kulevya,”amesema Batilda.

Pia,  kwa Bandari ya Tanga amesema Serikali inaweka utaratibu eneo hilo liwe maalumu kwa kusafirisha mazao ya kilimo,hivyo bidhaa zote za kilimo zitakuwa zinasafirishwa kupitia bandari hiyo.

Ofisa Mfawidhi Kituo cha Huduma Jumuishi Horohoro, Shadrack Mbonea amesema hali ya mpaka ipo salama na ufanisi wa ukusanyaji kodi umekuwa mzuri na kufikia asilimia 117.

Amesema kwa kuanzia Julai mwaka jana mpaka Aprili 2024, kituo hicho kimekusanya Sh68.5 bilioni na kuvuka lengo ambalo wamewekewa na Serikali la kukusanya Sh58.4 bilioni.

Kaimu Meneja Bandari ya Tanga, Peter Milanzi amesema kuna ongezeko la shehena katika bandari hiyo baada ya Serikali kutoa Sh429 bilioni kwa ajili ya kuongeza kina na upana wa eneo la bandari.

Amesema ndani ya miezi saba wameweza kuhudumia kiwango cha tani zaidi ya 950,000 , kinyume na mwaka uliopita.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Burian alikuwa kwenye ziara ya kujitambulisha maeneo hayo, ambayo ni moja sehemu umuhimu za kiuchumi kwa mkoa huo.

Related Posts