Baleke ndo basi tena Yanga

SIKU chache baada ya Mwanaspoti kuweka bayana kwamba straika wa Yanga, Mkongomani Jean Baleke amekalia kuti kavu katika kikosi hicho, sasa imethibitishwa kwamba ndoa ya pande hizo mbili imeisha baada ya kukabidhiwa barua yenye maumivu akisitishiwa mkataba wake wa mkopo akitokea TP Mazembe.

Tayari klabu hiyo imeanza msako wa kuleta mashine mpya kuziba nafasi ya Baleke aliyewahi kukipiga Simba na kucheza soka la kulipwa huko LIbya kabla ya Yanga kumchukua katika dirisha kubwa, Agosti mwaka huu.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, Baleke ameshapokea uamuzi wa klabu yake ikisitishia njiani mkataba wake wa mkopo.

Tangu atue Yanga, mchezaji huyo amekuwa akikosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi hicho akifanikiwa kufunga bao moja pekee.

Bosi mmoja wa juu wa Yanga alilithibitishia Mwanaspoti kuwa benchi la ufundi la timu hiyo limeshindwa kukubaliana na ubora wa mshambuliaji huyo na kufikia uamuzi huo.

“Unajua kila kocha amekuwa na mtazamo wake na kitu kibaya wote wanaona ubora wake hawakubaliani nao na sasa hivi karibuni yeye mwenyewe ameshindwa hata kuendelea kwenda mazoezini,” alisema bosi huyo.

Bosi huyo alifichua kwamba kuna msako wa haraka umeshaanza ukiwahusisha viongozi na kocha Sead Ramovic ukisaka mshambuliaji mpya.

“Tumeshaanza kazi ya kutafuta mshambuliaji mpya. Kocha bado anataka mshambuliaji mwingine licha ya kuamka kwa Dube (Prince) na Mzize (Clement) tukipata sasa itakuwa vizuri zaidi,” alisema.

Kuondoka kwa Baleke kunaifanya Yanga kutegemea nguvu ya washambuliaji watatu pekee ambao ni Dube anayeongoza kwa mabao akifunga mara nne, Mzize mwenye mabao matatu huku Kennedy Musonda aliye majeruhi akifunga mara mbili.

Related Posts