MABOSI wa Namungo, umefikia makubaliano ya kuachana na aliyewahi kuwa beki wa Yanga, Djuma Shaban akiungana na nyota wengine watatu.
Djuma aliyeitumikia Yanga kwa mafanikio akicheza misimu miwili na kutwaa mataji ya ligi na kucheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika ameitumikia Namungo kwa miezi sita.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo Ally Suleiman alisema ni kweli wamefikia makubaliano ya pande mbili za kuachana na beki huyo na sasa wapo katika mchakato wa kutafuta mbadala wake kikosini hapo.
Suleiman alisema mbali na Djuma pia wameachana na Raphael Daud waliyemchukua kwa mkopo kutoka Singida Black Stars, Moubacrak Amza alichukuliwa kwa mkopo kutoka Kagera Sugar na Ritch Nkoli.
“Ni kweli tumefikia makubaliano ya kuachana na wachezaji hao ambao wengi wao kwa asilimia kubwa tulikuwa nao baada ya kuwachukua kwa mikopo kutoka timu mbalimbali ni Djuma pekee ambaye tulimsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja,” alisema.
“Djuma tumefikia makubaliano ya kuvunja mkataba.”
Suleiman alisema baada ya kuwaondoa wachezaji hao wameongeza wengine kwa mkopo akiwemo Najim Mussa kutoka Singida BS, Emmanuel Charles kutoka Kagera Sugar na usajili wa Derrick Mukombozi.
“Licha ya kuongeza wachezaji ambao tayari tumewatambulisha tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji eneo la ushambuliaji na ulinzi mambo yakienda vizuri tutawatambulisha.”