Ubunge viti maalumu; Wadau wataka ukomo wa muda

Wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, wadau wamependekeza ukomo wa muda kwa wabunge wa viti maalumu, wakitaka iwe ni vipindi viwili vya miaka mitano pekee ili kutoa nafasi kwa wabunge hao kwenda kugombea majimboni.

Suala hilo limeibua mjadala mpana ambapo baadhi ya wanasiasa, wanazuoni na wanaharakati wa haki za wanawake wanaeleza umuhimu wa kuwa na ukomo wa muda wa ubunge wa viti maalumu, ikiwemo kudhibiti rushwa kwa wabunge waliokaa muda mrefu.

Hata hivyo, mapendekezo ya wadau hao yanategemea utashi wa kisiasa katika mabadiliko ya Katiba yatakayoweka bayana ukomo huo kwa wabunge hao, tofauti na ilivyo sasa ambapo hakuna ukomo wa muda.

Itakumbukwa kwamba Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba ilipendekeza kuwepo kwa vipindi vitatu vya ubunge ili kuwapa nafasi watu wengine kuwatumikia wananchi badala ya kufanya nafasi hiyo kukaliwa na baadhi ya watu kwa muda mrefu.

Tume hiyo ya Jaji Warioba ilipendekeza kufutwa kwa nafasi ya viti maalumu bungeni. Rasimu hiyo pia ilipendekeza kuwapo kwa nafasi tano za uteuzi, zibaki kwa Rais ambazo zitahusisha makundi maalumu ya watu wenye ulemavu pekee.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji anataka ubunge viti maalumu uwe na ukomo wa miaka miwili kama ilivyo kwa nafasi ya Rais.

Akizungumza kwenye kongamano la wanawake na uongozi lililofanyika jijini Dar es Salaam, Meghji anasema kipindi wanaenda kwenye mkutano wa Beijing, miaka 30 iliyopita, moja ya mambo waliyoyapambania ni pamoja na ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

Anasema ukilinganisha na miaka hiyo, kwa sasa kuna mabadiliko kwa wanawake kuteuliwa katika ngazi mbalimbali, zikiwemo wizara nyeti.

Hata hivyo, kwa upande wa viti maalumu ambavyo wanawake wamekuwa wakipewa, anasema vinapaswa kuwa na ukomo ili wengine nao waweze kuvikalia na anapendekeza angalau vipindi viwili.

“Hivi viti maalumu ambavyo vinajulikana kama viti vya upendeleo, malengo yake ilikuwa ni kuwapa uzoefu wa uongozi wanaoteliwa.

“Lakini kwa bahati mbaya wapo wanaovikalia hadi miaka 20, hii sio sawa, kwa sababu tunataka kuwajenga wanawake viongozi wengi wakiwemo vijana,” anasema Zakia ambaye aliwahi pia kuwa Waziri wa Afya na Waziri wa Maliasili na Utalii.

Anahoji kama kiti cha Rais kinakaliwa miaka kumi, kwa nini hicho cha mbunge kisikaliwe kwa muda huo na kueleza hilo linawezekana kama mamlaka zikiamua.

Hata hivyo, kutokana na mabadiliko yaliyotokea kwa wanawake, amewataka wazazi kuendelea kuona umuhimu wa kuwapeleka watoto wa kike shule ili kuwatengeneza viongozi wajao watakaolisaidia Taifa.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, wakati akizungumza na vyombo vya habari wiki iliyopita, alisema vyama vimekuwa ni muhimu kuweka utaratibu wa kuzuia watu kuwa viongozi wa maisha.

“Ubunge wa viti maalumu uliingizwa katika siasa za nchi yetu, katika vyombo vya uwakilishi wa nchi yetu, bungeni na katika halmashauri na serikali za mitaa ili kuwapatia wanawake uwezo na uzoefu wa kuwa katika nafasi za uwakilishi wa wananchi,” anasema.

Lissu anasema kwa sasa kwa kuangalia kwa macho bila hata kujiuliza zaidi kumejitokeza baadhi ya watu ni wabunge na madiwani wa kudumu wa viti maalumu.

“Kwa miaka yote wako bungeni kwa sababu wanapoondoka miaka mitano wanakuwa na fungu kubwa la fedha za kwenda kupiga kampeni na kurudi kwenye nafasi zilezile,” anasema.

Lissu anasema jambo hilo Chadema walianza kulizungumza tangu mwaka 2015 kwenye vikao vya kamati kuu na ndiye aliyeliibua kwa wakati huo akitaka kuwekwe ukomo wa viti maalumu.

“Tuweke ukomo ili tutoe fursa kwa watu wengi kujifunza, kupata uwezo na uzoefu wa kushiriki kwenye siasa ili kutekeleza azma ya kuanzishwa kwa viti hivyo,” anasema.

Lissu anajenga hoja kwamba suala hilo linashindwa kutekelezeka kwa sababu halijawekewa utaratibu kwenye Katiba ya nchi na katiba ya chama na matokeo yake linakuza baadhi ya watu kuwa haki yao ni ubunge wa viti maalumu.

“Nikishinda uchaguzi kwa nafasi ya uenyekiti, moja ya mipango yangu ni lazima tuweke utaratibu wa kurithishana viongozi, chama kwa sasa ni kikubwa, leo hatuna hofu tutakosa viongozi mahali popote,” anasema.

Lissu anafafanua kuwa kama chama kimekua lazima kuweka utaratibu wa kudhibiti viongozi kwa kuwawekea vizingiti vya kisheria na kikatiba kuweka ukomo wa madaraka.

“Ukitumikia vipindi viwili, asante sana, unapisha mwingine. Kuweka ukomo kutatuepusha na mengi na hasa wapambe wanaojitokeza hadharani kusema bila wewe hatuwezi kufika,” anasema.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Nusrat Hanje aliunga mkono hoja ya kuweka ukomo wa nafasi hizo, huku akieleza si kwa eneo hilo tu, bali hata nafasi za kugombea kwenye majimbo zinapaswa kuangaliwa.

“Nakubaliana na wanaokuja na hoja ya kuweka ukomo na si kwenye upande wa viti maalumu pekee, bali hata kwa wabunge wa upande wa majimbo hata tukiweka miaka 15 au 20 itakuwa sawa,” anasema.

Hanje anasema siasa za Afrika ni biashara, kadiri mtu anavyoendelea kukaa madarakani anakuwa na misuli maeneo yote katika kutengeneza mtandao na uwezo wa kiuchumi.

“Kuna tofauti kubwa kwa mtu anayeingia kwenye kinyang’anyiro kwa mara ya kwanza na akiwa anaingia mara ya nne, ukiingia mara ya kwanza watu wanakushangilia na kukufurahia,” anasema.

Mbunge huyo wa viti maalumu anasema malengo ya kuanzishwa kwake ilikuwa kuwajengea uwezo wanawake ili waongezeke kwenye nafasi za uamuzi, lakini Tanzania hakuna chama kilichoweka ukomo katika nafasi hizo.

“Ilikuwa busara kuwe na ukomo kama baada ya miaka 10 waachie wengine, kama kumjengea mtu uwezo huwezi kufanya hivyo kwa miaka 20 lazima ifikie hatua ahitimu ili tuone tija kutoka kwake,” anasema.

Hanje katika maelezo yake, anasema suala la kuweka ukomo kwa viti maalumu vya ubunge na udiwani ni zuri na vyama vya siasa vinapaswa kulazimishwa kwa kufanya mabadiliko ya kikatiba au sheria ya vyama vya siasa.

“Kama itashindikana kuweka ukomo, ifike muda nafasi hizo zifutwe, itaonekana haina maana na badala yake tuongeze majimbo mengine au majimbo kubadilika kuwa wilaya ili kuwe na mbunge wa jinsia ya kiume na kike,” anasema.

Kwa upande wake, mbunge wa viti maalumu (CCM), Zulfa Mmaka Omar kutoka Chakechake, Pemba huko Zanzibar, anasema kwa kuwa ni mnufaika kwenye nafasi hiyo, hawezi kutoa maoni yake kwa undani.

“Nikizungumza chochote inaweza kuwa ushahidi, ngoja tukiachie chama kiamue nini kinafaa, wakiona haifai waondoe, lakini wakiona inafaa, itakuwa sawa,” anasema Zulfa.

Diwani wa viti maalumu (CCM) Kata ya Kishili jijini Mwanza, Magreth Kuhanwa anasema ukomo wa ubunge wa viti maalumu ni sahihi, ingawa mbunge akiambiwa amekaa miaka mingi, atanuna.

“Ukomo ni sawa, hakuna chenye mwanzo kikakosa kuwa na mwisho, hata mtu huwa anaanza kutambaa, kutembea, unaweza kuwa diwani kwa miaka 10, angalau ikifika miaka 15 awaachie na wengine wachukue kijiti,” anasema.

Magreth anasema hilo ni jambo jema kupisha mawazo mapya, huku akijenga hoja kwamba hata makazini kuna watu wakifikisha miaka 60 wanastaafu, japo ukweli unauma, ndiyo maana hata urais una ukomo,” anasema.

Wanasiasa, wanazuoni walonga

Mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda anasema chama hicho kimejiwekea utaratibu wa kupata viongozi wa namna hiyo.

“Ni lazima vikao vikaliwe na kujadili namna ya kuwapata viongozi au wabunge wa viti maalumu na utaratibu huo ulishapitishwa na siwezi kuzungumzia tena lolote juu ya hapo kuhusu ukomo,” anasema.

Chatanda anasema utaratibu uliopo sasa haujazungumza chochote kuhusu ukomo, isipokuwa unaeleza kutakuwa na viongozi wa viti maalumu kupitia chama hicho.

“Chama cha Mapinduzi kitakuwa na wabunge wa viti maalumu vya wanawake, lakini umefafanua kutakuwa na nafasi ya wenye ulemavu, vyuo vikuu, asasi za kiraia, kundi la vijana na wa mikoani,” anasema.

Alipotakiwa kueleza maoni nje ya msimamo wa chama hicho, Chatanda alidai hawezi kufanya hivyo ka madai kwamba akieleza vikao vya chama bado havijafanyika na si busara kwa sasa kueleza maoni yake binafsi.

Wakili wa kujitegemea, Faraji Mangula anasema kuweka ukomo wa viti hivyo ni muhimu na kinachotakiwa ni kuundwa kwa sheria ya kusimamia suala hilo ili na wengine wapate fursa hiyo.

“Kuwa na ukomo ni wazo zuri na linapaswa lifanyiwe kazi kwa sababu kunatakiwa watu wapokezane angalau iwe miaka 10 anapisha na wengine, kikubwa liwekewe sheria,” anasema.

Mangula anasema kuacha utaratibu huo, athari zake ni waliopo kuendelea kukumbatia nafasi hizo kila uchwao na hawaangalii kama kuna wengine wanaohitaji kupata uzoefu.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, Dk Faraja Kristomus anasema kuna matatizo mawili yanayosababisha, ikiwemo mfumo wa kuwapata wagombea wa viti maalumu kwa baadhi ya vyama umekuwa na fiche.

“Mchakato chini unaweza kuwa wazi, lakini ukishafika ngazi ya kufanya uamuzi, nani apate na nani asipate, ni kama vile hauko wazi na ni changamoto ya kwanza, lakini ingelikuwa wazi upatikanaji wake ingekuwa rahisi,” anasema.

Dk Kristomus anasema jambo la pili nafasi za viti maalumu ni kama zimetengwa kwa ajili ya wenza wa wanasiasa fulani na imekuwa ikiibua malalamiko mengi kuhusiana na tija yake.

“Ni tuhuma ambazo huwezi kuzithibitisha, lakini ikifika mahali mtu anaanza kutaja majina na mwenza wa fulani, ukipata majina mawili, matatu inakufanya kuanza kupata mashaka huenda malalamiko hayo yakawa ya kweli,” anasema.

Katika maelezo yake, Kristomus anasema kinachoonekana watendaji wa kisiasa kwenye hivyo vyama hawana mishahara, sasa huwa wanawatunuku wenza wa wanasiasa hao ili walau familia iweze kupata chanzo cha mapato.

“Kingine ni kukosekana kwa usimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Sheria iliyotungwa ina vipengele vinavyoviagiza vyama vya siasa kusimamia viti maalumu, sasa nadhani kama kuna kasoro irekebishwe kuwekwe ukomo,” anasema.

Related Posts