Mafuriko yatikisa Bukoba, binti afariki dunia kwa kusombwa na maji

Bukoba. Binti mmoja mwenye umri wa miaka 19 amefariki dunia kwa mafuriko yaliyoukumba mji wa Bukoba mkoani Kagera kutokana na  mvua zinazoendelea kunyesha.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kagera, Zabron Muhumha leo Ijumaa Mei 10, 2024, amethibitisha kutokea kwa kifo cha mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Leah.

Msichana huyo aliyebainika kuwa mkazi wa Mtaa wa Kasarani Kata ya Bakoba, amefariki dunia baada ya kusombwa na maji wakati akitoka nje kuchuka maji huku mvua ikinyesha.

Zabron amewataka watu wote ambao wapo kando ya Mto Kanoni na mwambao wa Ziwa Victoria kuhama maeneo hayo ili kuepukana na madhara yanayoendelea kujitokeza kutokana mvua zinazoendelea kunyesha.

“Baadhi ya barabara na maeneo tumezuia watu kupita na kuingia kipindi hiki cha mvua na hadi sasa kifo kimoja kimetokea, binti ameenda kuchota maji akateleza na kusombwa na maji, nyumba zimezingirwa na maji, barabara hazipitiki.

“Niombe wananchi wote wachukue tahadhari ya kuhama maeneo hatarishi kuepuka athari za mafuriko. Tunaendelea na uokoaji, bado hatujabaini nyumba ngapi zimeathirika na mali, pia zilizosombwa,” amesema Zabron.

Mwendesha bodaboda, Elisha Elia amesema wameanza kukosa kipato kwa kuwa mafuriko yamezingira barabara, hakuna sehemu ya kupita.

Ameiomba Serikali kutafuta suluhisho la kujenga kingo za Mto Kanoni ambao umekuwa kichocheo cha mafuriko katika mji huo.

Taufik Salumu, Diwani wa Bilele amesema siyo mara ya kwanza maeneo ya kata yake kuathiriwa na mafuriko maana kila mwaka inakuwa hivyo, lakini kutokana na tahadhari zilizotolewa na vyombo vya habari wamejiandaa vizuri ingawa mitaa ya Uhuru na Omukigusha imepata madhara ya maji kuingia kwenye nyumba na kusababisha baadhi ya mali kuharibika.

Katibu wa mbunge wa Bukoba Mjini, Pasaka Bakari amesema kila mwananchi awe mlinzi wa mali za mwenziye na kusaidia ili kuokoa vitu vilivyoharibika.

Ameiomba Serikali kupitia miradi ya Tactic Mkoa Kagera ukiwamo ujenzi wa kingo za Mto Kanoni kuhimiza wahusika kuharakisha ujenzi huo kufanyika ili kuepuka madhara ya mafuriko.

Related Posts