AKILI ZA KIJIWENI: Vita ya mastraika Ligi Kuu sio mchezo

MSIMU uliopita nyota wawili wanaocheza nafasi ya kiungo, Feisal Salum na Stephane Aziz Ki ndio walishindana katika kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu.

Mshindi wa kinyang’anyiro hicho akawa ni Stephane Aziz Ki ambaye alimaliza msimu akiwa amefunga mabao 21 na Feisal Salum akamaliza katika nafasi ya pili akifumania nyavu mara 19.

Hapa kijiweni kukaibuka makundi mawili yaliyopishana mitazamo ambapo moja lilishangazwa na kuwalaumu wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji kwamba kukosa kwao ubora ndio kuliwapa fursa viungo kutawala katika kufumania nyavu.

Kundi la pili likawatetea washambuliaji kwa hoja kwamba soka la kisasa limefanya washambuliaji wasiwe wanafunga sana na kwamba makocha wanawatumia kufanya mikimbio ambayo inachangia wengine kupata mabao.

Hata hivyo mwisho wa siku tukakubaliana kwamba tuupe nafasi muda tujiridhishe ni kundi gani kati ya hayo mawili hapa kijiweni limekuwa na mtazamo sahihi na ambalo halijawa na mtazamo sahihi.

Baada tu ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, kundi la kwanza ambalo lilikuwa linaamini kwamba washambuliaji hawakutamba msimu uliopita kwa sababu ya udhaifu wao, linaelekea kuibuka kidedea.

Ukitazama chati ya wanaowania zawadi ya ufungaji bora wa ligi kuu msimu huu, utaona katika watano wanaoongoza, washambuliaji ni wanne na kiungo ni mmoja tu.

Na washambuliaji hao wameonekana kujitahidi kuwa na muendelezo wa kufunga tofauti na msimu uliopita ambapo mchezaji anaweza kufunga mechi moja akaja kuonekana akifunga tena baada ya mechi tano au sita au hata zaidi ya hapo.

Mwisho wa siku tunaelekea kuamini kwamba msimu jana washambuliaji halikuwa suala la mifumo ya makocha wala nini bali ni udhaifu wao tu wa kutoweza kutumia nafasi.

Related Posts