Na Mwandishi Wetu
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia kwa kishindo na kwa asilimia mia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Maji yenye jumla ya Shilingi 627,778,338,000 ili kwenda kutekeleza kazi na shughuli mbalimbali za Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso (Mb) akichangia hoja hiyo kabla ya kupitishwa Bungeni amesema Wizara ya Maji imejipanga kuwa mfano kwa Tanzania kwa kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuwahudumia wananchi.
Ametolewa mfano wa Hatifungani ya Kijani iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kupitia Mamlaka ya Majisafi Tanga (Tanga UWASA).
Waziri Aweso ameweka wazi kuwa Wizara ya Maji ilikuwa eneo la malalamiko na kero ila hivi sasa ni neema akisema miradi ya maji iliyokwama tangu miaka ya 70 hivi sasa imekamilishwa na wananchi wanapata huduma ya maji.