Dar es Salaam. Hatimaye Kikosi cha Saba cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kilichokuwa kikihudumu katika mpango wa Ulinzi wa Amani, Jamhuri ya Afrika ya Kati chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (Minusca), kimerejea nchini salama.
Kikosi hicho kilipokelewa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi kilichopo Mapinga na ujumbe kutoka Makao Makuu ya Jeshi ukiongozwa na Brigedia Jenerali George Itang’are, kwa niaba ya Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum Haji Othman.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Brigedia Jenerali Itang’are amewapongeza wapiganaji hao kwa kuliwakilisha jeshi na nchi kwa ujumla.
Amesema licha ya changamoto ndogo ndogo za kiutawala walizokutana nazo, lakini waliweza kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa.
“Ninathamini ushiriki wenu katika jukumu hili, mmeweza kupata uzoefu unaotokana na nguzo tatu muhimu za mwanajeshi: utiifu, uaminifu na uhodari,” amesema Brigedia Jenerali Itang’are.
Hata hivyo, amewakumbusha askari hao kutumia mitandao ya kijamii kwa namna chanya, na wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa ari na nguvu mpya.
“Nawapeni pole kwa kutengana na familia zenu kwa muda mrefu na kuwatakia kipindi chema cha kuungana nao tunapoendelea kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka,” amesema.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo ya mapokezi, Kamanda wa Kikosi hicho, Luteni Kanali Joseph Mushilu alikabidhi cheti ambacho kikosi kilitunukiwa na Umoja wa Mataifa kwa kutambua mchango wao katika kuwalinda raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuimarisha hali ya usalama katika taifa hilo.
Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na imekuwa ikichangia walinda amani, maofisa wanadhimu, na wataalamu wa kijeshi katika maeneo mbalimbali duniani.
Hivi sasa wanajeshi wa Tanzania wanaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika nchi za Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Lebanon na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kikosi hicho kilikuwa na maofisa na askari zaidi ya 560, wakiume na wa kike.