Djuma avunja ukimya Namungo | Mwanaspoti

BAADA ya kuitumikia Namungo kwa muda wa miezi sita kabla ya kutangazwa kutemwa, beki wa zamani wa AS Vita na Yanga, Djuma Shaban amefunguka sababu za kuvunja mkataba na Wauaji wa Kusini hao akisema ni kushindwa kutumika mara kwa mara kikosini.

Namungo, ilithibitisha kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na Djuma aliyejiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akiwa mchezaji huru, licha ya awali kujifua na Azam kisha kuhusishwa na Coastal Union ilipokuwa chini ya kocha Mwinyi Zahera aliyetimkia Namungo na ndiye aliyemsajili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Djuma alisema kukaa nje kwa muda kutokana na kuuguza majeraha ni sababu ya yeye kuomba kujiweka pembeni kwa muda ili kujiweka katika utimamu mzuri.

“Tangu nimejiunga na Namungo sina mwendelezo mzuri wa kucheza, hiyo haikuwa afya kwangu na kwa timu kwa vile walinisajili ili nicheze, naamini katika upambanaji na kucheza,” alisema Djuma na kuongeza;

“Nimeamua kujipumzisha kwa muda ili kujiweka kwenye utimamu mzuri nitarudi tena kucheza nikiwa imara na nitacheza kwa mafanikio.”

Akizungumzia ligi kwa ujumla, Djuma alisema imezidi kuwa ngumu msimu hadi msimu na imekuwa chachu ya kuimarisha ubora wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali.

“Nimecheza misimu miwili nikiwa na Yanga sasa nimemalizana na Namungo kuna utofauti mkubwa nimeuona, kuna mabadiliko ya timu na timu pia kuongezeka kwa wachezaji wa kigeni kwa timu tofauti,” alisema beki huyo aliyefunga bao pekee wakati Yanga ikifunga USM Alger katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023.

Related Posts