Shirika la habari la serikali – SANA limesema vikosi vya usalama vilifanya msako dhidi ya wapiganaji wanaomuunga mkono Assad katika mkoa wa magharibi wa Tartus, na kuwauwa wanamgambo kadhaa.
Shirika linalofuatilia hali nchini Syria, Syrian Observatory for Human Rights limesema wapiganaji watatu wanaohusishwa na serikali ya Assad waliuawa kwenye operesheni hiyo.
Imefanywa siku moja baada ya maafisa 14 wa polisi wa serikali ya mpito na wapiganaji watatu kuuawa katika makabiliano yaliyozuka kwenye mkoa huo.
Yalitokea wakati vikosi vya ndani vilijaribu kumkamata afisa mmoja wa utawala wa Assad.
Shirika hilo lenye makao makuu yake nchini Uingereza limesema Mohammed Kanjo Hassan, alikuwa afisa wa sheria wa kijeshi aliyetoa hukumu za kifo na za kiholela dhidi ya maelfu ya wafungwa katika gereza kuu la Saydnaya.
Watu wa Syria bado wanawatafuta wapendwa wao baada ya kuanguka utawala wa Assad
Gereza la Saydnaya, eneo kulikofanywa mauaji ya kiholela, mateso na watu kutekwa, lilidhihirisha ukatili uliofanywa dhidi ya wapinzani wa Assad.
Hatma ya mamia kwa maelfu ya wafungwa na wale waliotoweka imebakia moja ya urathi wa kutisha wa utawala wa Assad.
Wakati mapambano ya kuuangusha utawala wa kiongozi huyo, kundi la waasi linaloshikilia sasa madaraka nchini Syria la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) lilifungua milango ya jela na vituo vya ukamataji watu kote nchi humo na kuwaruhusu maelfu ya watu kutoka.
Katikati mwa mji mkuu, Damascus, ndugu wa baadhi ya wale waliopotea wamebandika mabango ya picha za wapendwa wao, kwa matumaini kwamba kuangushwa kwa utawala wa Assad, kutawawezesha kufahamu yaliyowafika jamaa zao.
Mataifa yenye nguvu duniani na mashirika ya kimataifa tayari yamewarai watawala wapya nchini Syria chini ya kundi la HTS kuanzisha mfumo wa utoaji haki utakaoambatana na uwajibikaji.
Lakini baadhi ya watu wa jamii ya Alawi wanahofia kwamba kuanguka kwa utawala wa Assad unawaweka kwenye kitisho cha kushambuliwa na makundi yenye hasira ya kulipiza kisasi au yanayochochewa na chuki za kikabila, kidini au kikanda,
Serikali mpya yapiga marufuku maudhui ya chuki za kikabila na kidini
Siku ya Jumatano, maandamano ya watu wenye hasira yalizuka kwenye maeneo kadhaa ndani ya Syria, ikiwemo kwenye mji wa nyumbani wa Assad wa Qardaha, baada ya kusambaa video inayoonesha eneo takatifu la jamii ya Alawi likishambuliwa.
Shirika linafuatilia hali nchini Syria, limesema mwandamanaji mmoja aliuawa na wengine watano walijeruhiwa “pale vikosi vya usalama vilipofyetua risasi kuutawanya” umati kwenye mji wa katikati mwa Syria wa Homs.
Utawala wa mpito chini ya kundi la HTS ulisema kwenye taarifa uliyoitoa kwamba shambulio kwenye eneo hilo takatifu lilitokea mapema mwezi huu, na wizara ya mambo ya ndani ikisema lilifanywa na “makundi ya watu wasiojulikana” na kwamba kusambazwa sasa video hilo kulikuwa na lengo la kuchochea hasira.
Mapema siku ya Alhamisi, wizara ya habari ya Syria ilitangaza marufuku ya kuchapisha au kusambaza “maudhui yoyote au taarifa za kibaguzi kwa misingi ya tofauti baina ya jamii za nchi hyo kwa lengo la kuchochea migawanyiko na unyanyasaji”.
Kwenye moja ya video za maandamano ya siku ya Jumatano, makundi makubwa ya watu yalikuwa yakipiga mayowe yakisema “Waalawi, Wasunni, tunataka amani”.
Kwa muda mrefu, Assad alijipambanua kama kiongozi mlinzi wa jamii za wachache kwenye taifa ambalo lina idadi kuwa ya waislamu wa madhehebu ya Sunni, lakini wakosoaji wake wanasema alitumia siasa za migawanyiko kujinufaisha kisiasa.