KOCHA msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma amesema ubora wa mchezaji mmoja mmoja wa kikosi hicho, ndio utakaoamua matokeo ya mchezo wa kesho dhidi ya Simba watakapofunga nao mwaka wakiwa nyumbani mjini Singida.
Singida iliyopo nafasi ya nne kwa sasa katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, itakuwa wenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Liti, ili kuhitimisha idadi ya mechi 15 kwa Wekundu hao wanaoongoza kwa sasa wakiwa na pointi 37 na ni mchezo wa Funga Mwaka kwa timu zote hizo zinazoundwa na mastaa walioweka rekodi kadhaa hadi sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema kikosi hicho kipo katika morali nzuri na kinataka kufunga mwaka kwa ushindi, hivyo wanaamini mchezo huo utakuwa bora na wa ushindani kutokana na timu zote kuwa kwenye kilele cha ushindi.
“Tumeshinda mechi tatu mfululizo morali ipo juu na nafurahia namna wachezaji wanavyopambana kuhakikisha timu inakuwa kwenye mazingira mazuri ya ushindani, kuhusu wachezaji kila mmoja ana nafasi ya kufanya vizuri,” alisema kocha huyo aliyewahi kuinoa Coastal Union.