Kufungiwa CS Sfaxien kwamfurahisha Fadlu, aonya Mastaa

TAARIFA kwamba Sfaxien ya Tunisia imefungiwa kucheza ikiwa na mashabiki katika mechi mbili za mwisho za Kundi A ikiwa nyumbani ikiwamo ile dhidi ya Simba, imemfanya kocha wa Msimbazi, Fadlu David kuchekelea, lakini akionya mashabiki kwamba wasibweteke kwa kuamini kucheza bila mashabiki ugenini itawabeba Tunis.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF), imedaiwa kuiadhibu klabu hiyo kutokana na vurugu zilizofanywa na mashabiki walipovaana na CS Constantine ya Algeria katrika mechi ya kwanza nyumbani ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulala 1-0, ikizuiwa kuingiza mashabiki itakapoikaribisha Simba Januari 5 na ile ya mwisho dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, mbali na faini ya Dola 50,000 (zaidi ya Sh 119 milioni) kwa kosa hilo.

Adhabu hiyo imekuja huku Sfaxien ikikabiliwa na rungu jingine sambamba na Simba kama zitakuwa na hatia kutokana na vurugu zilizotokea katika mechi yao ya kwanza Desemba 15 Kwa Mkapa ambapo Simba ilishinda 2-1 na maofisa na wachezaji wa timu hiyo kuanzisha fujo zilizopokewa na mashabiki wa Simba waliong’oa viti.

Kocha Fadlu aliliambia Mwanaspoti jana, kucheza bila mashabiki ugenini kwa timu kama Sfaxien ni nafuu kwao kwani mashabiki wa klabu za Afrika Kaskazini wanafahamika kwa mzuka, lakini bado haina maana mastaa wa Simba wabweteke na kufikiri watashinda kirahisi bila kujijituma.

“Ni taarifa nzuri kwetu, lakini bado tunapaswa kwenda kupambana kupata matokeo mazuri, timu za Afrika Kaskazini zina mashabiki wenye mizuka na kwa Simba ni nafuu, hata hivyo kwa sasa niseme ukweli akili na nguvu zetu zipo kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Singida kuliko ule wa CAF,” alisema.

Related Posts