KOCHA wa Yanga, Sead Ramovic na nahodha msaidizi wa timu hiyo, Dickson Job ni kama wametofautiana juu ya kasi na mwenendo wa timu hiyo iliyoshinda mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu tangu ilipotoka kuchemsha kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga iliyokuwa imepoteza mechi mbili za CAF za Kundi A mbele ya Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria kila moja kwa mabao 2-0, kisha kutoka sare ya 1-1 na TP Mazembe ya DR Congo imeshinda michezo ya Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa, TZ Prisons na Dodoma Jiji ikifunga mabao 11 na kufungwa mawili tu. Pia kabla ya kushinda mechi hizo mfululizo, Yanga ya Ramovic ilishinda 2-0 kwa Namungo na kumfanya awe na mechi nne mfululizo za ligi bila kupoteza tangu ampokee, Miguel Gamondi aliyetimuliwa alipopoteza dhidi ya Azam na Tabora United.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ramovic alisema, hii ndio Yanga aliyokuwa akiitaka, imeanza kucheza anavyotaka, japo hajaridishiwa na nafasi inazotengeneza na kuzitumia, ila ana matumaini.
Alisema katika mechi mbili zilizopita wamezidi kuimarika kwa kuwapa wapinzani wakati mgumu kiasi cha kushindwa kupumua kwa kuwashambulia kuanzia juu.
“Bado nataka kuona wachezaji wakiwa na njaa zaidi ya ushindi mkubwa kuliko huu wanaoupata kwa vile wana nafasi ya kufanya hivyo kwa ubora walionao. Kilichoongezeka kwa sasa ni mashambulizi yanayoanzia juu yakiwapa tabu wapinzani na hii ni moja ya kazi nzuri inayofanywa na timu,” alisema Ramovic aliyewataja wasaidizi wake, hasa wa viungo Adnan Behlulovic aliyetua karibuni.
Kwa upande wa Job, alisema licha ya matokeo mazuri katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu ikifunga mabao 13 na kufungwa mawili, bado anaona wanaendelea kujitafuta ili kufikia ubora wa misimu mitatu iliyopita walipobeba ubingwa wa ligi hiyo na Kombe la Shirikisho.
Yanga ya Ramovic katika ligi imeshinda 2-0 dhidi ya Namungo, kuilaza Mashujaa (3-2) na kushinda 4-0 dhidi ya Prisons na Dodoma, lakini Job alisema ushindi mfululizo umepandisha ubora wa kuendelea pale walipoishia, huku akiweka wazi, bado wanajitafuta ili kujijenga kiubora zaidi ya misimu mitatu iliyopita.
“Nawashukuru mashabiki kwa kuendelea kuwa nasi, kwani tulipita katika changamoto na hawakutuacha na ndiko kulitupa nguvu ya kupambana zaidi ili tuwape matokeo mazuri,” alisema Job na kuongeza;
“Tunashinda, ila nafikiri bado hatujajipata kurudi katika mstari wa ushindani, misimu mitatu nyuma tuliyotwaa mataji tulikuwa kwenye kilele cha ubora tunatamani kuvuka hapo tena ili tujijengee msimu mwingine imara zaidi.”
Job alisema misimu yote waliyokuwa bora chini ya makocha wawili waliaocha alama kuanzia Nabi Nasreddine na Gamondi na sasa chini ya Ramovic wana tumaini kubwa wakiamini watakuwa bora zaidi kadri siku zikiendelea.
“Unajua kila kocha ana ubora wake na tunajivunia.”