Medo amrudisha Amza Kagera Sugar

KLABU ya Kagera Sugar iko katika hatua za mwisho za kumrejesha aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho raia wa Cameroon, Moubarack Amza kutoka Namungo, ikiwa ni pendekezo la kocha wa timu hiyo Mmarekani, Melis Medo kwa viongozi wa klabu.

Nyota huyo anarejea ndani ya kikosi hicho kwa mara ya pili baada ya awali kujiunga nayo Januari mwaka huu kwa mkopo wa miezi sita akitokea Singida Black Stars (zamani Ihefu), kisha kuondoka msimu huu na kutua Namungo iliyotangaza kumtema pamoja na wengine wanne akiwamo Djuma Shabani na Ritch Nkolui.

Akizungumza na Mwanaspoti, Amza alisema kwa sasa asingependa kuzungumza chochote kama kweli ataondoka Namungo na kutua Kagera hadi pale atakapopata taarifa rasmi, ingawa anachokitambua yeye bado ni mchezaji halali wa ‘Wauaji wa Kusini’.

“Nafikiri kama kuna jambo lolote linalonihusu nitapewa taarifa rasmi na viongozi kwa sababu hadi sasa sijajua hatima ya kuwepo Namungo au kutolewa kwa mkopo, nakiri wazi msimu huu umekuwa ni mgumu hivyo, napambana kurejesha makali yangu.”

Mmoja wa viongozi wa Namungo ambaye aliomba jina lake kuhifadhiwa, aliliambia Mwanaspoti nyota huyo wamempeleka Kagera Sugar, ili kutoa nafasi ya kuipata saini ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Jean Baleke aliyetemwa.

Amza hadi sasa hajafunga bao lolote la Ligi Kuu Bara ingawa msimu bora kwake nchini ambao hata yeye anakiri ulikuwa wa 2022-23, wakati akiitumikia Coastal Union ambapo alimaliza msimu kwa kufunga mabao saba.

Katika kipindi chote cha miezi sita aliyoichezea Kagera alifunga mabao matatu ya Ligi Kuu huku mara ya mwisho kutupia ilikuwa ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora Utd, mechi iliyopigwa Aprili 17.

Nyota huyo anaenda kuboresha eneo la ushambuliaji la timu hiyo ambalo limekuwa butu baada ya kufunga mabao 10 tu katika michezo yake 15, huku akiungana na Edmund John kutoka Singida BS na Omary Buzungu aliyetokea Mtibwa Sugar.

Related Posts