Sakata mtuhumiwa kupigwa risasi lachukua sura mpya

Dar es Salaam. Wiki moja baada ya Mwananchi kuripoti tuhuma za ofisa wa Polisi kudaiwa kumpiga risasi Ronald Mbaga wakati akimhoji kwa tuhuma za kuiba bastola ya mfanyabiashara, mfanyabiashara huyo naye amelalamika kutotendewa haki na Polisi.

Ilidaiwa kuwa ofisa huyo wa polisi (jina limehifadhiwa) alimpiga risasi Mbaga akiwa anamhoji nyumbani kwake, lakini madai hayo yamekanushwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi akidai kuwa kijana huyo alichomwa bisibisi na vijana wenzake akiwa kwenye mgodi wa madini ya Tanzanite.

Hata hivyo, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi walituma timu ya wapelelezi kufuatilia sakata hilo.

Kamanda Katabazi alipoulizwa juzi kuhusu malalamiko ya mfanyabiashara huyo, alisema hawezi kuzungumzia kwa kuwa yuko nje ya kituo chake cha kazi.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana, mfanyabiashara huyo wa madini, Samson Mollel anayeishi Mirerani Wilaya ya Simanjiro, amesema baada ya kubaini nyumba yake imevunjwa kwenye dirisha na kuibiwa vitu, ikiwemo bastola na televisheni, alipata taarifa za watu waliohusika.

“Baada ya tukio hilo tulikwenda Polisi kuripoti, baada ya hapo nikamkuta tena yule kijana nyumbani kwake akiwa na askari polisi. Nikamwambia kwamba mimi sihitaji hiyo TV basi anipe tu nyara (bastola) ya Serikali.”

“Yule kijana alikiri kwamba amevunja nyumba na walikuwa wanne,” amesema.

Amesema baada ya kufika polisi, wote waliwekwa ndani akiwamo yeye, lakini alitolewa baada ya siku mbili.

“Baada ya siku kadhaa naona wale vijana wametolewa, japo yule Mbaga sijamwona,” amesema.

Alipoulizwa hali aliyokuwa nayo Mbaga kabla ya kukamatwa, Mollel amesema, “hakuwa na jeraha lolote, wala alikuwa hajapigwa, alikuwa mzima kabisa.

“Ninachoshangaa mimi ni kwamba nimepeleka malalamiko Polisi, mpaka sasa sina mwizi, sina wa kwenda naye mahakamani, sina silaha. Sasa hii ni biashara gani…? Polisi hawajanitendea haki.

“Polisi hawajawahi kuniita, kuniambia tumekosa silaha au tumepata, hawaniambii kama bastola imepatikana au imekosekana, mimi taarifa ninayoisikia ni kwamba watu wameachiwa

“Hata kama ni wewe umekamata wahalifu, Polisi ni sehemu ya kuweka watu na kupeleka mahakamani. “Nimerudi polisi kuuliza, wamesema nenda kakae sisi ndio tunajua namna ya kuitafuta silaha,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu madai ya kuiweka rehani bastola hiyo na kwamba anawasingizia vijana hao, Mollel amejibu, “Hapana, mimi sina biashara hiyo. Sitaki kuchafuliwa jina langu kwa sababu kila mtu ananijua.”

Juhudi za kumtafuta Mbaga kueleza kilichompata, bado zinaendelea.

Katika hatua nyingine, Mwananchi limetonywa kuwa ofisa anayetuhumiwa kumpiga risasi Mbaga amehamishwa na kuwekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Minjingu Babati, mkoani Manyara kufuatia upelelezi unaoendelea.

Juhudi za kumtafuta Mbaga kueleza kilichompata, bado zinaendelea.

Katika hatua nyingine, Mwananchi limedokezwa kuwa ofisa anayetuhumiwa kumpiga risasi Mbaga amehamishwa na kuwekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Minjingu Babati, mkoani Manyara kufuatia upelelezi unaoendelea.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za ofisa anayetuhumiwa kumpiga risasi mtuhumiwa Mbaga kwamba amehamishiwa Minjingu, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Raphael Lulandala amesema, “hayo ya mkuu wa kituo cha polisi kuondolewa, ni process ambayo ni sehemu ya uchunguzi tu.”

Mwananchi lina taarifa kuwa Jeshi la Polisi limetuma maofisa kutoka Makao Makuu kufuatilia sakata hilo na maofisa hao wamewahoji askari waliokuwa zamu tangu Mbaga na wenzake walipokamatwa.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Polisi, Kamishna Ramadhani Kigai alipoulizwa jana kuhusu sakata hilo, alimtaka mwandishi kumtafuta RPC Katabazi.

Awali  Lulandala alipozungumza na Mwananchi wiki iliyopita, alikiri ofisi yake kufuatiulia suala hilo na leo amesema bado uchunguzi unaendelea.

“Kwa mimi kama ofisi yangu bado hilo jambo siwezi kulizungumzia kwa sababu nilishakwambia kwamba uchunguzi unaendelea wa vyombo, hivyo ni vizuri tukasubiri hatima ya uchunguzi.

Alipoulizwa ni chombo gani kinachofanya uchunguzi, amesema, “Siwezi kukwambia kwa sasa kwamba nani anafanya uchunguzi, lakini elewa tu kwamba Serikali inafahamu juu ya hayo malalamiko na hizo tuhuma na yule kijana anafahamu kwamba jambo hilo ofisi yangu ililipokea na imekuwa ikilifanyia kazi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inalifahamu jambo hilo na inalifanyia kazi,” amesema.

Tukio hilo linadaiwa kutokea siku moja baada ya Mbaga na wenzake watatu kukamatwa Machi 30, 2024 wakidaiwa kuiba bastola na vitu vingine, mali ya mfanyabiashara wa madini, Samson Mollel na baadaye waliachiwa Aprili 21, 2024, huku Mbaga akidaiwa kujeruhiwa kwa risasi.

Related Posts