Wakati Wakristo wakisherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo kama mwokozi wa dunia Desemba 25, maeneo mengine kumekuwa na matukio tofauti huku baadhi ya Wakristo wakisubiri Krismasi yao Januari 7, 2025.
Akihubiri katika ibada ya Krismas, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametumia baraka yake ya ‘urbi et orbi’ (kwa jiji na kwa dunia) ya mchana kuomba kusitishwa kwa mapigano, au angalau kuboreshwa kwa hali ya raia, katika mizozo ya Ukraine, Gaza, na Sudan.
“Tusikie kelele za silaha zisitike katika Ukraine iliyoharibiwa na vita,” alisema kutoka kwenye balcony ya Basilika ya Mtakatifu Petro.
Syria waadhimisha Krismasi ya kwanza baada ya Assad
Wakristo wa Syria wamehudhuria ibada za usiku wa Krismasi kwa mara ya kwanza tangu kung’olewa madarakani kwa Rais Bashar al-Assad mapema Desemba 2024.
Katika mji wa Sednaya nchini Syria, umati mkubwa ulijikusanya karibu na nyumba ya watawa ya kihistoria usiku wa Krismasi kushuhudia kuwashwa kwa mti mrefu wa Krismasi uliopambwa kwa taa za kijani zinazoangaza.
Sherehe hiyo ilitoa muda wa furaha katika mji uliojeruhiwa kwa zaidi ya muongo mmoja wa vita na gereza lake maarufu, ambako makumi ya maelfu walizuiliwa.
Familia na marafiki walisimama karibu na mti uliokuwa umeangazwa, wengine wakiwa wamevaa kofia za Santa, huku wengine wakiangalia kutoka paa za nyumba, ambapo bendi ilipiga muziki wa sherehe na fataki zikaangaza anga.
“Mwaka huu ni tofauti, kuna furaha, ushindi na kuzaliwa upya kwa Syria na Kristo,” anasema muumini aliyejitambulisha kwa jina la Houssam Saadeh.
Naye Joseph Khabbaz anaelezea matumaini ya umoja kati ya madhehebu na dini zote nchini Syria.
Viti vya Kanisa la Mama wa Damascus katika mji mkuu wa Syria vilijaa waumini wa rika tofauti, vijana na wazee, wakiwa wameshika mishumaa huku nyimbo za dini zikiujaza hewa na kupaa ndani ya kanisa.
Saa chache kabla ya ibada, mamia ya waandamanaji mjini Damascus walikusanyika kulaani tukio la mti wa Krismasi kuchomwa moto katika maeneo ya vijijini ya kaskazini mwa Mkoa wa Hama, magharibi ya kati mwa Syria.
Wakiwa wamebeba misalaba ya mbao, walipaza sauti wakisema, “Sisi ni askari wako, Yesu, kwa damu na roho zetu, tunajitoa kwa Yesu na watu wa Syria ni wamoja.”
Desemba 9, 2024 Rais Bashar Al- Assad alipinduliwa madarakani na kukimbilia nchini Russia, baada ya kundi la waasi liliongozwa na kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) kuzidisha mashambulizi yake katika mji mkuu wa Damascus.
HTS limetangazwa kama shirika la kigaidi na Umoja wa Mataifa, Marekani, Uturuki na nchi nyingine.
Kundi hilo lilihitimisha utawala wa miaka 24 ya Assad aliyerithi madaraka kutoka kwa baba yake Hafez al-Assad, aliyetawala nchi hiyo kuanzia mwaka 1971 hadi 2000.
Bethlehemu waadhimisha Krismasi ya huzuni
Ni mji aliozaliwa Yesu Kristo miaka 2000 iliyopita, lakini kwa sasa uko shakani kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Gaza.
Ni mwaka wa pili sasa mji huo wa ulioko Palestina katika Ukingo wa Magharibi unashindwa kuadhimisha siku hiyo.
Bethlehemu, mji ulioko Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel ambao Wakristo wanaamini kuwa ndio mahali pa kuzaliwa kwa Yesu Kristo, unaadhimisha Krismasi nyingine ya huzuni chini ya kivuli cha mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.
Usiku wa kuamkia Krismasi Jumanne, mji huo ulikosa furaha ya kawaida ya sikukuu, bila taa wala mti mkubwa wa Krismasi kupamba Uwanja wake wa Manger, bila umati wa watalii na bila bendi za vijana zinazotembea kwa gwaride ambazo kawaida hufanya tukio hilo kuwa la pekee.
Baadhi ya waadhimishaji wa Palestina walitembea kimyakimya mitaa, tofauti na bendi yao ya muziki wa shaba yenye kelele.
Baadhi walibeba bango lililosema, “Tunataka maisha, sio kifo.”
Vikosi vya usalama vya Palestina, kwa upande mwingine vilipanga vizuizi karibu na kanisa lililojengwa juu ya mahali ambapo inasadikiwa Yesu alizaliwa.
Mfalme Charles aenda kanisani kwa miguu
Mfalme Charles III na baadhi ya wanafamilia ya kifalme ya Uingereza wamehudhuria ibada ya Krismasi katika kanisa la Sandringham, baada ya mwaka ambao mwanawe na mrithi wa kifalme, Prince William, alielezea kuwa mwaka magonjwa kwa familia.
Charles na Malkia Camilla walitembea umbali mfupi kutoka nyumba ya Sandringham huko Norfolk, kusini mashariki mwa Uingereza, hadi Kanisa la St Mary Magdalene, wakipita na kuwasalimia watu waishio na matumaini.
Walijiunga na William, mkewe Kate na watoto wao George, Charlotte, na Louis karibu na kanisa.
Charles anaugua saratani na ingawa maelezo yote kuhusu hali yake yamefanywa kuwa siri, Ikulu ya Buckingham hivi karibuni ilisema matibabu yanaendelea vizuri na yataendelea mwaka 2025.
Katika hotuba yake iliyorushwa kutoka kanisa la hospitali ya zamani ya Middlesex katikati ya London, mfalme amepongeza majibu ya jamii kwa machafuko ya majira ya kiangazi ya Uingereza na kuwashukuru madaktari wanaowatibu saratani ambao wamemuhudumia yeye na Malkia wa Wales.
Ethiopia bado wanasubiri Krismasi
Wakati dunia ikiadhimisha Krismasi Desemba 25, Waethiopia wao wanasubiri Krismasi yao ifikapo Januari 7, 2025, kwa sababu wanaamini kuwa Yesu Kristo, kiongozi wa kiroho wa Wakristo, alizaliwa tarehe hiyo.
Imani hiyo inatokana na madhehebu ya Wakristo wa ‘Coptic’ (wakazi wa kiasili wa Kikristo nchini Misri na Mashariki ya Kati), ambao hutumia kalenda ya Julian ya Kanisa la Orthodox badala ya kalenda ya Gregory.
Ethiopia siyo nchi pekee inayotumia kalenda ya Julian kusherehekea Krismasi Januari 7, wapo pia Wakristo wa Misri na Eritrea, ambao ni wafuasi waaminifu wa mafundisho ya Kanisa la Orthodox la Coptic.
Wakati sherehe za Krismasi kwa kalenda ya Gregory huanza na ibada maalumu ya usiku wa Desemba 24 (usiku mkuu) kabla ya asubuhi ya Desemba 25, Wakristo wa Coptic huanzisha sherehe zao za Krismasi kwa kufunga kwa siku 43 au 44 (ikiwa ni mwaka wa kuruka) kabla ya sherehe za Krismasi.
Kufunga huko hujulikana kama Tsome Nebiyat na huongozwa na mitume.
Wakati wa kipindi cha kufunga, kinachojulikana kama Kufunga kwa Kuzaliwa kwa Kristo au Kufunga kwa Mitume, kila Mkristo wa Coptic hutakiwa kula mboga za majani pekee, wakiacha kunywa maziwa, nyama na samaki na hufungulia kwa mlo wa unaoitwa vegan.
Usiku wa Krismasi, wakiwa wamevaa mavazi meupe, waumini huenda kwenye kanisa lililo karibu kwa ajili ya ibada ya Krismasi ya usiku kucha.
Mapadre na waimbaji huimba usiku mzima wakati wengine wakishangilia na kuwasha mishumaa.
Siku inayofuata (Januari 7) ndio huwa Krismasi ikijulikana kwa jina la Guena husherehekewa kwa furaha kubwa kwa kula vyakula vya kitaifa kama sosi ya kuku (Doro Wat), nyama mbichi (Tere Siga) na Tubes.
Pia, sherehe hizo huhusisha mchezo wa zamani unaofanana na ule wa kwenye barafu (ice hockey) ukijulikana kama Ye Guena Chewata, ukihusisha mabwana na watumishi wao, lakini mabwana huwa hawakerwi pale wanapofungwa na watumishi wao.
Kulingana na simulizi zao, Waethiopia wanaamini kuwa, mmoja wa Mamajusi walioifuata nyota iliyoonyesha alipozaliwa Yesu, alikuwa Muethiopia.