Dar es Salaam. Ghasia zinazoendelea nchi jirani ya Msumbiji zimesambaa maeneo tofauti nchini humo wakati vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania vikiimarisha ulinzi katika mipaka ya kusini huku Serikali ikiwatoa hofu wananchi waishio Mtwara.
Tanzania na Msumbiji zimepakana, kwa maana ya Mkoa wa Mtwara, umepakana na Mkoa wa Cabo Delgado uliopo kaskazini mwa Msumbiji unaotajwa kuwa maficho ya magaidi nchini humo.
Tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 9, 2024, yaliompa ushindi mgombea wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo, wananchi wamekuwa wakiandama wakipinga ushindi huo.
Hali tete na usalama nchini humo imekuwa ikiongeza hofu kwa Watanzania waishio kusini, hata hivyo Serikali imewahakikishia usalama huki ikieleza vyombo vya ulinzi viko kazini kulinda amani.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema hadi sasa Mtwara ipo salama na wanavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo.
“Wananchi wa Mtwara wamesherehekea Sikukuu ya Krismasi kwa amani na utulivu; na usalama unaendelea kutamalaki katika mkoa wetu na wananchi wanaendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa kama kawaida,” amesema Kanali Sawala.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kutofumbia macho mtu yeyote atakayetaka kuhatarisha amani na utulivu, hivyo watoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika ili hatua stahiki zichukuliwe.
Pia, amewataka wananchi wa Mtwara kuendelea kutumia utaratibu uliopo wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika za vijiji na vitongoji kwa wageni watakaowapokea na kama kuna mtu hawamfahamu, pia wafanye hivyo ili wahusika waweze kufuatilia.
“Utaratibu tulionao kwa Taifa, mwenyeji anapopokea mgeni anatakiwa kutoa taarifa kwenye uongozi wa kitongoji na kijiji kwamba nyumbani kwangu nina mgeni na eneo alilotoka na muda atakaokaa, hivyo niwaombe wananchi kufuata utaratibu huo,” amesema Kanali Sawala.
Jumatatu iliyopita, Desemba 23, 2024, takriban watu 21 waliuawa katika machafuko baada ya Mahakama Kuu ya Msumbiji kuthibitisha ushindi wa uchaguzi huo.
Uamuzi wa Baraza la Katiba uliibua maandamano mapya ya nchi nzima ya makundi ya upinzani na wafuasi wao wanaosema uchaguzi huo uliibiwa, tuhuma zilizokanushwa vikali na Frelimo.
Msumbiji, nchi iliyoko Kusini mwa Afrika, yenye takriban watu milioni 35, imetawaliwa na Frelimo tangu 1975.
Waangalizi wa nchi za Magharibi, pia, wamesema uchaguzi haukuwa huru na wa haki.
Takribani watu 130 wameuawa katika makabiliano na polisi, kwa mujibu wa shirika la ufuatiliaji wa mashirika ya kiraia la Plataforma Decide.
Matokeo ya awali kutoka kwa Tume ya Uchaguzi yalimpa nafasi ya urais Daniel Chapo wa Frelimo kwa kishindo huku chama hicho kikibaki na wingi wa viti bungeni.
Kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, aliyeshika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais, alikuwa ameonya kabla ya tangazo la Jumatatu kwamba Msumbiji ingeingia kwenye machafuko ikiwa Mahakama itathibitisha ushindi wa Frelimo.
Jana, Desemba 25, 2024, ghasia za magereza katika mji mkuu wa Maputo zilisababisha vifo vya watu 33 na wengine 15 kujeruhiwa.
Kamanda Mkuu wa Polisi, Bernardino Rafael amesema Jumatano iliyopita Takriban watu 1,534 walitoroka jela katika tukio hilo lakini 150 kati yao sasa wamekamatwa tena, Rafael alisema.
Msumbiji inakabiliwa na machafuko yanayoongezeka yanayohusishwa na uchaguzi wa Oktoba wenye utata, ulioongeza muda wa Frelimo kuendelea kubaki madarakani. Upinzani na wafuasi wao wanadai kura katika uchaguzi huo ziliibwa.
Wakati Rafael akilaumu maandamano nje ya gereza hilo kwa kuchochea ghasia hizo, Waziri wa Sheria, Helena Kida alikiambia kituo binafsi cha televisheni cha Miramar TV kwamba machafuko hayo yaliyoanzishwa ndani ya gereza hilo, hayana uhusiano wowote na maandamano nje.
“Makabiliano baada ya hapo yalisababisha vifo vya watu 33 na kujeruhiwa 15 karibu na gereza.” Rafael aliuambia mkutano na wanahabari. Utambulisho wa waliouawa na kujeruhiwa haukufahamika.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji alisema siku ya Jumanne kwamba watu wasiopungua 21 waliuawa katika machafuko baada ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kuthibitisha ushindi wa Frelimo, Jumatatu iliyopita.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Denis Konga amesema unapoangaliwa usalama usitazamwe kwa Msumbiji pekee, kwa kuwa nchi hizi ni marafiki na wapo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc).
Amesema Tanzania inaathirika japokuwa si moja kwa moja, lakini itapata athari kwa sababu ya wananchi wa Msumbiji kutaka kukimbilia nchi iliyopo karibu nao, hivyo ni rahisi kwa wao kuingia kama wakimbizi.
“Jimbo la Cabo Delgado lipo karibu na mikoa ya Tanzania kwa kuangalia hao watu kinachowapa nguvu, kwao pakiharibika wanajua pa kukimbilia ni nchi iliyopo jirani na kwao ambayo ni Tanzania na hapo kuna hali ya kupokea wakimbizi wengi, hivyo sio jambo la kufurahi na inatakiwa kuangaliwa kwa hali ya tofauti,” amesema Konga.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan yupo kwenye utatu wa uongozi wa Sadc katika kamati ya ulinzi na usalama, akimsaidia mwenyekiti ambaye ni Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, hivyo wana nafasi kufanya kitu ili hali iwe shwari kutokana na ukaribu uliopo baina ya Msumbiji na mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Mbali na hilo, Konga amesema kumekuwa na maswali mengi kwa nchi za Afrika kwenye Tume za Uchaguzi na Mahakama ambazo zimekuwa zikiongozwa na usiri katika kutoa uamuzi ambayo wananchi wanakuwa hawakubaliani nayo.
“Ukiangalia kwa yaliyotokea ni uamuzi uliochagizwa na Mahakama na ukifuatilia majaji wanateuliwa na watu waliopo kwenye uongozi, hivyo huu utamaduni ungebadilika, wasiwe wanateuliwa, bali waombe kazi,” amesema Konga.
Utaratibu huo, amesema utajenga hali ya haki na usawa kwani kwa sasa nchi nyingi majaji wakiteuliwa wanaendelea kulipwa hadi pale kifo kitakapomtenganisha na uso wa dunia hivyo anaweza kutoa maamuzi yenye utata.
Amesema wananchi walikuwa wanaweza kukubaliana na Mahakama na kurudi nyumbani kwao lakini wameona hakuna haki na kuamua kuingia barabarani, hivyo inapaswa kuangalia tume za uchaguzi na namna, zinavyotoa haki na kuaminika na jamii na mambo mengi yatabadilika.