Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kongowe Kibaha mkoani Pwani wakiwajulia hali watoto mapacha ambao mama yao amepata maradhi ya moyo baada ya kujifungua.
………………………………..
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
WATOTO Mapacha ambao mama yao amepata changamoto ya maradhi ya moyo muda mfupi tangu alipojifungua wakazi wa Kongowe Kibaha mkoani Pwani wanahitaji msaada wa hali na mali wa matunzo.
Mama ya watoto hao Amina Mohamed Simba (28) ambaye baada ya kupata changamoto hiyo alipelekwa Hosptali ya Tumbi Kibaha lakini kufuatia hali yake kuwa mbaya amehamishiwa Hospitali ya Mlongazila jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi ambapo inaelezwa kuwa bado hali yake sio nzuri.
Watoto hao hivi sasa wanalelewa na bibi yao ambaye hana uwezo ambapo wanaiomba jamii kujitokeza kusaidia malezi ya watoto hao kutokana na kutegemea maziwa ya kopo tu.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kongowe Kibaha, Saidi Kibaya akizungumza na mwandishi wa habari hii alisema watoto hao wa miezi miwili wanalelelewa na bibi yao mzaa mama yao ambaye hana uwezo na kuwa wanaomba msaada huo kutokana na mahitaji yao hasa kwa upande wa chakula kuwa makubwa ndio maana wameona jambo hilo kulieleza kwa jamii kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kuwasaidia watoto hao malaika wa Mungu.
“Mama ya watoto hawa ni mkazi wa hapa Kongowe Kibaha alipojifungua tu alipatwa na changamoto ya maradhi ya moyo na kupoteza fahamu tangu hapo hali yake sio nzuri alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) Hospitali ya Tumbi lakini hivi sasa amehamishiwa Hospitali ya Mlongazila kwa ajili ya matibabu zaidi,” alisema Kibaya.
“Leo mimi na viongozi wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi Tawi la Kongowe akiwepo Mwenyekiti wa chama hicho tulikwenda kuwaona watoto hao ambapo tuliambiwa kuna mdau mmoja waliye mtaja kwa jina moja la Mwamwaja ambaye aliguswa na changamoto ya watoto hao alitoa Sh.150,000 ili zitumike kuwanunulia maziwa,” alisema Kibaya.
Kibaya aliiomba jamii na Serikali kuwasaidia watoto hao ili waweze kupata chakula pamoja na bibi yao huyo ambaye hana uwezo wowote.
Ndugu Mtanzania watoto hawa kulwa na Dotto ni watoto wetu wanahitaji msaada wako wa mali na hali kwani kutoa ni moyo na wala sio utajiri.
Aliyeguswa kuwasaidia watoto hao kwa kiasi chochote cha fedha anaweza kuwasiliana na mwandishi wa taarifa hii kwa namba 0754-362990 au kwa Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Tawi la Kongowe, Saidi Kibaya kwa namba ya simu 0655-075310. Kazi iendelee.