Utata mauaji ya mtoto wa mfanyabiashara maarufu Dom, azikwa

Dodoma. Utata umegubika tukio la mauaji ya Graison Kenyenye (6), mtoto wa mfanyabiashara maarufu wa jijini Dodoma, Zainab Shaban maarufu  Jojo.

Graison aliuawa usiku wa kuamkia juzi, wakati mama yake alipokwenda matembezini na rafiki yake wa kiume.

Tukio hilo lilitokea Ilazo Extension jijini Dodoma, usiku wa kuamkia Desemba 25, 2024, wakati Jojo alipomuacha mtoto huyo nyumbani kwa rafiki yake huyo,  Hamis Mpeta, ambaye ni Ofisa uvuvi Mtera.

Wakati Jeshi la Polisi likieleza kwamba mtoto huyo aliachwa kwa  bodaboda, mjomba wa mtoto,  Dk Frank Makaranga, amesema Graison aliachwa kwa rafiki wa mama yake, ambaye hata hivyo hakufafanua ni yupi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema jana kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 25, 2024, saa 1:00 asubuhi ambapo Mpeta akiwa na mama wa mtoto, Zainab, walibaini  kuuawa kwa mtoto huyo.

“Walimkuta mtoto huyo akiwa ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na shingoni, amekatwa na kitu chenye ncha kali. Katika tukio hilo, mama wa mtoto alimwacha mtoto huyo kwa dereva bodaboda anayejulikana kwa jina la Kelvin Gilbert,” amesema.

Amesema walimuacha mtoto huyo kwa dereva bodaboda saa 6:00 usiku, nyumbani kwa Mpeta (rafiki wa Zainab) na kwenda matembezini.

Hata hivyo, Kamanda Katabazi amesema waliporudi saa 1:00 asubuhi, juzi Desemba 25, 2024, walikuta mtoto ameuawa na Kelvin hakuwepo nyumbani.

Kamanda Katabazi alisema Kelvin alikuja kujitokeza baadaye na kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia kwa mahojiano zaidi kuhusu tukio hilo, kwa sababu aliachiwa mtoto huyo amwangalie ili asiweze kudhurika.

Alipoulizwa ni nani alitoa taarifa ya kuuawa kwa mtoto huyo, Kamanda Katabazi amesema mara baada ya kukuta mtoto ameuawa, Mpeta na Zainab waliwasiliana na polisi ambao walifika katika eneo hilo.

“Lakini kipindi hicho, huyu Kelvin hakuwepo lakini alikuja kujitokeza baadaye na ndipo tulipomshikilia kwa ajili ya mahojiano zaidi. Kwa hiyo, tunao watuhumiwa wawili tunaowashikilia akiwemo mtuhumiwa mwingine,” amesema.

Akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, jana,  Dk Makaranga amesema taarifa za tukio hilo ziko chini ya Jeshi la Polisi na familia wamelipokea tukio hilo kama lilivyo kama jamii nyingine inavyosikia.

“Ni kweli ameuawa kwa kushambuliwa lakini majibu mengi ambayo sisi hatuna yako kwa Jeshi la Polisi. Kwa taarifa za awali nilizozipokea kutoka kwa dada yangu (Zainab) kuwa mtoto wake ama mjomba wangu, amefariki baada ya dada yangu kuamka asubuhi na kupewa taarifa hizo,” amesema Dk Makaranga.

Amesema alipata taarifa kuwa mtoto huyo alishambuliwa katika nyumba ya rafiki yake Zainab,  alikomwacha na yeye kwenda katika matembezi ya Sikukuu ya Krismasi.

“Sisi kama ndugu, kwa kweli ni masikitiko makubwa kwa sababu ni kitendo cha kinyama na kikatili ambacho amefanyiwa mjomba wetu na taratibu za nchi yetu zipo na zinaeleweka. Tunaliomba Jeshi la Polisi liendelee kufuatilia kwa haraka tupate angalau kujua nini kilimtokea (Graison),” amesema.

Dk Makaranga ameliomba Jeshi la Polisi lihakikishe  haki ya mjomba wake aliyeuawa kikatili.

Dk Makaranga amesema mtoto huyo amezikwa leo katika makaburi ya Kilimo Kwanza jijini Dodoma.

Katika ibada iliyofanyika nyumbani,  amesema mtoto huyo atakumbukwa kwa kipaji chake cha kuimba kwaya na tabia ya ucha Mungu.

Amesema merehemu alikuwa akisali katika katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Area D jijini Dodoma.

“Graison atakumbukwa kwa upendo na ucheshi aliokuwa nao kwa watoto wenzake. Graison alifariki dunia Desemba 25, 2024 kwa kuchinjwa na kupigwa na kitu kizito kichwani mpaka kuuliwa,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimwa Kusini, Samuel Erasto ametoa wito kwa wazazi kuendelea kuwa walinzi na kuwa karibu na watoto wakati huu wa kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

“Tunatumai kuwa mwisho wa mwaka familia zote huwa zinajumuika kwa pamoja; tujitahidi kuwa waangalifu, kuwadhibiti watoto wetu pamoja na watu wenye mahitaji maalumu,” amesema.

Mchungaji wa Kanisa TAG la Area D, Rehema Pangasi,  amesema mtoto huyo alikuwa ni mshirika wa kanisa hilo na alikuwa mwimbaji wa kwaya ya Shekina na kwamba alikuwa akifika kila Jumamosi kanisani kwa ajili ya mazoezi.

“Hata Jumamosi hii (Desemba 20, 2024) alikuwa kanisani kwa ajili ya mazoezi ya kwaya. Jumapili alikuwa kanisani anaimba, nilimchukua video kidogo wakati anaimba, hata sikujua kwanini niliichukua, Mungu anajua yote,” amesema Rehema.

Amesema Jumamosi iliyopita, alivyokwenda katika mazoezi ya kwaya, alimuuliza  iwapo amrudishe nyumbani kwao,  lakini alikataa kwa kuwa mama yake alimweleza kuwa atamtumia bodaboda imfuate.

Amewataka watu kumgeukia Mungu kwa kuwa wakiwa na hofu yake,  hawatafanya vitendo vya ukatili kama walivyofanya kwa mtoto huyo.

Amesema wakati wanasherekea sikukuu ya Krismasi kanisani, walimtafuta mtoto lakini hakuwepo na walikuja kupata taarifa baadaye kuwa ameuawa.

Mtoto Grayson Kanyenye (6) akiwa na mama yake enzi za uhai wake.

‘Baba’ wa Graison ajitokeza

Licha ya kwamba hadi sasa haijawekwa wazi baba mzazi wa mtoto huyo ni nani,  mwanamitandao,  Godlove Mwakibete kupitia ukurasa wake wa Instagram amejitokeza na kueleza yeye ndiye baba wa hiari wa  Graison.

Kupitia ujumbe wake aliombatanisha na picha akiwa na mtoto huyo,  Godlove ameonesha kusikitishwa na kitendo kilichotokea kwa mtoto huyo na kueleza anaacha sheria ichukue mkondo wake.

“Nilikuwa bado siamini kama binadamu wamegeuka wanyama kiasi cha kupoteza uhai wa mtoto asiye na hatia wala ugomvi  na mtu yeyote.

“Limeniumiza na sitoweza kulibeba kwa yeyote aliyehusika hatokuja kuishi kwa amani kwenye hii dunia na ahera. Najua wewe ni malaika huna hata chembe ya ugomvi wala hasira. Tunaicha sheria ichukue mkondo wake wote waliohusika wakamatwe,”ameandika.

Hata hivyo, rafiki wa karibu wa mama yake Graison, amesema marehemu alizoeana na Mwakibete na kumuomba kuwa baba yake wa hiari.

Tukio hilo limetokea wakati wakazi wa Dodoma wakiwa na kumbukumbu ya matukio mengine ya mauaji ya kikatili yaliyojitokeza katika siku tofauti kati ya Septemba na Oktoba, mwaka huu.

Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na lile lililotokea usiku wa kuamkia Agosti 28, 2024 ambapo katika Mtaa wa Mbuyuni Kata ya Kizota wilayani Dodoma, Michael Richard (36) aliuawa huku mkewe, Agnes Eliah na wanawe Ezra, Witness na Ephrahim Michael wakijeruhiwa.

Pia, usiku wa kuamkia Septemba 6, 2024, yalitokea mauaji katika Mtaa wa Muungano A, kata ya Mkonze ambapo Mwamvita Mwakibasi (33) na mtoto wake, Salma Ramadhan (13), waliuawa na watu wasiojulikana na kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Lakini Septemba 16, 2024 katika Mtaa wa Segu Bwawani, Kata ya Nala, Milcah Robert (12) na Mkazi wa Mailimbili jijini Dodoma, Fatuma Mohamed (20) waligundulika kuuawa ndani ya nyumba.

Katika tukio hilo, pia, binti aliyekuwa akifanya kazi katika nyumba hiyo, aliyetambuliwa kwa jina moja la Micky aliuawa  huku mama wa familia hiyo, Lusajo Mwasonge (40) akijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Related Posts