Malinyi. Wanakijiji wa Ngombo, wilayani Malinyi mkoani Morogoro wameilalamikia Serikali kwa kuanzisha oparesheni ya kuwaondoa katika kijiji hicho kupisha Pori la Akiba la Kilombero, bila kuwapatia eneo mbadala la kuhamia.
Wanakijiji hao, walioko katikati ya Bonde la Kilombero, wamekubali kuondoka lakini wanahoji; wataenda wapi?
Mkazi wa kijiji hicho, David Mkumba amesema alizaliwa Ngombo, na wazazi wake walikuwepo hapo tangu mwaka 1912 hivyo anashangazwa na madai kuwa wao ni wavamizi wa hifadhi hiyo, huku wakitakiwa kuondoka kwa fidia ndogo bila kupewa maeneo ya kuhamia.
“Makaburi ya wazazi wangu yako hapa, hatukatai kuondoka, lakini tunaondoka tunaenda wapi? Tunaondolewa bila kupewa utaratibu hata kuku anajengewa tundu,” amesema Mkumba.
Mkumba amekiri kuwa wanapewa fidia ya fedha kidogo, lakini hawapewi muda wa kutosha kuhamisha mali zao, ikiwemo makaburi ya ndugu zao.
Mkazi mwingine wa Ngombo, Tausi Crispin amesema wanapewa fidia ya Sh1 milioni kwa kila kaya ambayo haitoshi kwa mahitaji ya kuanzisha makazi mapya.
“Tuna watoto na wanafunzi hatuna uhakika kama huko tutakapokwenda tutapata huduma za elimu na afya,” amesema Crispin.
Ameongeza; “Unaingiziwa hiyo milioni moja leo, kesho wanataka uondoke, ukijaribu kuandaa vitu vyako, wanakuja kukupiga fimbo. Tunaomba Serikali kuu iingilie suala hili.”
Kwa upande mwingine, wanakijiji hao wamesema nyumba zao zimekuwa zikibomolewa bila kujali kama wamepata sehemu ya kuhamia au la, hali inayosababisha kina mama na watoto kulala nje wakati wa mvua.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba amethibitisha kuwepo kwa oparesheni hiyo na kusema kuwa imeanzishwa kwa lengo la kupisha uhifadhi na kuongeza kuwa Serikali imetenga zaidi ya Sh6 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia kaya zipatazo 1,156 na tayari wengi wameshalipwa.
“Zimebaki kaya 64 tu ambazo bado hazijalipwa, tunatoa maelekezo kuwa atakayelipwa lazima aondoke mara moja, kwani mvua zikiendelea kunyesha watashindwa kuondoka,” amesema Waryuba.
Akizungumzia suala la maeneo ya kuhamia, Waryuba amesema Serikali imewapa wananchi uhuru wa kutafuta maeneo yao ya kuishi, kwani hakuna sehemu maalumu iliyotengwa kwa ajili yao.