Takwimu zikionyesha kuwa China ndiyo mbia namba moja wa biashara na uwekezaji nchini, kumekuwa na mchanganyiko wa mawazo juu ya wingi wa raia Taifa hilo namba mbili kwa uchumi duniani.
Wapo wanaoona wingi wa Wachina nchini ni fursa ya maendeleo kwa kuongeza shughuli za kiuchumi na wengine wakihofu kuibuka kwa unyonyaji mpya wa uchumi na nguvu kazi.
Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), hadi Februari 2024, China imeshasajili miradi 1,274 yenye thamani ya Dola 11.4 bilioni, ikilenga kuzalisha ajira 149,759, ikiwa ni matunda ya ushirikiano wake na Tanzania.
Akizungumzia kuibuka kwa China kama kinara cha uwekezaji nchini, Profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Aurelia Kamuzora anasema kuna faida na hasara zake.
“Ukiangalia bidhaa wanazoleta kwetu, sisi hatuna uwezo wa kuzitengeneza, kwa mfano pikipiki wanazozileta zinatumika huku kama chanzo kwa ajira kwa vijana na inarahisisha usafiri na hivyo kuleta michango wa kiuchumi kwa wananchi. Hiyo ni chanya.
“Lakini kwa mtazamo hasi, nchi zetu sisi hazina teknolojia, hivyo tunategemea kuingiza bidhaa kutoka nje, hivyo tunazalisha ajira kwao kwa kuendelea kununua bidhaa zao.
Anasema kama nchi itaruhusu uingizwaji wa bidhaa kutoka China kupitia uwekezaji, maana yake ni kuua viwanda vya ndani na tunaongeza ajira kwao.
Ukiachilia mbali eneo la biashara, kuna dhana pia kuwa Wachina wametawala kila kona katika kandarasi za miradi mbalimbali.
Akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2024/25 Mei 2024 bungeni Dodoma, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi (sasa Waziri wa Mambo ya Ndani), Innocent Bashungwa alirejea takwimu za Bodi ya Usajili wa Makandarasi akisema katika jumla ya miradi 36,839, wazawa walitekeleza miradi 35,351 sawa na asilimia 95.9 ya miradi hiyo.
Hata hivyo, alisema miradi iliyotekelezwa na wazawa ni midogomidogo yenye thamani ya Sh23.74 trilioni, sawa na asilimia 38.5 ya miradi yote iliyosajiliwa na kutekelezwa katika kipindi hicho, ambayo ni Sh61.638 trilioni.
“Hivyo, makandarasi wa nje ambao ni takriban asilimia 4.1 walitekeleza miradi michache yenye thamani kubwa (asilimia 61.5 ya thamani ya miradi yote).
“Sababu kubwa inayochangia hali hii ni uwezo mdogo wa kifedha wa makandarasi wa ndani, mitambo na wataalamu, hivyo inakuwa vigumu kwao kushindana kwenye zabuni za kazi na makandarasi kutoka nje, hasa kampuni za Kichina,” alisema.
Miongoni mwa kampuni zinazotajwa kutawala kandarasi za ujenzi wa barabara na majengo nchini ni pamoja na China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), Sinohydro Construction Corporation, China Railways 15 Bureau Group Corporation (CR15BGC).
Nyingine ni China Wu Yi Co. Ltd, STECOL Corporation, JIANGXI, China Railway Seventh Group, China Henan International Cooperation (CHICO), China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Geo- Engineering Corporation.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam wanalalamikia baadhi ya wafanyabiashara wa China, wakisema wanaua biashara katika eneo la Kariakoo.
“Kwa mfano ukiagiza kontena moja ya miavuli, Mchina yeye anafungasha kontena 10 za miavuli zinakufuata nyuma,” anasema Frank Nduta, anayefanya biashara katika eneo la Kariakoo.
Anasema baadhi ya wafanyabiashara wa China wamefungua maghala na wanashindana na wazawa kuuza bidhaa za rejareja.
“Ukienda China kufungasha vipuri vya baiskeli, Mchina naye anakuja nyuma yako na kontena 10 za vipuri kama hivyo, unaposhusha na yeye anashusha, tena unaweza kukuta yeye akatangulia kushusha, kwa sababu wewe si utakuwa unatafuta fedha za kulipia kontena lako,” anasema.
Anasema wafanyabiashara hao hawaishii Dar es Salaam, bali wameshaanza kutafuta masoko mikoani, wakitumia pia wamachinga ambao hawalipi kodi.
Wanawapa wamachinga, kwa mfano ukifika Mtaa wa Narung’ombe, kuna wamachinga wengi, hivi unafikiri mtu mwenye duka anayelipa kodi anaweza kushindana nao?
“Kwa hiyo wakati wewe unapambana kulipa kodi mwenzako halipi, hivyo anauza bidhaa bei ya chini,” anasema na kuongeza:
“Pili wanachukua ajira za wazawa na wanalifanya soko liwe gumu, kwa sababu wewe unafungasha kulingana na mahitaji ya soko, mwenzako analeta kontena 10, maana yake soko linafurika bidhaa na likifurika, yeye anauza hata bei ya chini ili amalize.”
Malalamiko hayo pia yameungwa mkono na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martin Mbwana akisema walishapeleka malalamiko hayo kwa viongozi wa Serikali, lakini hayajafanyiwa kazi.
“Kuna vitu ambavyo mgeni hastahili kufanya ambavyo havihitaji teknolojia na tunaweza kufanya wenyewe, mathalani, mgeni kujiajiri kwenye bodaboda au teksi, ambayo sisi tunaweza kufanya,” anasema.
Anaongeza: “Sisi tunanunua mzigo kwao na wao wanakuja kwetu, halafu tunakwenda kuwauzia ndugu zetu na wao wanakwenda hukohuko kuwauzia ndugu zetu, hiyo haiwezekani.”
Mbwana anasema kuwabana wafanyabiashara hao inakuwa vigumu kwa kuwa wanashirikiana na wazawa.
“Wachina wanawatumia Watanzania kwenye biashara, hivyo hata ukimkamata, utakuta mwenye leseni na namba ya TIN ni Mtanzania, ila utagundua Mchina yuko nyuma na ndiye mwenye akaunti za benki,” anasema.
Mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo, Severine Mushi anakiri kuwepo malalamiko hayo, akisema ni miongoni mwa mambo aliyopanga kuyashughulikia.
“Malalamiko yaliyopo ni kwamba Wachina wakishaingiza mzigo wanafungua maduka ya rejareja kama sisi wazawa wakati hawaruhusiwi.
“Kwa kuwa sasa nimekuwa ni kiongozi, nitayashughulikia haya kwa kuzungumza na mamlaka zinazohusika ili kuhakikisha tunaangalia sheria zilizopo na jinsi ya kuondokana na kero hii,” anasema.
Kituo maalumu nacho tishio
Baadhi ya wafanyabiashara pia wameonyesha hofu ya ujio wa kituo cha biashara cha The East Africa Commercial and Logistics kinachoendelea kujengwa Ubungo Dar es Salaam, wakisema kinaweza kufifisha biashara eneo la Kariakoo.
Kituo hicho, ambacho ni uwekezaji wa Raia wa China, kitakuwa na jengo lenye ghorofa nne, kina maduka zaidi ya 2,000 na uwanja wa kuegesha magari zaidi ya 1,000.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa kituo hicho, Cathy Wang anawatoa hofu wafanyabiashara na wadau wenye hofu akisema, kituo hicho mbali na kuwa na maduka, kitawaunganisha wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa nchini China na kuepusha usumbufu kiuchukuzi.
“Mradi huu utakuwa ndio lango kuu la bidhaa zinazotoka China kuingia nchini na kusafirisha bidhaa kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki. Wafanyabiashara hawatalazimika kuagiza bidhaa nje ya nchi na kusubiri miezi mitatu minne, badala yake watachukua hapa Tanzania,” anasema Wang, alipozungumza na Mwananchi hivi karibuni.
Akizungumzia hofu ya kuzorota kwa biashara katika eneo la Kariakoo, Wang anasema: “Sidhani kwamba mradi huu utazorotesha biashara katika eneo la Kariakoo, kwa sababu hilo ni eneo kubwa lililoanzishwa tangu miaka ya 1940, hivyo watu hawataacha kwenda.
“Halafu kama tunataka nchi iendelee, hatuwezi kulazimisha kila mtu aende Kariakoo na ujifungie hapo ukisema tusipanue biashara kama tulivyojenga hapo Ubungo,” anasema.
Anasema katika kukuza biashara, wanakusudia kuongeza vituo katika maeneo mengine kama stendi ya Magufuli na soko kubwa wilayani Temeke.
Wang anasema eneo hilo litakuwa kituo cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na nchi za Jumuiya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).
“Hebu fikiria miaka ijayo, nchi za Afrika Mashariki hazitalazimika kwenda China kufungasha mizigo, watakuja hapa Dar es Salaam, kwa hiyo wafanyabiashara wa ndani waje hapa kuchukua bidhaa na tutawaunganisha na wazalishaji wa bidhaa,” anasema.
Akieleza manufaa ya mradi huo kwa uchumi wa Tanzania, Wang anasema ni pamoja na kuzalisha ajira.
“Mpaka sasa mradi bado haujakamilika lakini kuna ajira 5,000 zimezalishwa katika ujenzi na tutakapoanza mradi, walau ajira rasmi 15,000 zitazalishwa na zisizo rasmi zinatarajiwa kuwa 50,000.
“Pia mradi utawezesha kukua kwa biashara ya mtandaoni na itakapoanza itazalisha ajira nyingi, hasa kwa vijana,” anasema.
Akizungumzia malalamiko ya wafanyabiashara jana, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe anasema hajayapata rasmi, licha ya kukutana nao katika vikao.
“Juzi nilikuwa nao pale Ubungo, sijaona wakitoa hoja hiyo ya tishio la Wachina,” anasema.
Hata hivyo, anasema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kufungua milango kwa wawekezaji na kutoa fursa kwa Watanzania kushirikiana nao.
“Wewe huna mtaji wa fedha lakini unaweza kushirikiana na mwekezaji kwa kumkodisha ardhi Mchina akatumia eneo lako.
“Kuna wawekezaji wengi wanakuja kwetu na sisi tunaenda TIC ambao nao wanatafuta watu wenye ardhi ambao watawakodisha watu wenye viwanda, hizo ndizo fursa tunazotakiwa tuone, ushirikiano.”
Hata hivyo, anasema wajibu wao ni kuhakikisha wawekezaji wanafuata sheria.
“Kwamba anaingia hapa anajulikana anafanya nini na shughuli zake ni halali, analipa kodi na anatoa ajira kwa Watanzania,” anasema.
Anasema lengo la Serikali ni kualika wawekezaji wa viwanda wazalishie bidhaa zao nchini badala ya kuagiza bidhaa na kuuza nchini.