Bulaya alipua bomu wadaiwa sugu wa maji, vinara hadharani

Dodoma. Wakati Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akisema suala la ufinyu wa bajeti ya Wizara ya Maji litajadiliwa kati ya Kamati ya Bajeti na Serikali, mbunge wa viti maalumu, Ester Bulaya amesema taasisi za umma zinadaiwa ankara za maji za Sh26 bilioni.

Katika mchango wake bungeni, Bulaya alieleza taasisi za majeshi ndizo zinazodaiwa madeni makubwa.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso jana aliwasilisha bungeni taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/25, huku wizara ikiomba Bunge kuidhinisha Sh627.7 bilioni ambazo zimeidhinishwa.

Wakati Serikali ikieleza imetoa Sh68 bilioni kulipa madeni ya makandarasi wa ndani kwenye miradi ya maji, hoja ya Bulaya imejibiwa ikielezwa mita za malipo kabla ya matumizi itakuwa suluhisho.

Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew amesema ufungaji wa mita za malipo kabla ya matumizi utaondoa tatizo la malimbikizo ya madeni ya ankara za maji kwa taasisi hizo.

Wakati wa kupitisha vifungu vya bajeti, Bulaya alitoa hoja ya kushika shilingi kwenye mshahara wa waziri hadi aelezwe namna fedha hizo Sh26 bilioni zitakavyolipwa.

Licha ya hoja yake ya kushika shilingi kuungwa mkono na wabunge, Spika amesema ni ngumu kwa Bulaya kufanya hivyo kwa sababu Waziri Aweso hawezi kutoa ahadi kwa kuwa taasisi zake ndiyo zinadai, labda ahadi itolewe na Waziri wa Fedha au mawaziri wengine ambao taasisi zao ndizo zinadaiwa.

Awali, Bulaya akichangia mjadala wa Wizara ya Maji leo Ijumaa Mei 10, 2024 amesema:

“Mwaka jana nilizungumza hapa kuhusu taasisi za Serikali kutumia maji hawalipi, akasimama Waziri wa Fedha akasema ametoa maelekezo watalipa, leo taasisi za Serikali zinadaiwa bilioni 26 (Sh26 bilioni), wananchi wa kawaida kule wakitumia maji wanakatiwa, kwa nini msiwakatie.

“JWTZ (Jeshi la Wananchi wa Tanzania) wanadaiwa Sh12 bilioni, Magereza Sh6 bilioni, Polisi Sh5.7 bilioni, Serikali za mitaa Sh1.5 bilioni, hospitali za mikoa Sh635 milioni, Ikulu ndogo Sh102 milioni, mifugo Sh44 milioni,” amesema Bulaya, akihoji wizara itawezaje kuongeza miradi mipya wakati fedha hazilipwi.

Pia, amezungumzia upotevu wa maji, ikiwamo maji kutumika bila kulipwa na kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilionyesha kuna mamlaka 12 zina upotevu wa maji wa Sh9.9 bilioni ambao ni mita za ujazo milioni 8.7.

“Lazima tuweke mikakati ya kutatua tatizo la upotevu wa maji. Mfano, Mamlaka ya Maji Rombo (Kilimanjaro) hasara ya upotevu wa maji ni Sh5 bilioni, Handeni (Tanga) Sh2.1 bilioni, Bunda (Mara) Sh788 bilioni, Maswa (Shinyanga) Sh666 milioni na Turiani (Morogoro) Sh648 milioni,” amesema.

Mbunge huyo alisema, “tunapunguza bajeti ya maji zaidi ya Sh100 bilioni halafu tunataka tatizo la maji liishe.”

Wakati wabunge wakieleza kilio cha ufinyu wa bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Maji ambayo ni pungufu kwa Sh137 bilioni, Serikali imesikia kilio kingine cha wabunge cha malipo ya makandarasi wa ndani, ikisema imetoa Sh68 bilioni.

Malipo hayo licha ya kuwa ni kutokana na kilio cha wabunge, pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira iliita,ka Serikali ihakikishe inalipa malimbikizo ya madeni yote ya makandarasi kabla ya Juni 30, 2024 ili miradi ya maji ikamilike na kuwanufaisha wananchi.

Kamati pia ilitoa hoja ya ufinyu wa bajeti na kwamba upungufu huo unaonyesha wizara hiyo siyo miongoni mwa vipaumbele vya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.

Kabla ya Bunge kukaa kama kamati kupitisha vifungu vya bajeti ya wizara hiyo, mbunge wa viti maalumu, Halima Mdee alisimama akitumia kanuni ya 79 inayompa haki mbunge kutoa hoja ya kusimamisha mjadala bungeni.

Mdee ametumia kanuni hiyo akiliomba Bunge lisimamishe mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji ili kutoa nafasi kwa Kamati ya Bajeti kwenda kukaa na Serikali na kutoa majibu bungeni Jumatatu kueleza nyongeza ya Sh137 bilioni ambazo ni pungufu kwenye bajeti ya wizara hiyo.

Hata hivyo, Spika Tulia kwa kutumia kanuni ya Bunge ya 124 na kanuni ya 125 alisema hata kama Bunge litapitisha bajeti hiyo, bado kuna nafasi ya siku sita kwa Kamati ya Bunge na wenyeviti wote wa kamati za Bunge kukaa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza maelekezo ya wabunge.

Akijibu hoja ya wabunge kuhusu madai ya makandarasi, Waziri Aweso alisema Serikali imetoa Sh68 bilioni kwa ajili ya kuwalipa makandarasi nchini.

“Kuhusu maelezo ya wabunge ya madai ya makandarasi wa ndani, tumekaa na Waziri wa Fedha (Dk Mwigulu Nchemba) ametupa ‘commitment’ na hivi ninavyozungumza Katibu Mkuu wangu Wizara ya Maji amenieleza tumepatiwa Sh68 bilioni, twende tukawalipe makandarasi wetu.

“Niwaombe sana makandarasi, mmewasikia namna wabunge walivyowapigania, mmesikia kilio cha wabunge namna wanavyowatetea, niwaombe sana fedha hizi tumezipata na nimwelekeze Katibu Mkuu wa Wizara yetu ya Maji baada ya kuzipata fedha hizi twende tukalipe kwa wakati na wahandisi wa maji mikoani na wilayani msilete visingizio vya aina yoyote, fedha zinapofika mikoani au wilayani makandarasi wakalipwe fedha zao,” ameagiza.

“Maana wakati mwingine fedha zinaweza zikafika vikaanza visingizio vya kufanya tathmini, inakuwaje kufanya tathimini kutaja kiasi chote hicho maana yake uhakiki umeshafanyika. Muondoe visingizio, makandarasi wakalipwe fedha zao na niwaombe sana makandarasi fedha hizi mnazoenda kupewa nendeni mkafanye kazi, lakini kwa wale ambao watakuwa siyo wafanya kazi tutaendelea kushughulikiana,” amesema.

Naibu Waziri wa Maji, Mathew amesema mita za malipo kabla ya matumizi ndiyo suluhisho la matumizi mabaya ya maji, upotevu wa maji, kubambikiwa ankara na malimbikizo ya madeni.

“Malimbikizo ya madeni hapa wabunge wameongelea hata taasisi za Serikali zipo, ni kweli kabisa na changamoto hiyo tunaifahamu, hiyo ni changamoto na sisi tunaichukua na kwa kutumia mita za malipo kabla ya matumizi hakutakuwa na mgogoro na taasisi yoyote ile tunayoidai kwa sababu kila mtu atakuwa anajipimia kile ambacho anataka kukitumia, tunaenda kutatua hilo tatizo,” amesema Mathew.

Awali, Kamati ya Bunge katika maoni yake yaliyosomwa bungeni na mwenyekiti, Jackson Kiswaga ilieleza kutoridhishwa na bajeti hiyo kwa kuwa fedha za maendeleo ya wizara hiyo zimepungua na kunaweza kuathiri utekelezaji bora wa miradi ya maendeleo kwa kukosa tija iliyokusudiwa kwa wananchi.

“Makadirio ya bajeti yote ya Wizara ya Maji yamepungua kwa asilimia 17 ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2023/24.”

“Makadirio ya matumizi kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo yamepungua kwa kiasi cha Sh137.7 bilioni, sawa na asilimia 18.4 ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Ni mtazamo wa kamati kwamba, kupungua kwa kiasi hiki cha bajeti ya maendeleo kutaathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2024/25,” amesema Kiswaga.

Amesema kuwa makadirio ya matumizi ya kawaida yameongezeka kwa kiasi cha Sh9.2 bilioni sawa na asilimia 1.2 ya bajeti ya mwaka wa fedha unaoisha.

“Kamati haijaridhishwa na bajeti hii, kwani haijazingatia ipasavyo maelekezo kwa Serikali yaliyomo kwenye Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020-2025.

“Ilani ya CCM imeahidi kuimarishwa kwa huduma ya majisafi na salama ili ifikapo mwaka 2025 wakazi asilimia 85 waishio vijijini na asilimia 95 ya wakazi waishio mjini wawe wamefikiwa na huduma hiyo.

“Msisitizo wa Kamati kwa Serikali ni kuhakikisha bajeti ya Wizara ya Maji inaongezwa kwa Sh137.7 bilioni, ili angalau ibaki kama ilivyokuwa mwaka wa fedha 2023/24,” amesema.

Related Posts