Tunapokaribia mwaka mpya ni kawaida kutafakari juu ya mafanikio yetu na kuweka malengo kwa siku zijazo. Iwe ni kupiga hatua kazini, kuimarisha mahusiano au kufanikisha malengo binafsi.
Lakini kuna jambo moja muhimu ambalo linapaswa kupewa kipaumbele, nalo ni kujali afya yako.
Maana si jambo geni kusikia mtu wa karibu au tunayemfahamu kapata changamoto ghafla au amepoteza maisha, kutokana na tatizo la kiafya aliloishi nalo kwa miaka mingi bila yeye kujua.
Tanzania, magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) na magonjwa ya kuambukiza bado ni changamoto kubwa za afya.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hapa nchini magonjwa kama vile shinikizo la damu, kisukari na saratani yanachangia zaidi ya asilimia 33 ya vifo, wakati magonjwa ya kuambukiza kama VVU na homa ya ini yanaendelea kuwa changamoto.
Magonjwa haya mara nyingi humtafuna mtu kimya kimya, dalili zikitokea tu pale ugonjwa unapokuwa mkubwa na madhara yameanza kuonekana kwa wazi.
Lakini uchunguzi wa mara kwa mara husaidia kuyagundua mapema, kuokoa maisha na kupunguza gharama za matibabu.
Kwa mfano shinikizo la damu, ambalo mara nyingi huitwa ‘muuaji wa kimya’ linakadiriwa kuathiri karibu mtu mmoja kati ya watu wazima wanne nchini, lakini bahati mbaya wengi hawafahamu hali yao.
Vilevile magonjwa kama maambukizi ya VVU na homa ya ini ya aina B (Hepatitis B) kwa baadhi bado hubainika wakati ugonjwa umeshakua na kufikia hatua za juu.
Magonjwa haya yanaweza kugunduliwa na kudhibitiwa mapema kupitia uchunguzi wa afya wa mara kwa mara.
Uchunguzi wa kawaida wa mwili ni msingi wa tathmini ya afya yako. Daktari wako atapitia historia yako ya matibabu, mtindo wako wa maisha na hali yako ya afya kwa ujumla. Pia atapima uzito wako, shinikizo la damu na kusikiliza moyo na mapafu pamoja na viungo vingine.
Kipimo cha urefu na uzito ni muhimu kwa kukokotoa BMI (Body Mass Index) yako, ambayo husaidia kutathmini hatari yako ya kupata magonjwa kama vile ugonjwa wa moyo, kisukari cha aina ya pili na saratani fulani. Ikiwa BMI yako haipo katika kiwango cha afya, daktari wako atakushauri hatua za kuchukua.
Shinikizo la damu ni kiashiria muhimu cha afya ya moyo na mishipa. Watu wazima wanapaswa kupima angalau kila mwaka au mara kwa mara ikiwa wana historia ya shinikizo la damu, hasa katika familia. Shinikizo la kawaida ni 120/80 mmHg au chini, wakati 130/80 mmHg au zaidi linaonyesha shinikizo la damu.
Kiwango cha juu cha cholesterol huongeza hatari ya ugonjwa wa moyo na kiharusi. Watu wazima zaidi ya miaka 20 wanapaswa kupima cholesterol yao kila baada ya miaka minne hadi sita, lakini wale walio na historia ya ugonjwa wa moyo au hali kama kisukari wanapaswa kupimwa mara kwa mara.
Kisukari kinaongezeka kwa kasi nchini. Kipimo cha sukari ya damu kinaweza kugundua hali ya prediabetes au kisukari mapema na hivyo kuzuia matatizo kama ugonjwa sugu wa figo, upofu, kupoteza viungo, ugonjwa wa moyo na mishipa ya damu.
Uchunguzi wa kawaida unashauriwa kuanzia umri wa miaka 45 au mapema ikiwa una uzito kupita kiasi, shinikizo la damu au historia ya familia ya kisukari.
Uchunguzi wa magonjwa ya kuambukiza ni muhimu. Hapa Tanzania, magonjwa ya kuambukiza kama VVU na homa ya ini ya aina B bado ni changamoto kubwa za afya.
Kufanya uchunguzi wa magonjwa haya ni muhimu kwa sababu utambuzi wa mapema unaruhusu matibabu ya haraka, kupunguza matatizo na kuzuia maambukizi.
VVU bado ni tatizo na baadhi yetu bado hatufahamu hali ya maambukizo. Kipimo ni cha haraka, cha siri na huokoa maisha. Matibabu ya mapema yanaweza kusaidia watu walio na VVU kuishi maisha marefu na yenye afya.
Uchunguzi wa homa ya ini. Homa ya ini ya aina B mara nyingi husababisha uharibifu wa ini au saratani. Uchunguzi unaruhusu chanjo kwa walio katika hatari na matibabu kwa walioambukizwa.
Uchunguzi wa saratani ya matiti ni muhimu. Hii ni saratani inayoathiri zaidi wanawake nchini. Uchunguzi wa mapema huokoa maisha na unahusisha njia mbili kuu;
Uchunguzi wa matiti; Mtoa huduma za afya atapima matiti kwa mkono ili kugundua uvimbe au mabadiliko yasiyo ya kawaida. Njia hii ni hatua ya awali ya uchunguzi.
Mammogramu; Hiki ni kipimo maalum cha eksirei kinachochunguza ndani zaidi ya tishu za matiti kutambua uvimbe au mabadiliko ambayo hayawezi kugunduliwa kwa mkono. Kipimo hiki kinapendekezwa kwa wanawake kuanzia umri wa miaka 40 au mapema ikiwa wana historia ya familia ya saratani ya matiti.
Uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na tezi dume
Saratani ya shingo ya kizazi; Saratani hii ni chanzo kikuu cha vifo kwa wanawake nchini. Pap smear na kipimo cha HPV vinaweza kugundua mabadiliko ya awali na hivyo kuruhusu matibabu mapema. Wanawake wanapaswa kuanza uchunguzi kuanzia umri wa miaka 21.
Saratani ya tezi dume; Hii ni saratani inayoongoza kuathiri wanaume nchini. Inashauriwa kuanza uchunguzi kati ya umri wa miaka 40-45 huku wengine wakianza miaka 50. Uchunguzi unahusisha kipimo cha damu aina ya PSA au uchunguzi mwingine kulingana na ushauri wa daktari.
Uchunguzi wa meno ni muhimu. Afya bora ya kinywa ni muhimu kwa ustawi wa jumla. Uchunguzi wa meno unaweza kugundua matatizo kama mashimo ya meno na magonjwa ya fizi mapema. Tembelea daktari wa meno angalau mara moja kwa mwaka.
Pia vipimo vingine mbali na vile vya msingi kama shinikizo la damu na sukari, vipimo vingine kama kipimo cha figo, full blood picture (FBP) na vipimo vya ini vinaweza kupendekezwa kulingana na hali ya afya yako.
Kipimo cha figo husaidia kugundua matatizo kama maambukizi au kushindwa kwa figo, wakati FBP hutoa picha ya jumla ya afya ya damu, ikigundua matatizo kama upungufu wa damu au maambukizi.
Vilevile, vipimo vya ini husaidia kubaini matatizo ya ini kama homa ya ini na changamoto nyingine za ini kama ‘cirrhosis’ na vipimo vingine kama vya uric acid au thyroid vinaweza kupendekezwa kwa dalili maalumu kama maumivu ya viungo au uchovu wa kupindukia.
Hata hivyo, vipimo hivi vinategemea tathmini ya daktari wako, ambaye atazingatia historia yako ya afya, dalili zako na hatari za magonjwa kulingana na umri, jinsia na mtindo wako wa maisha.
Ni muhimu kujadili na daktari wako ili kuchagua vipimo vinavyofaa zaidi kwa afya yako. Lengo kuu ni kugundua matatizo mapema, kuzuia matatizo makubwa na kuhakikisha unadumisha afya bora kwa muda mrefu.
Watu wengine huepuka uchunguzi wa afya kwa sababu ya hofu. Hofu ya kugundua ugonjwa au dhana potofu kwamba hawahitaji uchunguzi ikiwa wanajisikia vizuri.
Hata hivyo, kuepuka daktari hakumalizi hatari za kiafya, badala yake kunaongeza uwezekano wa matatizo kuwa makubwa. Kinga daima ni bora kuliko tiba na kugundua matatizo mapema huokoa maisha, hupunguza gharama za matibabu na huepusha mateso ya muda mrefu.
Anza mwaka mpya ukiwa na afya bora. Mwaka unapofikia mwisho, jipatie na wapendwa wako zawadi ya afya. Panga kufanya uchunguzi wa kila mwaka ili kuhakikisha unaanza mwaka mpya ukiwa na afya njema.
Kumbuka, uchunguzi huu si wa kugundua matatizo tu, ni njia ya kuyazuia na kujipa uwezo wa kuishi maisha yenye furaha na afya bora. Tembelea kliniki au hospitali iliyo karibu nawe na panga miadi yako leo. Kujali afya yako sasa kunahakikisha unaweza kufurahia fursa na changamoto za mwaka mpya.
Dk Norman Jonas Kyala ni Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na Mratibu wa huduma za afya ngazi ya jamii, idara ya kinga – Wizara ya Afya