Simba, Yanga wabadilisha upepo Ligi Kuu, ufungaji nako moto

KATIKA Ligi Kuu Bara, upepo umegeuka. Simba na Yanga na nyota wa kigeni wamepindua meza kama utani na kuifanya ligi iliyopo raundi ya kwanza ya duru la pili,  hali iwe tofauti na ilivyokuwa awali au katikati ya duru la kwanza litakalofungwa rasmi wikiendi na vigogo.

Ndio. We, angalia msimamo ulivyo ndo utajua upepo umegeuka vipi? Awali kulikuwa na mchuano kati ya Singida Black Stars, Tabora United, Fountain Gate na Azam FC, lakini kwa sasa ni tofauti. Eneo la juu kuna wababe wawili tu, Simba na Yanga wanaotunishiana misuli ikijiandaa kukamilisha duru la kwanza.

Pia katika mbio za ufungaji, upepo umebadilika baada ya wazawa kuanza na kasi wakiongozwa na Seleman Mwalimu na Edgar Williams wa Fountain Gate ambao sasa wamefunikwa nyota wa kigeni wakiongozwa na Mkenya Elvis Rupia wa Singida, Jean Charles Ahoua wa Simba wanaofukuzana kileleni.

Wakati duru la kwanza likihitimishwa kwa mechi za Singida v Simba na ile ya Yanga dhidi ya Fountain, lakini hadi jana mchana jumla ya mabao 248 yalikuwa yamefungwa katika mechi 118, huku Rupia akiwa kinara akimiliki manane, moja zaidi na aliyonayo Ahoua aliyefunga saba, ilihali Mwalimu aliyekuwa akiongoza kwa muda mrefu akiwa na sita, huku wachezaji watano wakiwamo wazawa wawili na wageni watatu kila mmoja akiwa na matano.

Peter Lwasa wa Kagera Sugar, Leonel Ateba wa Simba na Prince Dube wa Yanga ni wageni wanaomiliki matano kila mmoja sawa na Clement Mzize wa Yanga na Edgar wa FOG ambao ni wazawa, ilihali nyota waliotamba msimu uliopita Stephane Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam wanaojitafuta.

Simba na Yanga zikitoka katika jukumu la mechi za kimataifa wakati timu nyingine zikikamilisha duru la kwanza, zimerudi kwa kasi zikila ‘viporo’ ilivyokuwa navyo kabla ya wikiendi hii kuhitimisha, lakini wakibadilisha upepo kwa kuzing’oa Azam na Singida zilizokuwa zikipokezana juu kwa muda mrefu.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 37 kwa mechi 14, ikiizidi Yanga yenye 36 kwa idadi sawa za mechi, huku Singida na Azam zikiwa nyuma kila ina 33,  zikicheza 15 kila moja na iwapo wikiendi vigogo vitashinda vitazidi kujiimarisha.

Hali ikiwa hivyo, ni kwamba katika mechi 118 (kabla ya jana kati ya Pamba na Prisons) mabao 248 yalikuwa yamefungwa, wageni 46 wakitupia 105 na wazawa 76 wakifunga 137 na mengine sita yakiwa ni ya kujifunga kupitia wageni wawili na wazawa wanne.

Makipa Daniel Mgore wa Dodoma Jiji na Mohamed Mustafa wa Azam pamoja na  nyota wengine wakiwamo Yannick Bangala aliyekuwa Azam, Fred Tangalo (KMC), Kelvin Kijiri (Simba) na Dickson Mhilu (Dodoma Jiji) ndio waliojifunga, huku Rupia akiongoza kwa wafungaji wote hadi sasa akiwa na manane.

Mkenya huyo alifikisha idadi hiyo mechi iliyopita Singida ilipoilaza KenGold 2-1, akifuatiwa na Ahoua aliyefunga saba na kuasisti nne akilingana na Fei Toto katika orodha ya  waliohusika na mabao mengi kila mmoja akiwa na 11. Fei amefunga manne na kuasisti saba akiwa kinara kwa asisti. Msimu uliopita Fei alimaliza na 19 na asisti saba, akizidiwa na Aziz KI aliyefunga 21 na asisti nane, ambao hadi sasa wanaendelea kujitafuta.

Kwa wazawa, Seleman licha ya kutocheza na kutofunga muda mrefu ndiye anayewaongoza akiwa na sita, akifuatiwa na Edgar na Mzize wenye matano, sawa na Ateba, Lwasa na Dube wanaofuata katika orodha ya wageni wenye mabao mengi baada ya Rupia na Ahoua.

Wazawa wamechanganyamka zaidi kwa wenye mabao manne, wakiwa wanane akiwemo beki wa Yanga, Ibrahim Bacca, Paul Peter (Dodoma Jiji), Offen Chikola (Tabora Utd), Nassor Saadun na Fei Toto (Azam), Maabad Maulid (Coastal Union), Ibrahim Joshua (KenGold) na Salum Kihimbwa (Fountain Gate).

Nyota wa kigeni wanaochuana na kina Fei (kabla ya jana) ni; Yacouba Songne (Tabora Utd), Marouf Tchakei (Singida BS) na Steven Mukwala (Simba), huku kipa wa Simba, Moussa Camara akiongoza kwa clean Sheet akiwa na 11 kwa mechi 14, akifuatiwa na mzawa Patrick Munthary wa Mashujaa mwenye nane.

Rekodi zinaonyesha katika mabao 105 yaliyofungwa na wageni, 16 ni ya nyota kutoka DR Congo, ikifuatiwa na Ivory Coast iliyochangia 15, huku Kenya na Uganda ikifuatia kwa kufunga 11.

Related Posts