KAMA wewe ni mcheza au mchezeshaji mchezo wa dubwi (Slot) mtaani na unafanya kinyume cha sheria, jiandae tu kwa sasa, kwani Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) imeanza msako ikiwatumia wenyeviti wa Serikali za Mitaa.
Mkurugenzi Mkuu wa GBT, James Mbalwe alisema jana wamepokea malalamiko ya baadhi ya watu kuendesha mchezo wa Sloti (dubwi) kinyume cha sheria ikiwamo kuendeshwa katika nyumba binafsi za watu.
“Pia wapo waliowahusisha watoto chini ya miaka 18 ambao kisheria hawaruhusiwi, kucheza michezo ya kubahatisha,” alisema Mbelwa na kuongeza, pamoja na mchezo wa dubwi upo kisheria, wapo wachezeshaji wanaouendesha kinyume cha sheria bila leseni.
“Hawa ndio wanaosababisha sintofahamu hii huko mitaa, hivyo tutawatumia wenyeviti wa mitaa ili kutokomeza uchezaji wa ma dubwi mitaani kinyume na utaratibu,” alisema Mbalwe akifafanua mchezo wa dubwi una maeneo yake maalumu ya kuwekwa mashine hizo ikiwamo kwenye baa na maeneo mengine ya starehe.
“Tumewapa wenyeviti wa Serikali za mitaa semina kuhusu uhalali wa mchezo huu, nani anastahili kucheza na eneo gani, hili tumelifanya kwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Dar es Salaam ambako ndiko kuna biashara kubwa ya michezo ya Sloti (dubwi) kisha tanakwenda mikoani.”
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Dar es Salaam, Juma Abbas, alikiri wamepewa semina na GBT iliyowapa mwanga wa kutambua mashine za dubwi ambazo si sahihi.
“Mwanzo hatukufahamu ipi ni sahihi na ipi si sahihi na mahala gani ichezwe ili kudhibiti japo malalamiko yalikuwa ni mengi,” alisema.