Hatua kwa hatua pambano la KO ya Mama

Unaweza kusema ilikuwa ni zaidi ya burudani kwa Watanzania katika pambano la Knock Out ya Mama lililoanza usiku wa jana Desemba 26 na kufikia tamati saa 12 asubuhi ya leo Desemba 27, 2024 kwenye ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini hapa.

Pambano hilo lililowakutanisha mabondia kutoka Ufilipino, Burundi, Afrika Kusini, Nigeria na wenyeji Tanzania, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.

Rais Samia Suluhu Hassan alinogesha pambano hilo kwa kutoa bonasi ya Sh10 milioni kwa Watanzania watakaoshinda mikanda ya ubingwa kwa Knock Out (KO) na Sh5 milioni kwa ushindi wa pointi na zawadi ya Boxing Day Sh1 milioni kwa mabondia waliocheza na wageni mapambano ya kimataifa yasiyokuwa ya ubingwa.

Bonasi hiyo ya Rais, sanjari na simu aliyowapigia mashabiki na mabondia katikati ya pambano usiku wa kuamkia leo viliongeza hamasa.

Kwa nyakati tofauti, mabondia walioshinda walisema hamasa waliyopewa na Rais na ujio wa Waziri Mkuu ilikuwa ni chachu kwao kupambana.

Katikati ya pambano hilo, Rais Samia alimpigia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kueleza kufuatilia mubashara.

Rais Samia ambaye aliwatakia mchezo mzuri mabondia na kuwapa salamu ya Sikukuu ya Krismasi na kuwatakia mwaka mpya mwema, alisema: “kilichonipa hamasa ni jina la mchezo Knock Out ya Mama.

“Wosia wangu mcheze vizuri, sheria zifuatwe,” amesema Rais Samia alipokuwa akizungumza na mashabiki na kuwataka mabondia kuiheshimisha nchi.

“Nimesikia kuna mabondia kutoka nje ya nchi, mabondia wetu Watanzania mpewe bendera ya taifa na mpiganie taifa lenu,” amesisitiza Rais Samia.

Baada ya simu ya Rais, Waziri Mkuu alieleza namna mchezo wa ngumi unavyopendwa nchini na kuwa ni mchezo wa tatu kupendwa baada ya soka na kikapu.

Viongozi wengine waliokuwepo ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paramagamba Kabudi na katibu wake, Gerson Msigwa, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa na viongozi wengine.

Mikanda yote yabaki Tanzania

Furaha ya Watanzania imeongezeka zaidi baada ya mabondia watano kutwaa mikanda ya ubingwa.

Mtanzania aliyefungua dimba la ubingwa ni Yohana Mchanja aliyetwaa ubingwa wa World Boxing Organisation Global Championship dhidi ya Miel Farjado kutoka Ufilipino.

Salmin Kassim aliyemchapa Adrian Lerassan wa Ufilipino kwa pointi za majaji 3-0, alitwaa ubingwa wa mabara wa World Boxing Federation (WBF) katika uzani wa super bantam.

Wakati Ibrahim Mafia ametwaa ubingwa wa World Boxing Champion (WBC) Africa kwa kumchapa Lusizo Manzana wa Afrika Kusini.

Jaji namba moja alimpa pointi 97-92, jaji namba mbili pointi 95- 94 na jaji namba tatu 96-93 pambano ambalo Mtanzania huyo alipata cutting ya jicho la kushoto raundi ya kwanza.

Said Chino ametetea ubingwa wa mabara wa International Boxing Association (IBA) kwa kumchapa kwa pointi Michael Klassen wa Afrika Kusini.

Wakati Kalolo Amir naye akishinda kwa pointi dhidi ya Shile Jelwana wa Afrika Kusini na kutwaa ubingwa wa Pugilistic Syndicate of Tanzania (PST).

Mabondia hao kila mmoja alikabidhiwa kitita cha Sh5 milioni kama bonasi ya ushindi huo.

Bonasi hiyo imetolewa na Rais Samia ambaye aliahidi Sh10 milioni kwa bondia Mtanzania atakayeshinda ubingwa kwa KO na Sh5 milioni kwa atakayeshinda kwa pointi huku mapambano yasiyokuwa ya ubingwa, kila Mtanzania aliyeshinda ameondoka na zawadi ya Boxing Day ya Sh1 milioni.

Mapambano mengine haya hapa

Katika mapambano mengine yasiyokuwa ya ubingwa, Maisha Samson alichapwa kwa Techinical Knock Out (TKO) sekunde ya 218 ya pambano dhidi ya Mtanzania mwenzake, Juma Thabiti.

Konde la kulia la Thabiti lilimpata sawia Maisha na kumpeleka chini na kuhesabiwa kabla ya kusalimu amri kwa kuruhusu kipigo cha TKO.

Omari Omari pia alikutana na kipigo kama hicho dhidi ya Shauri Athumani katika raundi ya tano.

Omari alishambuliwa kabla ya kupiga goti moja chini akionyesha ishara ya kuumia mkono wa kushoto kisha refarii kuonyesha ishara ya kumaliza pambano hilo la utangulizi.

Luqman Kimoko alimchapa Bismark Saah wa Ghana kwa pointi. Majaji wawili walitoa pointi 79- 73 kwa Kimoko huku mmoja akitoa sare ya pointi 76-76.

Mtanzania Ramadhan Ramadhan alimchakaza Manish wa India kwa pointi za majaji wote. Majaji wawili walitoa ushindi wa pointi 59-55 kila mmoja kwa Ramadhani huku jaji namba tatu akitoa pointi 60-54.

Leila Macho alimchapa Agnes Mtimaukanena wa Burundi kwa pointi za majai 3-0 baada ya majaji wawili kila mmoja kumpa ushindi wa pointi 59-55 na jaji namba tatu kumpa ushindi wa pointi 58-56.

Bondia namba moja nchini, Fadhil Majiha alimchapa kwa pointi za majaji wote, John Zile wa Ghana.

Mganda Latibu Muwonge alikalishwa kwa kipigo cha TKO na Abbada Cadabra dakika ya 2 na sekunde 22.

Huku Abdulrahman Magoma akishinda kwa pointi za majaji wote dhidi ya Festus Simon.

Bondia wa India, Gurpreet Signh alipigwa kwa TKO dakika ya 1:50 na Said Bwanga baada ya kuumia mkono wa kulia ulingoni.

Wakati Salim Mtango ‘Mesi wa ngumi’ akikutana na zomea zomea ya mashabiki baada ya kutangazwa mshindi kwa pointi dhidi ya Azeez Lateef wa Nigeria.

Related Posts