KLABU ya Fountain Gate a.k. a FOG imekamilisha usajili wa aliyekuwa winga wa Mtibwa Sugar, Kassim Haruna ‘Tiote’ kwa mkataba wa mwaka mmoja, baada ya dili la nyota huyo kukwama mwanzoni mwa msimu huu kutokana na kushindwa kufikia makubaliano.
Nyota huyo wa zamani wa Polisi Tanzania na Namungo amejiunga na kikosi hicho chenye makazi yake mjini Babati akiwa ni mchezaji huru, ikiwa ni pendekezo la kocha mkuu wa timu hiyo, Mohamed Muya ili akaongeze makali safu ya ushambuliaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tiote alisema ni kweli yupo hatua za mwisho za kujiunga na kikosi hicho, huku akiweka wazi ni muda mzuri kwake wa kuanza kuonekana tena katika michezo ya Ligi Kuu Bara, baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kucheza.
“Licha ya kukaa nje kwa muda mrefu ila nilikuwa nafanya mazoezi na nashukuru nimeipata nafasi ya kuichezea Fountain kwa mwaka mmoja, siwezi kuwaahidi sana makubwa mashabiki zangu ila ninachoweza kuwaambia watarajie mambo mazuri,” alisema Tiote, huku kocha wa FOG, Mohamed Muya alisema muda ukifika wa kutangaza nyota wapya watafanya hivyo, ingawa tayari alishatoa ripoti kwa viongozi na anashukuru wanaendelea kuifanyia kazi ili kuboresha kikosi hicho.
“Mapendekezo yote nilishayatoa kutokana na upungufu tuliokuwa nao, kama Haruna ni miongoni mwao basi tutaona muda ukifika kwa sababu bado usajili uko wazi, kikubwa nilichozingatia ni upatikanaji wa wachezaji bora na wenye uzoefu,” alisema Muya.
Mbali na ‘Tiote’, nyota wengine wapya waliosajiliwa na timu hiyo ni mabeki, Said Mbatty na Faria Ondongo kutoka Tabora United, Jackson Shiga (Coastal Union), Mtenje Albano (Dodoma Jiji) na Jimmyson Mwanuke aliyetokea Singida Black Stars.