Jicho la wadau minyukano makada wa Chadema mitandaoni

Dar es Salaam. Uchaguzi kuwapata viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) unaotarajiwa kufanyika Januari 21, 2025 unatajwa utaamua anguko au kuimarika zaidi kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Anguko litatokana na kilichoelezwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa, kwa namna minyukano inavyoendelea kuna dalili mgombea atakayeshindwa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa, huenda ataondoka na wafuasi wake.

Lakini kuimarika zaidi kwa Chadema kutatokana na iwapo uchaguzi utamalizika na wagombea wawili kati ya Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa sasa) na Tundu Lissu (Makamu Mwenyekiti -Bara), wataungana kuendeleza ujenzi wa chama hicho.

Mitazamo ya wanazuoni hao inatokana na hali halisi ya minyukano ya makada wa chama hicho inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, kati ya wanaomuunga mkono Mbowe na wale wa Lissu katika nafasi ya uenyekiti wa Chadema taifa.

Kila upande unatumia mitandao hiyo kuonyesha uhalali wa mgombea unayemuunga mkono, huku ukionyesha udhaifu wa mwingine.

Lissu na Mbowe si wagombea pekee wa nafasi hiyo, licha ya minyukano kuonekana zaidi kwa wafuasi wao, wengine waliochukua fomu kuutaka uenyekiti ni Romanus Mapunda na Charles Odero.

Hata hivyo, chaguzi ndani ya Chadema haziishii nafasi ya uenyekiti taifa, upo utakaohusisha viongozi wa mabaraza ya chama hicho, ingawa minyukano imebaki kwa Lissu na Mbowe.

Akizungumza na Mwananchi, mchambuzi wa siasa, Kiama Mwaimu anasema minyukano inayoendelea inaweza kuiimarisha au kuidhoofisha Chadema baada ya uchaguzi.

Anafananisha kinachoendelea Chadema sasa sawa na kilichowahi kutokea kwa Chama cha Wananchi (CUF), kati ya hayati Maalim Seif Sharrif Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba. Minyukano ilikidhoofisha chama hicho.

“Watu hawa wawili (Lissu na Mbowe), wote wana nguvu, ingawa naona nguvu ya watu wa kawaida ipo sana kwa Lissu kuliko kwa Mbowe anayeungwa mkono na watu wengi hasa viongozi wa mikoa. Sasa sijui hawa wanaomuunga mkono Lissu ni watu wanaopiga kura?

“Kwa ujumla nikitazama picha naona Lissu ana watu wengi wanaomuunga mkono, lakini siyo wengi wapigakura. Lakini najua matokeo yote ya uchaguzi yatakuwa na mambo mawili kukiimarisha Chadema kama vile kimepikwa upya kwenye tanuri au kukidhoofisha kisiweki tena,” anasema.

Mchambuzi wa siasa na jamii, Ramadhani Manyeko anasema yanayoendelea ndani ya chama hicho ni mafahari wawili (Mbowe na Lissu) wanapigana.

Anasema kwenye vita vya mafahari wawili zinazoumia ni nyasi, akifafanua baada ya uchaguzi huenda chama hicho kikuu cha upinzani nchini kikagawanyika.

“Kuna uwezekano ukatokea ufa mkubwa baada ya uchaguzi wa Januari, 2025. Busara inahitajika kutumika kwa mmoja wapo kumuachia mwenzake.

“Lakini wakienda wote kuna uwezekano mkubwa wa kuleta mpasuko, kwa sababu ukisikiliza mazungumzo ya Lissu kuna wakati anatoa madai huenda uchaguzi huo ukavurugika endapo utafanyika usiku, badala yake ameshauri kura zipigwe mchana kweupe,” anasema.

Anasema kunapokuwa na dalili kama hizo huenda kukatokea ufa ndani ya Chadema, akisisitiza busara zinamtuma mmoja amuachie mwenzake ili kukinusuru chama hicho.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalaam (UDSM) na mchambuzi wa siasa, Dk Faraja Kristomus anasema Mbowe anaungwa mkono na viongozi wa Chadema kuanzia ngazi ya kitaifa na mikoa na kwa muda mrefu inadaiwa amekuwa akiwaunga mkono baadhi yao walioshinda chaguzi ngazi za chini.

Desemba 12, 2024 Lissu akitangaza nia kuwania uenyekiti, alizungumzia hilo akieleza hata kama wanaomuunga mkono ni wale walioshindwa: “Nitakwenda na loosers (walioshindwa) wenzangu.”

“Hawa wanaomuunga mkono ndio wajumbe wa mkutano mkuu walio wengi, ukiangalia kwa jicho hilo unaweza ukasema Lissu atapoteza kwenye uchaguzi. Lakini wakati mwingine hali ya hewa inabadilika kutokana na kampeni mtu anazoifanya,” amesema Dk Kristomus.

Anasema Lissu anaungwa mkono na vijana huru, siyo kwa mikakati yake bali watu wanaomkubali wengi ni vijana.

“Ingekuwa uchaguzi wa kawaida kwa wanachama wote kupiga kura, Lissu angemgaragaza Mbowe kwa kiasi kikubwa, kwa sababu wanachama wengi ni vijana, hata wale wenye umri mkubwa wanatamani kuona mabadiliko au mageuzi ya kisiasa kupitia Chadema.

“Kiuhalisia Lissu siyo mtu wa mikakati, lakini Mbowe ni mbobevu kwenye siasa, sasa hapo ni ushindani. Lakini ni mchuano pia kati ya mtu anayependwa kwa asili na wanachama wa kawaida na mwingine anayependwa kwa sababu ya faida yake kwa viongozi wengine,” alisema Dk Kristomus.

Hatima ya Lissu, Mbowe baada ya uchaguzi

Wanaomuunga na kunufaika na uwepo wa Mbowe ndio wanaongoza kukabiliana na watu wa mitandao. Wakati wanaomuunga mkono na kudhani Lissu anastahili kuwa mwenyekiti wanajitolea kukabiliana na makundi yanayomzungumzia mwanasiasa huyo.

“Katika mazingira hayo mnyukano ni mkali, lakini kwa nje unaweza ukasema mechi itamuegemea Mbowe kwa sababu ya aina ya mikakati yake anayojiwekea na watu wanaomuunga mkono. Lakini inawezekana baadhi ya wajumbe hao wakashawishika kwa namna moja au nyingine wakawa upande wa Lissu.

“Mnyukano huu nauangalia kwa pande mbili, ikitokea Lissu ameshinda uwezekano mkubwa Mbowe kubaki Chadema upo, lakini Lissu asiposhinda uenyekiti, kwa hali ilivyo basi uwezekano mkubwa wafuasi wanaomuunga mkono wakatimkia vyama vingine na kusababisha anguko ndani ya Chadema,” amesema Dk Kristomus.

Minyukano inayoshuhudiwa katika mitandao ya kijamii kati ya makada wa Chadema, si jambo la ajabu na mtaji kwa chama hicho kuonyesha siasa za ushindani wa hoja, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo.

Kuhama au kuendelea kubaki ndani ya Chadema kwa mgombea yeyote atakayeshindwa anasema kutatokana na mtazamo wa wagombea wenyewe.

“Kwa sababu kama mtu umeingia kwenye ushindani kama hauko tayari kushindwa basi umeingia kwa nia mbaya, kwa sababu kama uamuzi unafanywa kwa kura basi majibu mawili utashinda au utashindwa,” amesema.

Dk Masabo anasema wanaoshangaa minyukano ya mitandaoni ni kwa sababu Tanzania hakuna utamaduni wa ushindani ndani ya vyama vya upinzani.

Anasema vyama vya upinzani vimekosa wanachama wenye ushawishi kwa muda mrefu, hivyo wachache wakiibuka, wengine ama wanaogopa au wanaamua kutoendelea kutia nia.

“Si kitu cha kawaida kuona upinzani mkali ndani ya vyama vya siasa. Tofauti na huko nyuma hivi sasa wagombea wote wameeleza hadharani nia yao ya kugombea,” anasema.

Anasema kinachopaswa kufanyika ni kutathmini hotuba za Lissu na Mbowe zinatoa ujumbe gani, badala ya kufikiria mashabiki wenye mambo mengi.

Anasema Lissu ndiye aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti aliyekiongoza chama hicho wakati Mbowe akiwa mahabusu kwa miezi minane na Chadema iliendelea kuwa imara.

“Kwa hiyo, sidhani wanaombeza Lissu kama wanachukulia historia, wanajua chama kimepitia nyakati gani, ndiyo maana nasema mimi natazama zaidi hotuba za hawa watu wawili,” amesema.

Dk Masabo anasema mgombea mmoja ana mtaji wa kujenga chama kwa rasilimali zake, lakini mwingine ana mtaji wa kujenga chama kutokana na ujuzi na uzoefu wake wa kujenga hoja.

“Wote wana mitaji miwili tofauti ambayo yote ni muhimu kisiasa, sasa kama mtakuwa mnafanya siasa halisi nadhani wajumbe wa mkutano mkuu wana nafasi kubwa na nzuri ya kufanya uchaguzi halisi kuliko miaka yote, kwa sababu kuna wagombea wawili wenye ushawishi mkubwa na misingi iliyoegemea kwenye rasilimali mbili tofauti,” anasema.

Anasema minyukano inayoendelea kama haina nia mbaya inatoa fursa nzuri ya kukijenga chama hicho kidemokrasia.

“Kwa mara ya kwanza mkutano mkuu watakuwa na nafasi nzuri ya kufanya uchaguzi kwa kuwa na watu wawili wenye ushawishi unaovutana kwa karibu, lakini watatuma ujumbe kwa upande wa pili kwa sababu siasa watakazokuwa wamefanya ni ishara ya siasa zitakazofanyika katika uchaguzi mkuu 2025,” amesema.

Wakati makada wakitangaza nia na kuchukua fomu kwa nafasi za uenyekiti wa taifa, ujumbe wa kamati kuu na mabaraza ya chama hicho ambayo ni vijana, wanawake na wazee; ukimya umetawala nafasi ya makamu mwenyekiti- Bara.

Licha ya baadhi ya makada kutajwa kuwania nafasi hiyo, akiwamo Ezekia Wenje aliyetangaza nia kabla ya mchakato kuanza, inadaiwa hakuna aliyejitokeza kuchukua fomu, huku zikibaki siku nane kabla ya pazia la kuchukua na kurejesha fomu kufungwa.

Related Posts