Mtendaji wa kijiji adaiwa kujinyonga kisa ugumu wa mazingira ya kazi

Sikitu Mwasubila (31) anadaiwa kujinyonga katika mtaa wa Melinze mjini Njombe Disemba 24, 2024 kisa ugumu wa mazingira ya kazi.

Inaelezwa kuwa Mwasubila alikuwa Mtendaji wa kijiji cha Mkwayungi mkoani Dodoma ambapo alipata kazi hiyo hivi karibuni na siku kadhaa zilizopita alirudi mjini Njombe anapoishi mume wake kabla ya kujinyonga.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe ACP. Mahamoud Banga amethibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa siku hiyo Marehemu aliandika ujumbe wa kuwaomba radhi ndugu na Mume wake kwa maamuzi aliyoyachukua.

“(Marehemu) aliacha ujumbe kwamba ndugu zake wamsamehe kwa maamuzi haya ambayo ameyachukua na kwamba mume wake sasa aendelee na maisha na mzazi mwingine ambaye huyo mume wake alizaa naye”amesema Banga

Aidha Banga amesema kufuatia operesheni mbalimbali mkoani humo wamefanikiwa kumkamata Regan Sanga (Kihelikopta) akituhumiwa kuongoza genge la wahalifu ambapo mtuhumiwa aliwaongoza Askari na kufanikisha kukamata simu ndogo mpya 25, Simujanja(Smartphone) 9, betri za simu 11, flash 25, Memory Card 7, Power Bank 2, Laptop 1, CCTV Camera 2, Saa ya Ukutani 1, Subwoofer 1 na mashine ya kuhesabia hela 1 ambavyo walipora katika matukio mbalimbali.

Hata hivyo wakati matukio mbalimbali yakiendelea kujitokeza mkoani humo,mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka ameshaweka wazi waraka unaosomwa makanisani akisikitishwa na matukio yanayofedhehesha mkoa huo huku pia akilaani vitendo vya ukatili vinavyozidi kujitokeza.

Related Posts