Ramovic amtaja anayeipa jeuri Yanga

Ushindi wa mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Bara kwa Yanga tangu ianze kufundishwa na Kocha Sead Ramovic, umewafanya mashabiki wa timu hiyo kupata jeuri ya kurudi  kwenye mbio za ubingwa.

Wakati mashabiki wakipata jeuri hiyo huku wakiishuhudia timu yao ikicheza soka safi la kushambulia bila kuchoka mwanzo mwisho, Kocha Ramovic amemtaja mtu muhimu anayefanya kazi hiyo kwa ufasaha.

Ramovic ambaye katika mechi nne za ligi ameshinda zote dhidi ya Namungo (2-0), Mashujaa (3-2), Tanzania Prisons (4-0) na Dodoma Jiji (4-0), amesema hayo yanayoendelea yamewezekana kutokana na kazi nzuri ya benchi lake la ufundi huku ishu ya utimamu wa mwili ikiwa chini ya kocha wa viungo, Adnan Behlulović.

Behlulović raia wa Bosnia and Herzegovina aliyetambulishwa kikosini hapo Desemba 7, mwaka huu, amechukua nafasi ya Taibi Lagrouni ambaye hajaonekana na timu hiyo tangu Yanga ilipoenda Algeria kucheza dhidi ya MC Alger, Desemba 8 mwaka huu.

“Haya yamewezekana sasa kutokana na kazi nzuri inayoendelea kufanywa kwenye mazoezi ya wachezaji na kocha wa viungo Adnan Behlulovic na wasaidizi wake wengine,” alisema Ramovic.

Ramovic anayehusudu soka la kushambulia kwa kasi muda wote bila ya kuwapa wapinzani nafasi, alisema kwa sasa anaiona timu yake ikielekea katika kiwango anachohitaji ingawa haijafika anakotaka.

“Bado nataka kuona wachezaji wangu wakiwa na njaa zaidi ya ushindi mkubwa kuliko huu wanaoupata kwani wana nafasi ya kufanya hivyo kutokana na ubora walionao. Kilichoongezeka zaidi kwa sasa ni mashambulizi yanayoanzia juu yanayowapa tabu wapinzani wetu,” alisema Ramovic.

Hata hivyo, Yanga bado ina kazi kubwa ya kufanya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kufuzu robo fainali kwani hatua ya makundi tayari imepoteza mechi mbili dhidi ya Al Hilal (2-0) na MC Alger (2-0), sare moja dhidi ya TP Mazembe (1-1) ambapo Ramovic zote amesimamia.

Related Posts