Unguja. Wakati tukielekea katika uchaguzi Mkuu wa 2025, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema sekta ya utalii ndiyo imebeba uchumi wa Zanzibar, hivyo ikitokea ikakosekana amani sekta ya kwanza kuathirika ni utalii.
Hivyo, amewataka wananchi kila mmoja kuepusha chokochoko na vurugu ambazo zitafanya sekta hiyo kudorora.
Ametoa kauli hiyo leo Desemba 27, 2024 alipofungua nyumba za kambi ya kikosi cha kuzuai magendo (KMKM) Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema ukiathirika utalii, utaathirika uchumi wa Zanzibar.
“Sekta hii inachangia asilimia 30 ya pato la Taifa, leo tukiondoa hii asilimia, iwapo amani ikikosekana ikazorota uchumi wetu utaathirika kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo niwasihi ndugu zangu tuendelee kulinda amani wakati tukielekea katika uchaguzi mkuu,” amesema.
Amesema ipo haja ya kuwasaidia viongozi wakuu wanaopambana kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kutekeleza miradi mbalimbali, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuona umuhimu huo.
Akizungumza kuhusu kufungua kambi hizo, Mudrick amesema katika ukanda wa Kusini kunahitaji usalama kwani sekta hiyo inakua kwa kasi.
Soraga amesema zitasadia kuimarisha usalama katika mkoa huo ambao sekta ya utalii inakua kwa kasi.
“Kuwapo kwa kambi hii katika mkoa huu, kutasaidia usalama, kutapunguza magendo na biashara haramu katika bahari yetu vitu ambavyo vinahitaji kulindwa,” amesema.
Amesema askari anaongozwa na misingi ya uzalendo, utii, nidhamu, uadilifu na uwajibikaji, hivyo kambi hiyo itaendelea kuwa kiungo baina ya raia wema na Serikali katika kuhakikisha usalama.
“Ni vyema mkaendeleza ushirikiano na wananchi jirani na siyo vyema kusababisha manung’uniko kwa wananchi wa eneo hilo na Serikali juu ya mambo ambayo hayaendani na maadili ya kazi yenu na sheria za nchi,” amesema.
Akitoa taarifa za kitaalamu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ, Issa Mahfoudh Haji amesema kambi hiyo yenye nyumba saba imegharimu Sh567 milioni.
Amesema kuwapo na mazingira bora ya kazi, kutaboresha utendaji kazi wa vikosi hivyo kutokana ana mazingira wanayowekwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed amesema moja ya kazi kubwa ya KMKM ni kuilinda Serikali hivyo lazima watambue umuhimu huo na kuendeleza uzalendo.
Amesema Kizimkazi inajengwa bandari kubwa, hivyo kujengwa kwa kambi hiyo watahakikisha usalama ambao kwa kiasi kikubwa unategemea milango ya baharini.
Mkuu wa KMKM, Azana Hassan Msigiri amesema kikosi hicho kitaendelea kutii pamoja na kulinda usalama, lakini kitahakikisha miradi kinayopewa kinaitekeleza kwa uaminifu.