Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema vijiji hivyo vya mashariki vilivyochukuliwa ni Ivanivka katika mkoa wa Donetsk, na Zahryzove katika mkoa wa Kharkiv. Taarifa za shirika la Habari la Urusi, RIA zimeinukuu wizara ya ulinzi ya Urusi imesema jeshi limeyaangusha makombora manne aina ya Storm Shadow, yaliyotengenezwa na Uingereza.
Wakati huo huo Ukraine imesema mfumo wake wa ulinzi wa anga umezidondosha ndege zisizo na rubani 13 kati ya 24 za Urusi.
Jeshi la anga la Ukraine limesema ndege 11 zisizo na rubani za Urusi zilipotea bila kusababisha uharibifu wowote. Wachambuzi wa maswala ya kijeshi wamesema Ukraine imekuwa ikitumia vifaa vya vita vya kielektroniki kuzielekeza kwingine au kuzidanganya ndege hizo zisizo na rubani za Urusi.
Soma Zaidi: Urusi yataka ihakikishiwe usalama katika mkataba wa Ukraine
Katika vita hivyo vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, Shirika la kijasusi la Korea Kusini limesema mwanajeshi mmoja wa Korea Kaskazini aliyejeruhiwa na ambaye alitekwa na wanajeshi wa Ukraine amefariki kutokana na majeraha.
Kwingineko Urusi na Ukraine zinaendelea kutupiana lawama kutokana na ndege ya shirika la ndege la Arzebaijan iliyoanguka nchini Kazakhstan.
Mkuu wa shirika la usafiri wa anga la Urusi Dmitry Yadrov, amesema hii leo kwamba ndege zisizo na rubani za Ukraine zilikuwa zinaushambulia mji wa Grozny ulio katika jimbo la Urusi la Chechnia, wakati ndege ya shirika la ndege la Azerbaijan ilipokuwa inajaribu kutua.
Ukraine kwa upande wake imesema Urusi ni lazima iwajibishwe kwa ajali ya ndege ya abiria ya Azerbaijan iliyoanguka.
Naibu Waziri Mkuu wa Kazakhstan, Kanat Bozumbayev, amesema Urusi na Azerbaijan bado hazijawasilisha taarifa kuhusu ajali ya ndege iliyotokea huko Aktau na ametahadharisha juu ya kutoa matamko yasiyo na uhakika.
Soma Zaidi: Wataalamu wa anga wasema mifumo ya Urusi huenda iliiangusha ndege ya Azerbaijan
Kuhusu kutafuta njia za kusimamisha mapigano, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi yake iko tayari kuipokea Slovakia kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani yanayolenga kuvimaliza vita vyake nchini Ukraine.
Putin amewaambia waandishi wa habari kaskazini mwa St Petersburg, kwamba Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico alitoa pendekezo hilo wakati wa ziara yake mjini Moscow Jumapili iliyopita.
Vyanzo:DPATRTRE