Putin aja na mpya vita ya Russia, Ukraine

Rais wa Russia, Vladimir Putin amesema anaamini Mungu yuko upande wa taifa hilo katika mzozo unaoendelea kati yake na Ukraine inayoongozwa na Rais Volodymyr Zelenskyy.

Putin alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada kuhitimishwa kwa Mkutano wa Baraza la Uchumi la Mataifa ya Ulaya na Asia (Eurasia) la SEEC uliofanyika jijini St. Petersburg.

Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na mwandishi wa habari iwapo anaamini mzozo huo utamalizika mwaka 2025 kwa Russia kupata ushindi ambapo alijibu; “Ninaamini katika Mungu na Mungu yuko upande wetu.”

Rais huyo alisema uamuzi wa kumalizika mzozo huo uko mikononi mwa Marekani, pindi itakapokubali kuzileta pande hizo mezani huku akidokeza kuwa isingekuwa kucheleweshwa na Marekani kwa kuifadhiri Ukraine silaha, huenda suala hilo lingekuwa limemalizika.

Alisema kucheleweshwa huko kulipendekezwa na Rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden, mwaka 2021 na kwamba taifa hilo kwa mara ya kwanza lilielezwa kuwa Russia haitokubaliana na hoja ya kusitishwa kwa mapigano hayo.

“Hata sisi tunapambana kuhakikisha kwamba mzozo huu unakoma,” alisema Putin huku akiongeza kuwa lengo namba moja la Russia kwa mwaka 2025 ni kuhakikisha inatimiza ndoto ya kushinda vita hiyo.

“Tunaamini kwamba tutafanikiwa kutimiza ndoto hiyo na kufanikisha lengo kiuchumi pamoja na masuala ya kijamii, kijeshi na kiusalama katika upana wake,” alisema Rais huyo.

Tayari Rais mteule wa Marekani, Donald Trump ametamka wazi nia yake ya kuratibu mazungumzo kati ya pande zote zinazozozana ili kupata mwarobaini wake ndani ya saa chache baada ya kuingia kwake madarakani.

Pamoja na kuwa hajaweka wazi hatua za awali kufikia lengo hilo, Trump anaonekana kuwa na kipaumbele cha kusitisha mapigano kati ya pande hizo kisha hatua nyingine za kupata mwafaka wa maeneo yaliyotwaliwa na Russia zifuate.

Al-Jazeera imeripoti kuwa hadi sasa pande zote mbili hazijakubaliana na suala la kusitishwa kwa mapigano hayo, badala yake kila upande unavutia kwake kwa kushinikiza matakwa yake ndiyo yazingatiwe.

Matakwa ya Russia kwa Ukraine ni pamoja na kumtaka Rais Volodymyr Zelenskyy aitishe uchaguzi wa Rais ili kuruhusu wananchi kumbakisha madarakani kwa sanduku la kura na Ukraine kuachana na mawazo ya kujiunga Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO).

Pia, Russia inaitaka Ukraine kuachana na matumizi ya silaha za Marekani na wanachama wa NATO kushambulia maeneo ya Russia sambamba na kuyatambua maeneo ambayo yametwaliwa kutoka Ukraine kuwa ni rasmi yako chini ya usimamizi wa Russia.

Maeneo hayo ni pamoja na Mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson, Zaporizhia, sehemu ya Pekroviskzi na Crimea ambayo ilitwaliwa na kuingia mikononi mwa Russia tangu mwaka 2014.

Wakati huohuo, Ukraine inaitaka Russia kuyarejesha maeneo hayo ambayo iliyatwaa tangu vikosi vya Russia vianze operesheni zake nchini humo Februari 2022 na kuondokoa vikosi vyake katika mipaka ya taifa la Ukraine.

Vilevile, Ukraine inaitaka NATO kukubali ombi lake kujiunga na jumuiya hiyo, jambo ambalo limekuwa gumu kutekelezwa na wanachama wa NATO kwa hofu ya kuingia vitani moja kwa moja dhidi ya Russia.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts