Mv Serengeti yazama upande Ziwa Victoria, Tashico yasaka chanzo

Mwanza. Meli ya Mv Serengeti imepinduka na kuzama upande moja majini kwenye Bandari ya Mwanza Kusini, ikiwa imefungwa katika gati.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma cha Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) imesema meli hiyo imepinduka na kuzama upande mmoja wa nyuma jana, saa saba usiku.

Mv Serengeti ni meli ya abiria na mizigo inayofanya kazi katika Ziwa Victoria. Meli hiyo, mali ya Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), ilijengwa mwaka 1988 ikiwa na makao makuu yake Mkoa wa Mwanza, Tanzania.

Meli hiyo yenye urefu wa mita 55.6 (futi 182), ina uwezo wa kubeba abiria 593 na mzigo wa tani 350. Iliegeshwa tangu mwaka 2016 ikisubiri kufanyiwa matengenezo, hata hivyo, kwa mujibu wa Tashico, imekuwa ikifanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara.

Tashico imesema inashirikiana na timu mbalimbali za wataalamu kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na wadau wengine katika juhudi za uokoaji.

 “Taarifa rasmi ya chanzo cha Tatizo itatolewa meli hiyo itakapokuwa imeinuliwa na Uchunguzi wa kubaini tatizo utakapokuwa umefanyika,” ilisema taarifa.

Kufuatia tukio hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), Alphonce Sebukoto amesema wamepanga kuzifanyia maboresho ya kisasa meli zao zote ikiwa ni pamoja na kufunga mifumo ya kiusalama, kuweka kamera na vifaa vya tahadhari vitakavyotoa taarifa endapo kuna dalili zozote za hitilafu.

Hatua hiyo ya Tashico inalenga kudhibiti meli zake kupata hitilafu za mara kwa mara na hata kuzama pindi zikiwa zimeegeshwa.

Sebukoto amesema hayo leo, Ijumaa Desemba 27, 2024, jijini Mwanza kufuatia kuzama kwa meli ya Mv Serengeti iliyozama eneo la nyuma, usiku wa kuamkia Desemba 26, 2024.

Tukio hilo la kuzama meli ya kampuni hiyo ikiwa imeegeshwa, ni la pili mwaka huu ambapo Mei 19, 2024, Meli ya MV Clarias, iliyokuwa inafanya safari zake katika Kisiwa cha Goziba, ilizama ikiwa imeegeshwa katika Bandari ya Mwanza Kaskazini baada ya kutoka safari.

Sebukoto amesema meli nyingi za kampuni hiyo ni za muda mrefu na sehemu kubwa zilitengenezwa bila mifumo ya kisasa ya usalama, hivyo katika utengenezaji na uboreshaji unaopangwa kufanyika, wataweka mifumo hiyo.

Amesisitiza kwamba baada ya uchunguzi kufanyika, kama itabainika kuna hujuma zinafanyika, basi Serikali itachukua hatua stahiki kwa waliohusika.

“Tunaamini jinsi tunavyoendelea kuzifanyia matengenezo na kuongeza umakini kwa kutumia mifumo ya kisasa ya usalama, haya matukio baadaye yatabaki kuwa historia,” amesema Sebukoto.

Alipoulizwa kama wanahisi kuna hujuma ikiwa ni miezi saba tangu kuzama Mv Clarias, Sebukoto amesema: “Hilo tukio hatutaki kulisemea sana kwa sababu bado liko kwenye vyombo vya kiserikali kwa uchunguzi, tuna uhakika litakapofikia mwisho litatolewa taarifa stahiki na ikibainika kuna uzembe au kuna hujuma watu, watafikishwa mahakamani,” amesema Sebukoto.

Akieleza tukio la kuzama kwa meli hiyo, Sebukoto amesema usiku wa kuamkia Desemba 26, 2024, walipata taarifa kwamba meli hiyo inaonekana imelalia upande wa nyuma, jambo ambalo ni matokeo ya kuwa maji yameingia ndani ya meli.

Amesema licha ya kuegeshwa muda mrefu tangu mwaka 2016, meli hiyo imekuwa ikikaguliwa na wataalamu mara kwa mara na siku tatu zilizopita kabla ya tukio hilo ilikuwa imetoka kukaguliwa, hivyo, baada ya jitihada za kuinyanyua watafanya ukaguzi kubaini kama ni bahati mbaya au ni hujuma.

“Katika kipindi hiki ambacho ilikuwa imeegeshwa hapo na maji kuingia, ilikuwa ina siku mbili au tatu imetoka kukaguliwa na kuthibitishwa kwamba iko sawa, maana yake ni lazima kutakuwa na chanzo kilichoosababisha kuingia maji na kuipeleka chini upande wa nyuma,” amesema kaimu mkurugenzi huyo.

Amesema shughuli ya kuinyanyua meli hiyo imeanza leo Desemba 27, 2024 na litadumu kwa siku moja, ambapo itaondolewa maji na kupandishwa kwenye cherezo kwa ajili ya kukaguliwa mwili wake wote, kisha kutafuta chanzo kilichosababisha maji kuingia, ndipo watatoa taarifa.

“Tukio hili ni tofauti na lile la Mv Clarias, yenyewe ilikuwa imeegeshwa baada kutoka kwenye safari na tunahisi kulikuwa na utumikaji uliosababisha maji kuingia kwa sababu moja au nyingine, ambapo ilikuja kubainika kwamba matundu maalumu ambayo huruhusu meli kupumua, yalikuwa na upana usio wa kawaida,” amesema Sebukoto.

Kiongozi wa kikosi cha uokoaji wa Zeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Said Sekibojo, amesema jitihada za kuinyanyua meli hiyo zinaendelea na tayari wazamiaji wamefunga nyaya zitakazowezesha kuinyanyua na baada ya hapo uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo utaanza

“Tulipata taarifa na kufika eneo la tukio saa 8 usiku, tukaangalia hali ilivyokuwa, kwa wakati huo kulikuwa hakuna uwezekano wowote wa kufanya kazi kwa sababu tayari ilikuwa imeshafika chini, tunashirikiana na vikosi vingine vya ulinzi na usalama na wazamiaji, kuinyanyua meli na tunatarajia leo meli itanyanyuliwa,” amesema Sekibojo.

Related Posts