Polisi Mbeya yapiga marufuku kulipua baruti mwaka mpya

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limepiga marufuku na kuonya wazazi watakaoshindwa kuwadhibiti watoto wanaojihusisha na ulipuaji baruti kwenye mkesha wa kuaga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025.

Jeshi hilo, pia limewaagiza wenyeviti wa serikali za mitaa kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama na kutoa elimu kwa wazazi kuwa walinzi wa familia zao.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 27, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema yapo malalamiko ya wananchi kuhusiana watoto kuzua taharuki wanapopiga baruti katika makazi ya watu nyakati za usiku, hususani sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.

“Mtoto haruhusiwi kupiga baruti muda wowote ule, ni kinyume cha sheria na wanazua taharuki kwa jamii, wazee na wagonjwa majumbani. Suala hilo tunalifanyia kazi na kutoa maelekezo kwa wenyeviti wa serikali za mitaa,” amesema Kuzaga.

Kuzaga amefafanua kuwa kitendo cha kujihusisha na ulipuaji wa baruti wakiwa na umri mdogo kunawapa uzoefu kwa siku za mbeleni kujitumbukiza kwenye vitendo vya uhalifu, jambo linaloweza kukatisha ndoto zao.

“Ninatoa maelekezo pia kwa askari wa doria kukabiliana na wimbi la watoto mitaani  kujihujisisha na matukio hayo, kuwakamatwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo na kuwakumbusha wazazi kujua wajibu wao kuwasimamia,” amesema Kuzaga.

Amesema katika kuelekea mkesha wa kuaga mwaka 2024 na kukaribisha mwaka mpya 2025, wamejipanga kikamilifu kuhakikisha Watanzania wanasherekea kwa amani na utulivu.

“Tunaendelea na doria za kuimarisha ulinzi katika Mkoa wa Mbeya na tunatahadharisha watu wanaojihusisha na uhalifu kutafuta kazi nyingine au wajisalimishe,” amesema.

Awali, mkazi wa Mbeya, Neema Mulungu alilalamikia taharuki zinazotokana na baadhi ya watoto kupiga milipuko ya baruti na kuomba Jeshi la Polisi kudhibiti ili kulinda hali ya utulivu hususani kwa wazee.

“Kumekuwa na kero kubwa hususani kwa sikukuu ya Krismasi watoto wamepiga baruti tangu jioni ya saa 12:00 jioni hadi saa 3:15 usiku, kimsingi inakera, tunaomba hatua zichukuliwe,” amesema.

Related Posts