Arusha. Sakata la ‘upigaji’ wa Sh200 milioni zinazodaiwa kuchotwa kwenye akaunti ya Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha (Uboja) sasa kutua kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Sakata hilo litafikishwa kwa Rais Samia kupitia kwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM), Mohamed Kawaida kufuatia ombi la Mrisho Gambo, mlezi wa Uboja na mbunge wa Arusha mjini, anayedai kuwa suala hilo limeshindikana kutatulika na watu wa ulinzi na usalama.
Fedha hizo zilizotokana na vyanzo mbalimbali vya fedha za chama hicho ikiwemo ada na michango ya wadau, zinadaiwa kuibiwa kwa nyakati tofauti mwaka 2018 hadi 2021 na waliokuwa viongozi wa umoja huo.
Tuhuma za wizi wa fedha hizo zilianza kuibuliwa mwaka 2022 na viongozi walioingia madarakani baada ya kukuta akaunti hiyo tupu huku wakikabidhiwa nyaraka zilizoeleza kuwepo kwa fedha hizo.
Akizungumza kwenye mkutano wa kawaida wa umoja wa bodaboda jijini Arusha leo, Desemba 27, 2024 kwa ajili ya kupatiwa elimu ya ushirika na mikopo ya jiji, Gambo amesema wahusika hao wanafahamika lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao.
“Watu hawa wanafahamika lakini wameshindwa kupatikana kuchukuliwa hatua za kisheria na sisi tumelalamika kila ngazi ya vyombo vya ulinzi na usalama na bungeni. Juhudi za kuwapata zimekuwa ndogo, sasa tunaomba ufikishe kwa Rais kupitia vyombo vyake, naye atusaidie watu hawa wapatikane,” amesema Gambo.
“Uzuri ushahidi upo kwa waliochukua fedha hizo, tena kwa kitambulisho cha Nida na wako hai, lakini hakuna hatua madhubuti zimechukuliwa dhidi yao, sasa nikuambie tu kuwa kilio kimetuzidi kimo na umri, tunaomba fikisha kwa Rais, atusaidie kupitia vyombo vyake. Waliokula hizo fedha wakamatwe na kama kuna mali walizonunua, wafilisiwe,” amesema.
Mbunge huyo wa Arusha mjini ameahidi kutoa Sh1 milioni kwa mwanachama yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa watu hao.
Akizungumzia suala hilo, Kawaida ameahidi kulifisha jambo hilo kwa Rais Samia huku akiwataka waendesha bodaboda hao kuendelea kufuata sheria za barabarani ili kuiheshimisha kazi hiyo.
Mbali na hilo alifanikiwa kuzindua mfumo wa kidigitali wa usajili wa wanachama wa madereva bodaboda ndani ya Jiji la Arusha.
Akitoa risala ya umoja huo, Katibu wa Umoja wa Bodaboda wa Jiji la Arusha, Richard Maghembe amesema lengo la mkutano huo ni kupata elimu ya kuanzishwa kwa ushirika wa umoja wao, sambamba na kupata fursa za mikopo kutoka halmashauri ya Jiji la Arusha.
Amesema changamoto kubwa waliyonayo kwa sasa ni mtaji wa Sh10 milioni kwa ajili ya kuanzisha chama chao cha ushirika, ili kusaidia kiuchumi wanachama wao zaidi ya 12,500.
“Tunaomba Serikali ipunguze gharama za kukata leseni kwa wanachama kutoka Sh70,000 ya sasa hadi Sh30,000 ili kusaidia wengi kumudu,” amesema.
Kawaida ameukabidhi umoja huo Sh10 milioni zilizotolewa na Rais Samia kwa ajili ya mtaji wa kuanzisha chama chao cha ushirika pamoja na pikipiki mbili kwa ajili ya kusaidia kuzunguka kwenye vituo na mitaani kusikiliza kero zao na kuziwasilisha serikalini.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Gambo ametoa Sh10 milioni ili kuutunisha kwa ajili ya kuanzisha chama cha ushirika.