YANGA imerudi kwa mshambuliaji wa Ghana aliyekuwa katika hesabu tangu msimu uliopita, huku Singida Black Stars ikiwa tayari kwenye mazungumzo naye.
Mshambuliaji huyo anakumbukwa zaidi alipokutana na Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita hatua ya makundi akifunga bao katika sare ya 1-1 akiwa na Medeama ya Ghana kabla ya kucheza jijini Dar es Salaam na timu hiyo kupasuka mabao 3-0, huku akilimwa kadi nyekundu dakika ya 90.
Mwanaspoti liliwahi kuripoti juu ya Yanga kuwa katika mazungumzo ya kumsajili Jonathan Sowah dirisha kubwa mwaka huu kwa mkopo akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya ambako ana mkataba wa miaka miwili akitokea Medeama.
Ilielezwa kuwa kama dili hilo lingetiki, basi kibarua cha aliyekuwa mshambuliaji wa yanga, Joseph Guede na Kennedy Musonda kingekuwa matatani, lakini lilikwama. Wakati huo Yanga ilikuwa chini ya kocha Miguel Gamondi, lakini sasa yupo Saed Ramovic huku washambuliaji Kennedy Musonda, Clement Mzize na Prince Dube wakionekana kuwaka ukilinganisha na msimu ulivyoanza.
Rekodi zinaonyesha msimu huu licha ya kuwa Al-Nasr, lakini Sowah hajacheza kabisa, huku uliopita akicheza miezi sita na kufunga mabao saba katika michuano ya ligi.
Inaelezwa Yanga imeanza kumpigia hesabu wakati huu, huku Singida nayo ikitajwa kutaka kumvuta kusaidia katika kikosi hicho kilichoachana na Guede kiliyemsajili kutoka Yanga aliyoitumikia miezi sita.
Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa Sowah zinasema Yanga na Singida zote zimeanza kumfuatilia mchezaji huyo ili kumvuta nchini kutoka Libya.
“Alishakubaliana kila kitu na Singida, lakini ilibaki kusaini tu, ila Yanga wameibuka juzi wakimtaka, hivyo lolote linaweza kutokea kwani mchezaji mwenyewe hatamani kusalia Uarabuni,” kilisema chanzo cha karibu na mchezaji huyo.
Hata hivyo, kubanwa kwa mkataba alionao na kasi iliyoonyeshwa na washambuliaji waliopo katika timu hizo ni wazi vinampa ugumu Sowah kutua iwe Yanga au Singida na hata akifanikiwa kutua itabidi afanye kazi ya ziada mbele ya Mzize, Dube na Musonda na kule Singida kuna Elvis Rupia, Victorien Adebayor na Mohammed Camara.