KAMA we’ ni shabiki wa Simba na ulikuwa na mawazo huenda kiungo Fabrice Ngoma anaweza kuondoka hivi karibuni, basi sahau kwani nyota huyo kutoka DR Congo bado yupo sana na kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids ameweka bayana mbinu alizotumia kumtuliza fundi huyo wa mpira.
Awali, kulikuwa na tetesi kwamba Ngoma hana furaha Msimbazi na alikuwa akifikiria kuondoka dirisha dogo la usajili ikielezwa pia mabosi walikuwa wakimlia taimingi kabla ya kumtosa, lakini upepo umebadilika baada ya kuonekana kuwa lulu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Mbali na kuwa nyota muhimu wa kikosi cha kwanza, pia amekuwa akivaa kitambaa cha unahodha anapokosekana Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ licha ya Shomary Kapombe kucheza naye pamoja, na kocha Fadlu amefichua kwamba amempandisha cheo kuwa nahodha msaidizi wa timu hiyo.
Ngoma ameitumikia Simba chini ya makocha wanne tofauti kuanzia Roberto Oliviera ‘Robertinho’, Juma Mgunda, Abdelhak Benchikha na sasa Fadlu, ambaye ndiye anayeonekana kumkubali zaidi licha ya kuanza vibaya msimu kiasi cha kuibua tetesi kwamba anaweza kuondoka dirisha dogo.
Ghafla Ngoma alibadili ramani na kuwa bora zaidi, jambo lililomshawishi kocha anayemtumia kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na hata kumchezesha eneo la beki wa kati kabla ya kuteuliwa kuwa nahodha msaidizi akimsaidia Tshabalala, na kumchomoa kiaina Kapombe aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kitambo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema amempa kiungo huyo unahodha akiwa msaidizi wa Tshabalala na amefanya hivyo kutokana na nidhamu na uzoefu alionao.
Fadlu alisema Ngoma amekuwa msaada kwa wachezaji wenzake hasa kama ushauri, lakini mwenyewe amekuwa na nidhamu karibu kila maeneo kwenye kambi na hata mechi zao. “Ni wazi kuwa kiwango cha mchezaji huyu kimebadilika zaidi lakini namna yake ya maisha nje na ndani ya uwanja kimekuwa cha tofauti jambo ambalo limemfanya awe kiongozi kabla hata sijamteua. Nidhamu ya mchezaji ni suala muhimu kuliko vyote kwa sababu mtu wa aina hiyo ni mwepesi hata kufundishika, kwani ni haraka kwake kutii na kuelewa mafundisho, na hili ndilo lilitokea kwa Ngoma kwa hiyo najivunia,” alisema Fadlu.
Kukubalika kwa Ngoma mbele ya Fadlu kumpa uhakika kiungo huyo kusalia ndani ya kikosi na kufuta uwezekano wa kuondoka kutokana na kile kinachosemwa na Msauzi huyo.
Katika mechi zote za Kombe la Shirikisho Fadlu amempanga staa huyo kikosi cha kwanza na kuweka rekodi ya kucheza dakika 270, hivyo unaweza kusema ameshiriki mwanzo mwisho. Katika ligi amecheza mechi 11 akitumia dakika 757 alizofunga mabao mawili.