Gusa achia Yanga… Ina mambo matatu!

HUKO kitaani kwa sasa mashabiki wa Yanga wameanza kunenepa kwa furaha kwa aina ya soka linalopigwa na nyota wa timu hiyo maarufu kama ‘Gusa Achia Twende Kwao’ ambalo siku za karibuni limezitesa timu pinzani katika mechi za Ligi Kuu Bara, huku kocha wa timu hiyo, Sead Ramovic akifichua siri tatu za soka hilo.

Kocha huyo aliyeiongoza Yanga katika mechi nne mfululizo za ligi na kushinda zote, huku tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika ikipoteza mbili na sare moja, lakini soka inalopiga kwa sasa limefanya mashabiki kuwa na mzuka  kwenda uwanjani kwa jinsi wachezaji wanavyotengeneza mashambulizi na kuwabana wapinzani mwanzo mwisho na Ramovic amesema soka hilo mambo matatu.

Ramovic alisema falsafa ya soka hilo inabebwa na viungo wenye uwezo wa kutimiza majukumu matatu ya kucheza kwa kasi, nidhamu na ufundi mkubwa mwanzo mwisho.

Kocha huyo aliyejiunga na Yanga hivi karibuni kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyetimuliwa baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za ligi mbele ya Azam na Tabora United, ametokea TS Galaxy ya Afrika Kusini na akizungumzia falsafa hiyo alisema inabebwa zaidi na viungo ambao ni uti wa mgongo wa mfumo wa 4-2-3-1.

Ramovic alisema eneo hilo ndilo msingi wa mafanikio ya timu hivi karibuni na viungo wamekuwa wakitekeleza majukumu kwa viwango cha juu, jambo lililompa urahisi wa kuanzisha mtindo wa kucheza soka la kisasa linalojikita kwenye pasi nyingi za haraka.

“Eneo la kati limebeba timu kwa ujumla kukiwa hakuna nguvu kubwa hapo ni rahisi timu kukosa mawasiliano. Ninafurahia ubora wa wachezaji nilionao sio tu kati, hata  maeneo mengine,” alisema.

Akitolea mfano alimtaja Khalid Aucho – kiungo mkabaji aliyemwelezea kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kusoma mchezo, kuzuia mashambulizi na kusukuma mpira mbele kwa ufanisi.

Aucho ameonekana kuwa mhimili wa nidhamu na uongozi ndani ya uwanja akisaidia timu kudhibiti mchezo dhidi ya wapinzani wao. 

Ramovic pia aliwatambua viungo wengine kama Mudathir Yahya ambaye amekuwa akitoa msaada  kiufundi na kuhamasisha mashambulizi kutoka katikati ya uwanja, kadhalika akimtaja Duke Abuya aliyemsifia kwa kasi na ubunifu akionekana kuwa mmoja wa wachezaji wanaoweza kubadili mchezo. Pia kuna Salum Abubakar ‘Sure Boy,’ aliyetajwa kuwa kiungo mwenye nidhamu kubwa, uwezo wa kutuliza mchezo na akili ya kiufundi.

 Ramovic alifafanua: “Viungo wa kati wanacheza nafasi mbili muhimu za kuimarisha ulinzi na kushambulia. Hivyo ni muhimu zaidi katika nafasi hizo kuwa na wachezaji wenye utimamu mkubwa.”

Mfumo huo, kulingana na Ramovic umeleta uwiano mzuri kwenye timu akisisitiza viungo wamekuwa wakizingatia maelekezo ya kiufundi.

Alisema falsafa yake inalenga kushinda mechi na  kuhakikisha timu inacheza soka la kuvutia.

Ramovic ameiongoza Yanga katika michezo saba – tatu za Ligi ya Mabingwa na nne za Ligi Kuu ambapo ilipoteza dhidi ya Al Hilal (2-0) na MC Alger (2-0) na sare dhidi ya TP Mazembe (1-1) zote zikiwa Ligi ya Mabingwa Afrika kisha ikashinda nne za ligi dhidi ya Namungo (2-0), Mashujaa (3-2), Prisons (4-0) na Dodoma Jiji (4-0).

Timu hiyo kesho itashuka kwenye Uwanja wa KMC Complex, kuikabili Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku kwa sasa ikiwa nafasi ya pili na alama 36 baada ya mechi 14 wakati wapinzani wao hao wapo nafasi ya sita.

Related Posts