Wanajeshi wa Israel wavamia na kuchoma hospitali Gaza – DW – 28.12.2024

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, moto uliteketeza maeneo kadhaa ya Hospitali ya Kamal Adwan, ikiwemo maabara na idara ya upasuaji. Jeshi la Israel lilidai kuwa hospitali hiyo ilikuwa ikitumiwa na wapiganaji wa Hamas kama kituo cha operesheni zao, lakini halikutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo.

Wakati huo huo, jeshi hilo lilieleza kuwa moto mdogo ulizuka katika jengo tupu la hospitali lakini halikujua chanzo chake. Tukio hili limeongeza hali ya wasiwasi na machungu kwa wakazi wa Gaza, ambao tayari wanakabiliwa na mateso makubwa kutokana na vita vya muda mrefu.

Ripoti kutoka Wizara ya Afya ya Gaza zinaonyesha kuwa zaidi ya Wapalestina 45,400 wameuawa tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas. Zaidi ya nusu ya vifo hivi ni wanawake na watoto, hali inayozidisha machungu katika jamii ya Gaza.

Vita hivi vilianzishwa na Hamas mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya shambulio lao kusini mwa Israel ambalo liliua watu takriban 1,200 na kuwachukuwa mateka watu 250.

Hadi sasa, mateka 100 bado wanashikiliwa Gaza, ingawa ni theluthi mbili tu ya idadi hiyo wanaoaminika kuwa hai. Hali hii imezidi kuibua maswali kuhusu mustakabali wa ukanda huo na mateso yanayoendelea.

Ua wa Ukanda wa Gaza katika Hospitali ya Kamal Adwan huko Beit Lahia baada ya shambulio la anga la Israeli
Wapalestina wakitembea kati ya vifusi kufuatia shambulio la Israeli kwenye ua wa Hospitali ya Kamal Adwan na majengo yanayozunguka Beit Lahia, Gaza mnamo Desemba 25, 2024.Picha: Khalil Ramzi Alkahlut/Anadolu/picture alliance

Familia nyingi zilizokimbia makazi yao Gaza zinakabiliana na hali mbaya ya maisha wakati wa msimu wa baridi. Katika kambi za muda kando ya ufukwe wa Deir al-Balah, wakazi wanajitahidi kukabiliana na baridi kali na mazingira magumu.

Soma pia: Israel inaendeleza vita vyake dhidi ya wanamgambo katika Ukingo wa Magharibi

Hema zao zimejengwa kwa turubai na vitambaa vilivyoshikiliwa kwa kamba na mbao, ambazo hazitoi ulinzi wa kutosha dhidi ya upepo mkali wa bahari.

Muhammad al-Sous, mkaazi wa kambi hiyo, alieleza kuwa watoto wake wanakusanya chupa za plastiki kwa ajili ya kuzichoma ili kupata joto. Watoto watatu walifariki wiki hii kutokana na baridi, huku daktari mmoja pia akiripotiwa kufariki kutokana na hali mbaya ya mazingira. Familia nyingi zinategemea msaada wa majirani kwa mavazi na chakula kidogo walichonacho.

Wahuthi, Israel washambuliana

Waasi wa Huthi wa Yemen walifyatua kombora kuelekea Israel Ijumaa asubuhi, saa chache tu baada ya Israel kufanya mashambulizi makali ya anga katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sanaa.

Jeshi la Israel lilisema kuwa kombora hilo lilikamatwa kabla ya kuingia eneo la Israeli, huku tahadhari za mashambulizi ya anga zikitolewa katika maeneo kadhaa ya kati ya Israel.

Waasi wa Houthi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Israel, wakiyaelezea kama njia ya mshikamano na Wapalestina wa Gaza.

Aidha, mashambulizi ya hivi karibuni yanajumuisha kushambulia meli katika njia ya bahari ya Red Sea, huku Houthi wakisisitiza kuwa mashambulizi yao hayataisha hadi Israel itakapositisha mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza.

Yemen Sanaa 2024 | Majengo yaliyoharibiwa katika uwanja wa ndege baada ya shambulio la anga la Israel
Watu wakitembea karibu na majengo yaliyoharibiwa ya Uwanja wa Ndege wa Sanaa, kufuatia shambulio la anga la Israeli huko Sanaa, Yemen, Desemba 27, 2024.Picha: Khaled Abdullah/REUTERS

Mashambulizi ya anga ya Israel yaliyalenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sanaa nchini Yemen, yakisababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine 40.

Soma pia: Israel na Wahouthi washambuliana kwa makombora

Uwanja huo wa ndege ni mojawapo ya miundombinu muhimu katika mji mkuu wa Yemen na hutumiwa kwa safari za kibinadamu na abiria wa kawaida.

Israel ilidai kuwa mashambulizi hayo yalilenga miundombinu inayotumiwa na waasi wa Houthi, ambao wamekuwa wakifyatua makombora kuelekea Israel.

Hata hivyo, mashambulizi hayo yamesababisha madhara makubwa kwa miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na kuharibu mfumo wa urambazaji wa ndege na jengo la abiria.

Maandamano Yemen kya mshikamano na Gaza

Maelfu ya watu walikusanyika mjini Sanaa, Yemen, kushiriki maandamano makubwa ya mshikamano na Wapalestina wa Gaza. Maandamano haya, yanayoongozwa na waasi wa Houthi, yalijumuisha kuchoma bendera za Israel na Marekani huku washiriki wakipaza sauti za kupinga mataifa hayo.

Waandamanaji walibeba bendera za Palestina, Lebanon, na Yemen, pamoja na mabango yanayokemea uvamizi wa Israel Gaza. Waasi wa Huthi wamekuwa sehemu muhimu ya vita vya Mashariki ya Kati, wakishirikiana na vikundi vingine kama Hezbollah na Hamas katika kile kinachoitwa “Mhimili wa Upinzani” unaoongozwa na Iran.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limekosoa vikali mashambulizi ya Israel katika sekta ya afya ya Gaza. Mashambulizi haya, yanayojumuisha hospitali na kliniki, yameathiri vibaya uwezo wa huduma za afya katika eneo hilo.

Maandamano ya wafuasi wa Wahuthi mjini Sanaa.
Maandamano ya wafuasi wa Wahuthi mjini Sanaa.Picha: Mohammed Mohammed/Xinhua/picture alliance

Wakazi wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na dawa muhimu. Hali hii imefanya idadi ya vifo na majeruhi kuongezeka, huku juhudi za kibinadamu zikiwa na changamoto kubwa katika kufikia walioathirika.

Syria waandamana kuunga mkono umoja wa kitaifa

Wananchi wa Syria walikusanyika katika miji kadhaa, ikiwa ni pamoja na Damascus, Hama, Daraa, na Homs, wakidai umoja wa kitaifa dhidi ya migawanyiko ya kimadhehebu.

Maandamano haya yalifanyika baada ya sala za Ijumaa na yaliwaleta pamoja watu wa madhehebu mbalimbali wakihimiza mshikamano wa kitaifa.

Familia za waliopotea wakati wa utawala wa Bashar al-Assad pia zilijitokeza, zikidai majibu kuhusu wapendwa wao waliopotea. Hali ya mshikamano imekuwa muhimu baada ya kuondolewa kwa utawala wa Assad, huku hofu ya migawanyiko ikitanda.

Related Posts

en English sw Swahili