Bao sasa kuchezwa kila mkoa

KATIKA kuhakikisha mchezo wa bao unachezwa kila kona ya nchi, chama cha mchezo huo Tanzania (Shimbata), kimepanga kuanzisha mashindano ya kila mkoa kuanzia mwakani.

Mchezo wa bao ni moja ya michezo ya jadi iliyoasisiwa miaka mingi iliyopita na ulikuwa ukipendwa kuchezwa na Rais wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na ulikuwa ukitumiwa katika ukombozi wa nchi kwa wazee waliokuwa wakikutana jioni kuucheza wakihamasishana.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Shimbata, Rashid Kayombo, alisema lengo la mashindano hayo ni kutafuta washiriki watakaoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia yajayo.

“Sisi kama Shimbata tumedhamiria kuunda timu kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa ambazo zitashindana kwa lengo la kupata washindi wa jumla watakaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa yajayo,” alisema Kayombo na kuongeza;

“Tunataka kufanya hivi kwa sababu tumejifunza katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika Khazakhstan ambayo walienda watu wachache akiwamo na rais mwenyewe, kutokana na maandalizi finyu.”

Katika mkutano huo, Shimbata iliiomba serikali kusaidia matibabu ya Rais wa chama hicho, Monday Likwepa aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kutokana na matatizo ya moyo tangu Jumanne ya wiki hii.

Kwa mujibu wa Kayombo, rais huyo wa Shimbata alianza kuugua mara tu baada ya kurudi nchini akitokea Khazakhstan alikoenda kwa ajili ya kushiriki mashindano ya dunia ya mchezo huo Oktoba mwaka huu.

“Tumeona pia tufikishe ujumbe kwa umma, wadau wa mchezo wa bao hapa Tanzania wajue, pia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aone na aangalie namna ya kumsaidia katika gharama za matibabu, kwa sababu Monday ni mmoja wa walioitangaza nchi vyema.”

Related Posts