NA BALTAZAR MASHAKA, MISUNGWI
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendesha ukaguzi wa magari ya abiria mkakati wa kudhibiti ajali na uvunjaji wa sheria za barabarani zinazofanywa na madereva.
Ukaguzi huo ulifanyika 27 Disemba 2024 ,katika eneo la Usagara, Wilaya ya Misungwi, umelenga magari yanayosafiri mikoani ili kuzuia ajali zinazotokana na uzembe wa madereva na pia, kuhamasisha abiria kuchukua hatua dhidi ya vitendo viovu vinavyofanywa na madereva hao mabasi.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Mwanza, Mrakibu wa Polisi (SP) Sunday Ibrahim, amesimamia ukaguzi huo amechukua hatua za kisheria dhidi ya madereva wa mabasi yaliyobainika kukiuka taratibu .
Pia, amewaelimisha abiria kuhusu haki zao na kuwataka kutofumbia macho vitendo vya uvunjaji sheria vinavyofanywa na baadhi ya madereva, badala yake wawe na ujasiri wa kutoa taarifa kwa polisi.
SP Sunday amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani halitasita kuchukua hatua dhidi ya madereva wanaovunja sheria na kusababisha ajali,aliwataka wamiliki wa mabasi kutimiza masharti, kanuni, na taratibu zinazotakiwa kisheria.
Katika ukaguzi huo, magari mawili yamepatikana na makosa ya kuendeshwa na dereva mmoja badala ya wawili, wamiliki wao walichukuliwa hatua za kisheria kwa kushindwa kuajiri madereva wawili kwa mabasi yanayosafiri umbali mrefu wa zaidi ya saa nane,inavyohitajika kisheria.
Ukaguzi huo wa kushtukiza uliofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza umeleta matokeo chanya kwa kuongeza usalama barabarani na kuhimiza utii wa sheria, huku abiria na madereva wakipongeza kuwa ni juhudi muhimu za kuzuia ajali.
Adha, abiria wamejitokeza kutoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kwa kufanya ukaguzi wa kushtukiza, wamesema kuwa vitendo vya uvunjaji sheria vinavyofanywa na madereva husababisha hatari kwa maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Miongoni mwa abiria hao Donald Chakachaka,amesema; “Zoezi linalofanywa na Jeshi la Polisi ni kwa ajili ya usalama wetu sisi wananchi, sio vyema na haiwezekani gari la mwendo mrefu likawa na dereva mmoja.”
Abiria mwingine, Mwajuma Hamisi, amesema: “Nimelipokea zoezi hili kwa mikono miwili kwa sababu linatusaidia sisi wasafiri kutuepusha na ajali, hivyo nawapongeza polisi wako sawa.”
Naye Hassan Maneno, dereva wa kampuni ya mabasi ya Nyehunge, ameeleza kuwa vitendo vya uvunjaji sheria za usalama barabarani vimepungua mkoani Mwanza kutokana na madereva kujitambua na kutii sheria.
Ameongeza; “Hakuna zile vurugu za kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, tunazingatia mistari sana sana, kwa hiyo nawapongeza sana askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani kwa kazi nzuri wanayofanya.”