KIUNGO mshambuliaji wa Asec Mimosas, Serge Pokou ameomba rasmi kuondoka klabuni hapo huku akihusishwa na Simba inayoelezwa inampigia hesabu kali.
Fundi huyo wa mguu wa kushoto ambaye aliwahi kuifunga Simba hapa nchini wakati timu hizo zilipokutana Ligi ya Mabingwa alisema ingawa ana ofa nyingi lakini amevutiwa na ofa ya Tanzania.
“Nina ofa nyingi ikiwemo moja ya hapo Tanzania, lakini bado sijajua wapi nitakwenda ingawa napenda kuja kufanya kazi Tanzania, kuna marafiki zangu hapo wananiambia namna ligi ya huko ilivyo na ushindani,” alisema Pokou.
“Nimewaomba viongozi wa klabu wasiniwekee ngumu katika kuondoka, nafahamu hii ni timu ambayo inapenda kuuza wachezaji wake Ulaya, napenda kwenda huko lakini nani anajua ni lini ofa kama hiyo itakuja?”
Wakati Pokou akiyasema hayo, kocha wake Jullie Chevalier alisema kiungo huyo uamuzi wa kuondoka kwake unategemea na uongozi wa klabu yao endapo timu inayomtaka itawafuata kwa kuwa bado amesalia na mwaka mmoja.
“Serge (Pokou) ni mchezaji mzuri, nadhani kama atataka kuondoka itategemea na ofa ambayo itakuja kwa uongozi wa klabu, kwa kuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja hapa, ingawa sijawahi kuona viongozi wanazuia mchezaji akitaka kuondoka,” alisema Chevalier