Hamdi arithi mikoba ya Aussems Singida BS

MABOSI wa Singida Black Stars wamemalizana na Kocha Miloud Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, ili kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mbelgiji Patrick Aussems aliyeondoka Novemba 29, mwaka huu.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zililiambia Mwanaspoti kuwa, mazungumzo na kocha huyo mwenye Leseni A ya UEFA yamefanyika kwa ufanisi na walikuwa katika hatua ya mwisho ya kusainishwa mkataba wa miezi sita, ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja kama atakuwa na ufanisi.

“Ni kweli mazungumzo yameenda vyema na tupo hatua ya mwisho ya kumsainisha mkataba, kama kila kitu kitaenda sawa hususani suala la maslahi. Mkataba tutakaompa utakuwa ni wa hadi mwisho wa msimu na iwapo atafanya maajabu, ataongezewa mwingine wa mwaka mmoja,” kilisema chanzo hicho kilichorudi baada ya kuthibitisha kocha huyo ameshasainishwa mkataba wa kuinoa timu hiyo.

Hata hivyo, uongozi wa Singida ulipotafutwa kwa ajili ya kuzungumzia jambo hilo haukuweza kutoa ushirikiano kwa kile walichodai wako bize na mchezo wa jana wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, uliopigwa kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.

Hamdi aliyezaliwa Juni Mosi, 1971, huku akipenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 katika timu mbalimbali alizofundisha, alikuwa hana timu yoyote tangu alipoachana na Al-Khaldiya FC ya Bahrain, aliyoifundisha Julai Mosi, 2023 hadi Desemba 13, 2023.

Kocha huyo mbali na kuifundisha Al-Khaldiya FC, lakini timu nyingine alizowahi kuzifundisha ni USM Alger na JS Kabylie za kwao Algeria, Al-Salmiya ya Kuwait, Athletico Marseille na ES Vitrolles za Ufaransa na Al-Ettifaq FC (U-23) kutoka Saudi Arabia.

Kutua kwa Hamdi kunamfanya afanye kazi kwa kushirikiana na kocha msaidizi, David Ouma huku kwa aliyekuwa kaimu kocha mkuu, Ramadhan Nswanzurimo anarejeshwa katika nafasi ya mkurugenzi wa ufundi.

Related Posts