Wahamiaji 69 wafa maji wakivuka kwenda Ulaya

Mali. Wahamiaji 69 wamefariki wakiwemo raia 25 wa Mali, kufuatia boti waliyokuwa wamepanda kutoka Afrika Magharibi kwenda Hispania barani Ulaya, kupinduka katika Bahari ya Atlantic upande wa Morocco.

Shirika la Associated Press (AP) limesema jana Desemba 27, 2014 kuwa mamlaka nchini Mali zimethibisha vifo vya raia wake 25 waliokuwa wakivuka kwa kutumia boti hiyo kwenda Kisiwa cha Canal nchini Hispania kupitia Morocco.

Boti hiyo inadhaniwa kubeba wahamiaji 80, ilipata ajali hiyo Desemba 19, 2024 na watu 11 waliokolewa muda mfupi baada ya kuzama kwake.

Mshauri wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali, Doulaye Keita, alipotoa taarifa kutoka Shirika la Associated Press, amesema idadi kubwa ya waathirika wa ajali hiyo, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali, ni wakazi wa Mkoa wa Kayes uliopo mashariki mwa taifa hilo.

Ruti (njia) ya Atlantic ni miongoni mwa njia zinazotumiwa na wahamiaji wengi kutoka mataifa ya Afrika Magharibi wanaojaribu kukimbilia na kutafuta kazi katika mataifa ya Ulaya hususan Hispania.

Takwimu zinaonyesha takriban wahamiaji 41,425 walitua nchini Hispania kupitia Kisiwa cha Canal kati ya Januari hadi Novemba 2024 ikilinganishwa na wahamiaji 39,910 mwaka 2023.

Uhamiaji wa watu hao nchi za Ulaya unatajwa na Umoja wa Mataifa kuwa unachochewa na migogoro inayoendelea katika mataifa ya Afrika Magharibi sambamba na changamoto ya ukosefu wa ajira na mabadiliko ya tabianchi yaliyoathiri uzalishaji mali na chakula hususan ni nchini Mali.

Miongoni mwa maeneo ambayo wahamiaji hao huyatumia kukatiza Bahari ya Atlantic na kuingia Ulaya ni pamoja na fukwe zilizopo nchini Senegal, Gambia, Mauritania na Morocco na njia hiyo inatajwa kuwa hatari kwa usalama wa binadamu kutokana na mawimbi yake kutotabirika.

Kwa mujibu wa Tovuti ya Walking Borders, zaidi ya watu 10,000 wamefariki wakijaribu kuvuka bahari hiyo kuelekea mataifa ya Ulaya mwaka huu. Idadi hiyo inatajwa kuwa kubwa tangu njia hiyo ianze kutumiwa na wahamiaji mwaka 2007.

Katika njia hiyo ya Bahari ya Atlantic, mlango unaoanzia wa taifa la Mauritania, unatajwa kuwa hatari zaidi kwa wahamiaji hao wanaouaga ukanda wa Sahel kutokana na kusababisha vifo vya wahamiaji 6,829 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Hata hivyo, Tovuti ya Walking Borders imekuwa ililaumu kutochukuliwa hatua dhidi ya wahamiaji na kusuasua kwa jitihada za uokozi kuchangia kuchangia ongezeko la idadi ya wahamiaji wanaokufa wakijaribu kuvuka bahari hiyo.

Pia, ililaumu mamlaka za utalawa katika mataifa ya Ulaya na Afrika kuweka mbele sheria za kudhibiti uhamiaji na kutelekeza haki ya kuishi kwa binadamu.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika

Related Posts