Serikali kujenga barabara ya njia sita Mbagala hadi Kongowe

Dar es Salaam. Huenda changamoto ya ajali na foleni inayowakabili watumiaji wa barabara ya Kilwa, eneo la Mbagala Mto Mzinga, ikawa historia baada ya Serikali kutangaza kuanza mchakato wa upanuzi wa barabara hiyo kwa njia sita kuanzia Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe.

Upanuzi huo wa barabara ya njia sita zenye, urefu wa kilomita 3.8, utakwenda sambamba na ujenzi wa daraja la kisasa la Mto Mzinga ili kurahisisha magari kupita kwa ufanisi katika eneo hilo linalokumbana na ajali za mara kwa mara.

Kwa mujibu wa watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kwa sasa wapo katika michakato ya manunuzi itakayokamilika kati ya Januari na Februari 2025 kisha hatua ya kuwasaka wakandarasi watakaotelekeleza ujenzi inafuata.

Walieleza hayo leo Jumamosi Desemba 28, 2024 wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyekuwa akikagua ujenzi wa miundombinu katika wilaya za Ilala, Temeke na Ubungo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta amesema mchakato wa manunuzi ya ujenzi wa barabara hiyo upo katika hatua za mwisho na matarajio ikifika Februari yatakuwa yamekamilika sambamba na mkandarasi atakayetelekeza jukumu hilo.

Bosi huyo wa Tanroads amesema ujenzi daraja la Mto Mzinga unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) iliyotoa Dola za Marekani 70 milioni zitakazoelekezwa katika taasisi hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi huo.

Besta amemwambia Waziri Ulega kwamba watahakikisha wanafanya haraka kukamilisha taratibu za manunuzi ili ikifika Januari 31, 2025 mchakato huo uwe umekamilika, wakishirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam.

“Tutajitahidi kwa kila tunaloweza kuharakisha mchakato huu, kwa kutambua umuhimu hali iliyoko hapa eneo la Mbagala,” amesema Besta.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo amesema eneo hilo litakuwa na miradi miwili ya ujenzi wa daraja na upanuzi wa barabara ya njia sita.

Mkumbo amefafanua kuwa daraja la sasa la Mto Mzinga lina urefu wa mita 45, lakini litakalojengwa litakuwa na urefu wa mita 60 ili kukidhi mahitaji.

“Baada ya kuleta watalaamu na kufanya tathimini, tutajenga daraja la mita 60 na kutakuwa na barabara ya njia sita, mbili za magari kwenda, mbili za magari kurudi na zilizobaki kwa ajili ya mabasi ya mwendokasi.

“Sasa hivi tupo kwenye mchakato wa malipo ya fidia ambao tulitarajia umalizike Desemba 31, 2024, lakini huenda likasogea kutokana na malalamiko na hoja za watu katika kutambuliwa,” amesema Mkumbo.

Mkumbo amesema wametenga Sh12.6 bilioni zinazolipwa kwa ajili ya fidia kwa wananchi ili kupisha mradi wa ujenzi wa njia sita kuanzia Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe.

“Daraja jipya tutakalolijenga litakuwa na nguzo ndogo ndogo 72 kuelekea chini ili kuendana na kasi ya maji yanayopita katika eneo hilo,” amesema Mkumbo.

Kwa upande wake, Waziri Ulega amesema eneo hilo ni sehemu korofi katika Jiji la Dar es Salaam inayosababisha Watanzania wanaotumia barabara ya Kilwa kupata adha kubwa wakifika eneo la Kokoto Mto Mzinga.

“Nimekuja hapa kuleta matumaini ya kwamba kazi inakuja kufanyika eneo hili kwa upanuzi wa barabara sita sambamba na ujenzi wa daraja litakaloondoa kero. Niwaombe watumiaji wa barabara hii kuwa watulivu, muda si mrefu tunakwenda kuanza kazi,” amesema Waziri Ulega.

Waziri Ulega ameuagiza uongozi wa Tanroads kuhakikisha wanawapata wakandarasi wenye uwezo watakaofanya jukumu hilo kwa weledi na sio wale wababaishaji wasiokuwa na uwezo wa kuifanya kazi hiyo.

“Wapo wakandarasi wazuri nchini wenye uwezo wa kusimamimia viwango vya ubora wa miradi hii kwa wakati. Hakikisheni mnapata mkandasi wa maana na hilo mlifanye haraka,” amesema Waziri Ulega.

Kwa upande wake, mbunge wa Mbagala (CCM), Abdallah Chaurembo amesema barabara hiyo ni lango la kuingia Mkoa wa Dar es Salaam kwa watu wanaotokea mikoa ya Kusini, akisema njia hiyo ina muhimu wa kipekee ya kufanyiwa maboresho.

“Tangu niwe mbunge nimewahi kushuhudia vifo vya watu vilivyotokana na magari kushindwa kupanda mlima kwa sababu ya wingi wa foleni. Mimi nimewahi kukwama hapa kwa saa nne kutokana na foleni, hii ni miongoni mwa kero kubwa.

“Kikubwa tunaomba mchakato uharakishwe ili Machi Mosi, 2025 mkandarasi awe eneo la kazi kuondoa changamoto hii ya foleni,” amesema Chaurembo.

Related Posts