Chalamila atoa siku 14 za kukomesha foleni ya malori Ubungo

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa siku 14 kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Tanzania (Tarura) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kufanya marekebisho ya haraka ya barabara inayoelekea bandari kavu ya Ubungo.

Pamoja na hayo, ameiagiza TPA na kampuni ya usafirishaji makontena ya Bravo Group Limited, ndani ya wiki mbili, waweke utaratibu wa magari yanayobeba madini ya shaba kutoingia mjini badala yake yawe na eneo la kusubiri.

Foleni ya malori eneo la Shekilango Ubungo yanayosubiri kuingia bandari kavu ya Ubungo.

Chalamila ametoa maagizo hayo leo Desemba 28, 2024 baada ya kutembelea kampuni hiyo na kujionea foleni ya malori yanayosubiri kushusha madini hayo yanavyosababisha adha kwa wananchi.

“Kumekuwa na foleni kubwa sana inayosababishwa na mambo matatu; mosi, ni wingi wa mizigo, tulikuwa tunaweza kuwa na malori 50 hadi 60 lakini leo tunakwenda malori 120 na hii inaonyesha mizigo imekuwa mingi sana.

“Sasa barabara inayokuja eneo hili inaweza kuchangia kuwa na foleni kubwa, hivyo tumekubaliana Tarura na TPA watatue kero hiyo ili malori yanayoingia katika eneo hili yasizuliwe na ubovu wa barabara,” amesema.

Jambo la pili, Chalamila amesema vifaa vinavyopakia na kushusha makontena ndani ya kampuni hiyo viongezwe pamoja na rasilimali watu ili kuwezesha ushushaji wa mizigo kwa haraka.

Agizo lingine la mkuu huyo wa mkoa, ni malori yote kutopaki katikati ya jiji na kuwekwe utaratibu kuwezesha magari hayo kuingia kwa wito maalumu katikati ya jiji.

“Sasa hivi hakuna huo utaratibu, ndiyo maana wananchi wetu wanapitia changamoto ya kuwahi mapema kutokana na foleni, pia, tumekubaliana kusiwe na mzaha kwenye kazi,” amesema.

Chamila amesema kwa kiwango kikubwa eneo la Ubungo limevamiwa na malori pamoja na mabasi ambayo yalipaswa kupakia abiria Kituo Kikuu cha Mabasi Magufuli.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uendeshaji Kampuni ya Bravo, Bosco Haule amesema changamoto hiyo imejitokeza kutokana na ongezeko la mizigo huku miundombinu ikiwa bado ni ileile.

“Mizigo iliyokuwa ikipita bandari ya Beira sasa inapitia bandari ya Dar es Salaam kutokana na hali ya kisiasa nchini Msumbiji, hii ni fursa kwetu lakini pamoja na kuongezeka miundombinu yetu bado ni ileile,” amesema.

Pamoja na hayo amesema maelekezo ya mkuu huyo wa mkoa watayatekeleza kuondokana na adha iliyopo sasa kwa kushirikiana na TPA.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam Abed Gallus amesema watatekeleza maelekezo hayo ya Mkuu wa Mkoa ya kukarabati kwa haraka barabara ya kuingia eneo la bandari kavu.

“Pia tutashirikiana na halmashauri kutafuta kutafuta eneo la kuweka malori kabla ya kufika hapa, TPA tutaendelea kusimamia shughuli zetu ili kuleta ufanisi wa bandari yetu ya Dar es Salaam,” amesema.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Jaffary Nyaigesha amesema watakaa na TPA pamoja na kampuni ya Bravo kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo ya foleni ya malori.

Amesema Tarura na TPA wanapaswa kuijenga barabara hiyo kwani halmashauri iliomba ijengwe kupitia Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar escSalaam (DMDP) na kuelezwa tayari taratibu za ujenzi zilianza chini ya Tarura na TPA.

Kwa upande wao, madereva ambao hawakutaja kutaja majina yao, wamesema changamoto wanayopitia kutokana na foleni hiyo inawaathiri kiafya na kiuchumi.

“Hapa hakuna choo, hakuna maji na tunalala kwenye magari hela kidogo tunayolipwa, unarudi nyumbani huna kitu, tatizo la foleni hapa ni kubwa tumelalamika kwa muda mrefu,” wamesema madereva hao.

Related Posts